3442; Kadiri inavyohitajika.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kujenga mafanikio yoyote makubwa, kunahitaji mtu uweke kazi kubwa sana.
Kadiri kile unachojenga kinavyopaswa kuwa kikubwa na imara, ndivyo pia kazi inayowekwa inapaswa kuwa kubwa.

Uzuri ni kwamba ukishajenga kitu mara moja, kinaendelea kusimama imara kwa muda mrefu.
Baada ya kukamilisha kujenga huhitaji tena kuendelea kuweka kazi kubwa.
Badala yake unaweka kazi ndogo ya kutunza tu.

Ni kipindi kifupi cha juhudi kubwa sana, kinachofuatiwa na kipindi kirefu cha juhudi za kawaida.
Lakini wengi wamekuwa wanakwama kukamilisha kujenga mafanikio makubwa, kwa kutokuwa tayari kuweka juhudi kubwa kadiri ya inavyojika kwenye huo wakati wa kujenga.

Wapo ambao wanaogopa ule ukubwa wa juhudi zinazopaswa kuwekwa, kwa kuona maisha yao yote yatakuwa ya mateso.
Na hilo linapelekea kubaki na matokeo ya kawaida tu, ambayo yanawatesa zaidi.

Na wapo ambao wanajiwekea ukomo kwenye juhudi kiasi gani waweke. Hawa wakishakadiria kiasi cha kazi ya kuweka, wanakuwa hawapo tayari kwenda zaidi ya hapo.
Wanachoshindwa kujua ni kwamba wakati wa kujenga, huweki kazi uliyopanga wewe kuweka. Bali unaweka kazi inayohitajika kuwekwa, kulingana na matokeo yanayohitajika.

Hupaswi kujiangalia wewe upo tayari kufanya nini, bali unapaswa kuangalia kile unachojenga kinataka nini.
Unalisha kile unachojenga ili kikamilike na siyo kutaka kujisikia vizuri wewe.
Ukiwa unajisikia vizuri wakati wa ujenzi kuna makosa unakuwa unafanya.

Njia ya haraka ya kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako ni kuweka kazi kadiri ya inavyohitajika na siyo kadiri ya unavyotaka au kuweza wewe
Fanya kila kinachohitajika kufanyika ili uweze kupata kile unachotaka kupata.
Hapo utapata kile unachotaka na kunufaika nacho.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe