3452; Kujiamini na Unyenyekevu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa huwa ni kitendawili ambacho wengi hawawezi kukitegua.
Ili ufanikiwe, unapaswa kujiamini kupitiliza.
Yaani ujiamini sana, kuliko ilivyo kawaida.
Unatakiwa kujiamini hata kama huna sababu ya kujiamini.
Kujiamini kunahitajika sana kwa sababu mafanikio makubwa siyo rahisi,
Yana vikwazo na changamoto za kila aina.
Kama hujiamini kupitiliza, utakata tamaa haraka na kuishia njiani.
Lakini pia ili ufanikiwe, unapaswa kuwa na unyenyekevu mkubwa.
Unapaswa kujua kuna mengi ambayo hujui na unapaswa kujifunza ili uweze kupiga hatua.
Unatakiwa kukubali kwamba huidai dunia au yeyote chochote.
Ujue chochote unachotaka, unapaswa kukipambania sana ili kukipata.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unyenyekevu unavyopaswa kuzidi.
Kwa sababu mafanikio huleta kiburi na kiburi ndiyo chanzo cha anguko.
Ukiangalia kwa haraka, kujiamini kupitiliza na kuwa mnyenyekevu ni vitu vinavyoonekana kupingana.
Ni kweli kwa juu juu vinapingana, lakini kwa ndani vinaungana.
Wale wanaoweza kuelewa hivyo viwili na kuviishi ndiyo wanaojenya mafanikio makubwa na kudumu nayo kwa muda mrefu.
Huwa kuna kauli inasema; TEMBEA KAMA MUNGU, FANYA KAZI KAMA MBWA.
Tafsiri ni hiyo hiyo, jiamini kupitiliza, lakini pia kuwa mnyenyekevu sana.
Amino unaweza chochote, lakini jua hakuna kitakachokuja kwako kirahisi.
Elewa hilo na umefanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe