Habari njema matajiri wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu inayoendeshwa kwa msingi kwamba KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI na kupitia programu hii tunatekeleza hilo kwa vitendo.
Wakati sisi tunapambana kujenga utajiri ili tuweze kufikia uhuru wa kifedha na kuwa huru, kuna wengine wanapambana kutuibia utajiri huo. Hivyo kama hatutakuwa na tahadhari nzuri, tunaishia kupoteza kile ambacho tumekipambania kwa muda mrefu.
Hizi siyo habari mpya kwenye jamii zetu, tumekuwa tunaona watu wanafanya kazi kwa miaka mingi, wanastaafu na kupata mafao, halafu wanaishia kupoteza fedha zote ndani ya muda mfupi kwa sababu ya kutapeliwa au kushauriwa vibaya.
Hatuwezi kuruhusu hilo litokee kwenye hii jamii, ndiyo maana tunapeana maarifa na miongozo sahihi na kuifuata ili tunufaike.

Moja ya vitu vinavyoweza kutusaidia sana kuweza kujenga uwekezaji na kuepuka kuupoteza ni kuzielewa na kuziishi sheria tano za fedha kutoka kitabu maarufu cha fedha binafsi kinachoitwa THE RICHEST MAN IN BABYLON.
Kitabu hiki licha ya kuandikwa miaka mingi na kuwa na misingi sahihi na muhimu kifedha, bado watu wamekuwa wanarudia makosa yaliyokatazwa kwenye kitabu hicho na kuishia kuumia.
Ipo kauli ambayo mwandishi anaieleza kwenye kitabu hicho, anasema; “Mtu akiambiwa achague kati ya fedha na sheria za fedha, atakimbilia kuchagua fedha, ambazo ataishia kuzipoteza kwa sababu hazijui sheria za fedha.”
Sisi kama jamii ya NGUVU YA BUKU tumechagua kuzijua na kuziishi sheria za fedha ili tusipoteze hata senti moja yetu. Nichukue nafasi hii kukukaribisha kwenye kujifunza sheria hizi za fedha na kuziweka kwenye matendo ili kutajirika kwa uhakika.
SHERIA YA KWANZA; KUJILIPA MWENYEWE.
Gold comes easily and in increasing quantity to the person who saves at least 1/10th of their earnings.
Fedha inakuja kirahisi na kwa kuongezeka kwa yule ambaye anaweka akiba angalau moja ya kumi ya kipato chake.
Sheria hii iko wazi, kwa kila kipato unachoingiza, anza kujilipa wewe mwenyewe kwanza kwa kuweka akiba. Unapaswa kuweka hiyo akiba kabla hata hujafanya matumizi yoyote.
Umasikini wa wengi huwa unaanzia kwenye kushindwa kutii sheria hii ya kwanza. Wengi wanatumia kipato chao chote na hata kukopa, kitu ambacho kinawafanya kubaki kwenye hali duni.
SHERIA YA PILI; KUWEKEZA PANAPOZALISHA.
Gold labors diligently and multiplies for the person who finds it profitable employment.
Fedha inamfanyia kazi yule ambaye anaiwekeza mahali ambapo inazalisha.
Kuweka akiba peke yake haitoshi, kwani thamani ya fedha huwa inapungua kutokana na mfumuko wa bei. Ili fedha ikupe utajiri, inatakiwa iwe inakufanyia kazi na kukuingizia faida hata kama umelala.
Wapo ambao wanaweka akiba, lakini hawawekezi na hao wanaishia kubaki chini. Hata kama hawatakuwa na changamoto za kifedha, wanashindwa kujenga utajiri.
SOMA; Jinsi Ya Kufikia Uhuru Wa Kifedha Ndani Ya Miaka 15 Kwa Uwekezaji Mdogo.
SHERIA YA TATU; KUWEKEZA KWA HEKIMA.
Gold clings to the protection of the person who invests their gold with wise people.
Fedha hukaa kwa mtu ambaye anaiwekeza na watu wenye hekima.
Watu huwa wanadhani kutokuwa na fedha ni tatizo kubwa, ila tatizo kubwa zaidi ni pale mtu unapokuwa na fedha na watu wakajua una fedha. Utashauriwa na kila mtu na kudhani ushauri wa watu wote uko sahihi. Hakuna kitu unapaswa kuwa na tahadhari nacho kama ushauri wa wengi kwenye fedha. Unapaswa kufuata ushauri wa watu sahihi, wenye hekima kwenye mambo ya fedha na yale wanayokushauri.
Wengi wanaopata fedha nyingi kwa pamoja wamekuwa wanapoteza zote kwa kufuata ushauri usiokuwa sahihi.
SHERIA YA NNE; USIWEKEZE USIPOPAJUA.
Gold slips away from the person who invests gold into purposes through which they are not familiar.
Fedha humkimbia mtu ambaye anaiwekeza mahali ambapo hapajui.
Kuwekeza kwa kufuata mkumbo imekuwa sababu ya wengi kupata hasara na kupoteza fedha. Watu wakisikia fursa fulani inalipa, wote wanaikimbilia. Wasichojua ni kwamba mpaka unasikia kwamba fursa inalipa, jua umeshachelewa, hiyo hailipi tena.
Ili kutunza fedha yako isipotee, unapaswa kuwekeza maeneo ambayo una uelewa nayo na siyo kufuata mkumbo wa wengine. Pia endelea kujielimisha kwenye yale maeneo unayowekeza ili uendelee kujiamini kupitia uwekezaji.
SHERIA YA TANO; USIWEKEZE KWA TAMAA.
Gold flees the person who tries to force it into impossible earnings
Fedha humkimbia mtu anayejaribu kuiwekeza ili kupata faida kubwa zisizowezekana.
Niambie kama hujawahi kusikia hii; ‘Panda pesa yako hapa, kila mwezi inakua mara mbili bila wewe kufanya chochote. Ukishapanda wewe subiri kuvuna tu.’ Huu ni utapeli ambao umekuwepo tangu enzi na enzi, leo hii upo na hata kesho tuna uhakika utakuwepo. Sababu ni watu kuwa na tamaa ya kupata faida kubwa na haraka.
Wengi sana wamepoteza fedha zao kwa sababu ya hizo tamaa za faida kubwa. Wewe epuka sana hizo tamaa, pale unapoahidiwa faida kubwa, ya uhakika na isiyohusisha wewe kufanya kazi, shtuka haraka sana, unataka kupigwa hapo.
Hizo ndizo sheria tano za fedha ambazo ni moja ya NGUZO ZETU kwenye programu huu ya NGUVU YA BUKU. Zijue, zielewe na zikariri ili usije kupoteza uwekezaji ambao umeufanya kwa muda mrefu.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, jibu maswali yafuatayo kama sehemu ya uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kwenda kufanyia kazi.
1. Andika sheria ya kwanza ya fedha na jinsi unavyoifanyia kazi kwa vitendo.
2. Andika sheria ya pili ya fedha na jinsi unavyoifanyia kazi kwa vitendo.
3. Andika sheria ya tatu ya fedha na jinsi unavyoifanyia kazi kwa vitendo.
4. Andika sheria ya nne ya fedha na jinsi unavyoifanyia kazi kwa vitendo.
5. Andika sheria ya tano ya fedha na jinsi unavyoifanyia kazi kwa vitendo.
6. Karibu kwa maswali, maoni na mapendekezo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya ushiriki wako kikamilifu kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.