Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Lengo kuu la usakaji kwenye biashara ni kuwafikia wateja kule walipo na kupata njia ya kuwashawishi kuja kwenye biashara. Mahali popote penye watu, pana fursa ya kufanya usakaji. Pia njia zozote zinazotuwezesha kuwafikia watu, ni sahihi kuzitumia kwenye kufikia wateja na kuwashawishi kununua.
Vyombo vya habari vya kuchapa, yaani magazeti, majarida na machapisho mengine ni njia ya kuwafikia wateja ambayo imekuwa inatumika kwa muda mrefu.
Pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea ambayo yanafanya wengi kusoma kidijitali zaidi kuliko kwenye uchapaji, bado machapisho ni njia muhimu ya kutumia kuwafikia wateja.

AINA ZA MACHAPISHO.
Kufikia wateja kwa njia ya machapisho kumegawanyika kwenye aina mbalimbali, kubwa mbili ni magazeti na majarida.
Magazeti huwa habari zake ni za muda mfupi, hivyo huwa yanatoka kila siku au kila wiki. Gazeti linaweza kuwa linasambazwa maeneo mengi au kwenye eneo moja.
Majarida huwa habari zake ni za muda mrefu, hivyo huwa yanatoka kila mwezi mara moja au baada ya miezi kadhaa. Jarida linaweza kuwa la mambo ya jumla au kuwa mahususi kwa vitu vya aina fulani.
Tutajifunza jinsi ya kuchagua gazeti au jarida kwa usahihi ili kuwafikia wengi zaidi.
NGUVU YA MACHAPISHO.
Machapisho bado yana nguvu kwenye kuwafikia wateja kwa sababu;
1. Watu huwa wanakumbuka zaidi vitu ambavyo wamesoma kuliko walivyosikia na kuona tu. Kwa kutumia machapisho ambayo watu wanasoma, unakuwa na nafasi ya kukumbushwa zaidi.
2. Watu bado wana imani kubwa kwenye vyombo vikongwe vya habari kama magazeti na majarida. Hivyo wanaweka uzito kwa taarifa wanazokuwa wamezipata kwa njia hizo.
3. Machapisho mengi yamehamia mtandaoni hivyo kuendelea kuwa njia nzuri ya kuwafikia wateja wengi zaidi.
SOMA; Tumia Watu Wenye Ushawishi Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUPATA MATOKEO MAZURI.
Ili kutumia vizuri machapisho kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kununua, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa;
1. Anza Na Sifa Za Wateja Unaowalenga.
Kabla ya kuweka tangazo kwenye gazeti au jarida ili kuwafikia wateja wengi, unapaswa kuanza na sifa za wateja unaowalenga. Ainisha sifa za hao wateja na jua ni magazeti au majarida ya aina gani wanapendelea zaidi kusoma. Kama wateja wako wanapendelea zaidi michezo, watasoma magazeti ya michezo. Kadhalika kama wapo kwenye taaluma fulani, watasoma majarida ya taaluma husika.
Kwa kuanza na sifa za wateja utajua ni kwa njia ipi unaweza kuwafikia kwa wingi zaidi.
2. Chagua Machapisho Sahihi Yanayowafikia.
Baada ya kuainisha sifa za wateja unaowalenga ndiyo utachagua machapisho ambayo yataweza kuwafikia kwa usahihi. Magazeti na majarida ni mengi, yanayolenga eneo fulani au ya jumla na yanayolenga aina fulani ya taaluma. Chagua machapisho ambayo yanawafikia watu wengi zaidi ili unapoweka tangazo uwe na uhakika wa kuwafikia watu wengi zaidi.
Lengo ni kuwafikia wateja wengi zaidi wajue uwepo wa biashara yako, hivyo unapochagua machapisho ya kutumia, hakikisha hilo linafikiwa.
3. Andaa Tangazo Linalonasa Umakini.
Unapaswa kuandaa tangazo ambalo linanasa umakini wa wateja na kuwasukuma wasome. Kichwa cha habari kinapaswa kuwa kinachomvutia mtu kutaka kujua kilichopo ndani. Maelezo mafupi yanapaswa kumfanya mtu aone kuna kitu kwa ajili yake. Pia kunapaswa kuwa na maelezo ya kuibua tamaa ndani yao na hatua ya wao kuchukua. Ni hatua ya kuchukua ndiyo inawafanya wateja waliolengwa kuifikia biashara na biashara kuweza kuwafikia. Mawasiliano yatakuwa kwenye tangazo ambayo watu watayatumia kuifikia biashara.
Tangazo linapaswa kuwa fupi lakini lenye ushawishi kwa watu kuchukua hatua iliyokusudiwa. Hilo ni muhimu ili kuweza kuwafikia wengi zaidi.
4. Ambatanisha Na Picha Inayowavutia Watu Kuangalia.
Pale unapochukua nafasi kubwa ya kutangaza kwenye gazeti au jarida, ambatanisha picha ambayo inawavutia wateja kuangalia. Kama utatumia picha basi hakikisha tangazo linakuwa la rangi na siyo nyeusi na nyeupe pekee. Tangazo linapokuwa la rangi huwa linawavutia watu wengi zaidi.
Tangazo lenye picha huwa linakuwa na ushawishi zaidi kama linachokua sehemu kubwa ya ukurasa au hata ukurasa mzima. Japo gharama inakuwa kubwa kulingana na ukubwa wa ukurasa uliotumika, ushawishi wake unakuwa mkubwa pia. Matangazo madogo ya gharama ndoto wengi wanaweza kuyaruka, lakini yale yaliyochukua ukurasa mzima na kuwa na mwonekano mzuri, wasomaji wote wa chapisho husika huwa wanayaona.
5. Zingatia Gharama Za Matangazo Na Za Kumpata Mteja.
Gharama za matangazo huwa zinatofautiana kulingana na aina ya chapisho, wingi wa watu ambao wanafikiwa na ukubwa wa tangazo. Kadiri chapisho linavyofikia wengi ndivyo gharama zinakuwa kubwa. Pia kadiri tangazo linavyochukua sehemu kubwa, ndivyo gharama yake inavyokuwa kubwa. Kujua gharama sahihi kuingia, jua gharama ya kumpata mteja kwenye biashara yako haipaswi kuzidi kiasi gani, kisha jua kwa kutangaza unaweza kupata wateja wangapi.
Tangaza pale ambapo gharama utakayotumia kwenye matangazo ipo ndani ya gharama ya kumpata mteja. Kama matangazo ya nafasi kubwa gharama yake ni kubwa kuliko bajeti ya biashara, tumia nafasi ya matangazo madogo madogo (classified ads). Japo inaweza isionekane na wengi, lakini wale wanaoyaona matangazo hayo huwa ni wenye uhitaji hasa kwa sababu wanakuwa wameyatafuta wao wenyewe.
6. Pima Matokeo Unayopata Na Boresha Ili Kufanikiwa.
Unapaswa kupima matokeo unayoyapata kupitia matangazo unayofanya kwa njia ya machapisho na kuboresha ili kufikia lengo la kufikia wateja wengi zaidi. Utaweza kupima vizuri kama hatua ya wateja kuchukua imewekwa inayojitofautisha. Kwa mfano namba ya simu ambayo inatumika kuwa ya tofauti au aina nyingine ya mawasiliano kuwa kwa ajili ya matangazo hayo tu. Au kuwa na neno maalumu ambalo wanaochukua hatua kupitia matangazo hayo ya machapisho wanalitumia ili kupata zawadi au punguzo na ukaweza kujua wangapi wametokea kwenye matangazo hayo.
Ni kwa kupima matokeo ndiyo unaweza kuona fursa za kuboresha zaidi matangazo unayoyafanya kupitia machapisho. Kwa machapisho ambayo yanasambazwa kwa njia ya mtandao, kuwa na kiungo maalumu ambacho wateja wanafungua kuja kwenye biashara ni njia nyingine ya kupima.
Kwa machapisho ambayo yanawekwa kwenye mtandao badala ya kuchapwa, mchakato wake hautofautiani na ule wa machapisho ya kuchapa. Tofauti yake ni umakini wa watu unakuwa mfupi zaidi kuliko kwenye kuchapa. Watu wanapokuwa wanasoma machapisho yaliyochapwa huwa wanakuwa na umakini mkubwa kuliko wakisoma machapisho hayo hayo kwa njia ya mtandao.
Kulingana na aina ya biashara unayofanya na wateja unaowalenga, chagua machapisho ambayo yanawafikia wateja wengi unaowalenga kisha weka matangazo kwenye machapisho hayo. Andaa matangazo yako vizuri ili yawe na ushawishi, yakiambatana na picha na hatua za wateja kuchukua. Pia pima kila tangazo unaloweka ili uweze kuboresha zaidi na kufikia malengo yaliyopo. Hakikisha unatumia gharama sahihi kulingana na matokeo unayopata ili njia hii iweze kuwa na tija kwa biashara.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.