Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye kipengele cha #HadithiZaKocha ambapo tunapata hadithi fupi zenye masomo makubwa ya maisha.

Kwenye hadithi ya leo tunakwenda kupata kisa cha mbwa na kivuli. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kuwa na maisha bora.

Mbwa alikuwa na njaa kali na chakula hakipatikani eneo ambalo alikuwepo.

Hivyo akalazimika kuvuka mto na kwenda upande wa pili kutafuta chakula.

Baada ya kuwinda kwa muda mrefu, alifanikiwa kukamata mnyama ambaye angemtosheleza kwa chakula.

Hapo aliamua kurudi kwenye makazi yake ili akafurahie mawindo yake.

Alibeba mnyama aliyemwinda kwa kumshika kwa meno yake. Alipoanza kuvuka mto, aliangalia kwenye maji na kumwona mbwa mwingine naye ameshika nyama.

Aliingiwa tamaa na kuona anaweza kupata nyama aliyobeba mbwa yule. Hivyo akafungua mdomo na kumrukia yule mbwa ili amnyang’anye nyama aliyokuwa nayo.

Mbwa aliishia kujikuta yupo kwenye maji na nyama yake hana tena. Akarudi nyumbani kwa huzuni, akiwa amechoka, mwenye njaa na hana kitu cha kula.

Rafiki, hiyo ndiyo hadithi yetu fupi ya mbwa na kivuli, tafakari kwa kina mafunzo ya maisha unayoyapata hapo kisha shirikisha kwenye maoni hapo chini.

Shirikisha nini umejifunza na unaendaje kutumia kwenye maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimesimulia kisa hicho pia, unaweza kuangalia na kujifunza kisha kushirikisha. Karibu sana.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.