3446; Ni yale yale.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mchezo wa mpira wa miguu ndiyo sehemu ambayo matokeo mabovu huwa hayavumiliwi kwa muda mrefu.
Kama timu haipati ushindi, kazi ya kocha wa timu hiyo inakuwa mashakani.

Pale ambapo timu inashindwa kufanya vizuri kama ilivyotegemewa, kazi ya kocha huwa inaishia hapo.
Cha kushangaza sasa, anapokuja kocha mwingine, haji kuanza upya, bali anaendelea kufanya yale yale ya msingi kabisa.

Kocha mpya atafanya kwa ubora yale yale ambayo kocha aliyeondoka alikuwa anayafanya.
Ni ubora kwenye kufanya ndiyo unaoleta tofauti ya matokeo.

Kwenye biashara, unapata ushindi kwa kufanya kwa ubora wa hali ya juu, yale yale ambayo tayari yamekuwa yanafanyika.
Huhitaji kuja na mapinduzi mapya kabisa kwenye uendeshaji wa biashara.

Kwanza unahitaji mfumo unaoeleza vizuri mambo yote yanayofanyika kwenye biashara na jinsi yanavyofanywa.

Mbili unahitaji kuajiri watu wazuri kwenye kutekeleza mfumo wa biashara kama unavyoelekeza.

Tatu unaweka mauzo kuwa kipaumbeke cha kwanza kwenye biashara. Kila kinachofanyika kinaangaliwa jinsi kinavyokwenda kuathiri mauzo.

Nne unafanya wateja kuwa ndiyo lengo kuu la biashara, hivyo zoezi la kuwatengeneza na kuwatunza ni muhimu.

Tano unakuwa na udhibiti mzuri wa mzunguko wa fedha kwenye biashara. Unahakikisha unajua kila senti inayotoka na kuingia kwenye biashara iko wapi.

Kwa kuyasimamia maeneo ya msingi kama hayo, hakuna namna biashara itashindwa.

Watu huhangaika na mambo makubwa, wakati hayo ya msingi bado wanakuwa hawajaweza kuyasimamia.

Fanya yale yale ya msingi kwa ubora na muda mrefu, ushindi unakuwa wako kwa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe