3443; Ushindi mkubwa sana.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kuna watu ambao wamewahi kuwa kikwazo kwa namna fulani maishani mwako.
Labda ni washindani wako wa moja kwa moja ambao wanachukua rasilimali muhimu kutoka kwako na hivyo kukukwamisha.
Au inaweza kuwa ni mtu ambaye ulitegemea afanye sehemu fulani ili kurahisisha safari yako wewe.
Kwa vyovyote vile, watu wanaokukwamisha wamekuwa hawakosekani kwenye maisha yako.
Na uwepo wa watu hao imekuwa pia ni chanzo cha hasira kwako kutaka kufanya makubwa.
Maana unakuwa na majukumu mawili, kupata unachotaka na kuwaonyesha wanaokukwamisha kwamba unaweza.
Unaweza pia kutamani kuona angulo la wale wanaokukwamisha.
Lakini hicho ni kitu ambacho hata kikitokea hakitakuwa na manufaa kwako.
Huwa wanasema njia bora ya kulipa kisasi ni kupata mafanikio makubwa sana ambayo yanawafunika kabisa wale waliowahi kukukwamisha.
Hilo ndilo unalopaswa kufanya wewe, kuhakikisha unapata mafanikio makubwa sana kiasi kwamba wale wote ambao wamewahi kukukwamisha au kukubeza wajione siyo kitu.
Haipo ndani ya uwezo wako kuwageuza wengine ili kupata matokeo unayoyataka.
Lakini ipo ndani ya uwezo wako kujigeuza wewe mwenyewe na kupata matokeo makubwa sana.
Usiwaombee wengine mabaya, hata kama ni maaduo zako kabisa.
Badala yake weka juhudi kubwa sana kwenye kile unachofanya kiasi cha kuweza kuzalisha matokeo makubwa sana.
Matokeo ambayo ukilinganisha na wengine wanavyopata, wanaonekana kabisa ni kama wanacheza tu.
Wajibu wako mkubwa ni kupata ushindi mkubwa sana kwenye maisha yako, mpaka ushindi wa wengine uonekane ni kama mchezo wa watoto.
Hilo liko ndani ya uwezo wako, lifanyie kazi kubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe