Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya kujenga utajiri, uwekezaji ni kiungo muhimu sana.
Watu wengi wamekuwa wanachanganya kipato kikubwa (rich) na utajiri (wealth).
Wengi huwa na maisha mazuri pale wanapokuwa na kipato kikubwa, kinachokuwa kinatokana na kazi au biashara wanazofanya.
Lakini pale kazi au biashara hizo zinapoisha, huwa wanarudi kwenye maisha duni kwa sababu hawakuwa wamefanya uwekezaji wa kuyawezesha maisha yao kwenda.
Na siyo kwamba wengi wanaokuja kuwa na maisha duni baadaye hawakuwa na uwezo wa kufanya uwekezaji. Waliweza sana, lakini hawakuwa na maarifa sahihi ya nini ni uwekezaji na nini siyo uwekezaji.
Kwa mfano, watu wengi huwa wanadhani kujenga nyumba ya kuishi ni uwekezaji, kitu ambacho siyo. Nyumba unayojenga kwa ajili ya kuishi wewe, siyo uwekezaji. Haijalishi unaamini kiasi gani, ukweli ni siyo uwekezaji.

Kabla hujapatwa na hasira, maana ukiwa umeshajenga nyumba ukiamini ni uwekezaji halafu anatokea mtu na kukuambia siyo, hutajisikia vizuri. Tuangalie kwanza maana ya uwekezaji halafu turudi kuiangalia nyumba ya kuishi kama ina sifa hizo.
Uwekezaji ni kitu ambacho kinakuingizia wewe kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Yaani uwe umelala au unafanya mambo yako mengine, kipato kinakuwa kinaingia. Ukishahusika tu kwenye kufanya ndiyo kipato kiingie, tayari hapo siyo uwekezaji.
Tukianza tu na hiyo maana ya uwekezaji, tayari nyumba ya kuishi inakosa sifa.
Twende kwenye utetezi ambao utakuwa nao kwamba nyumba inachangia sehemu ya utajiri wako kwa kuthaminishwa kwake. Ndiyo, hilo ni kweli, lakini je unapanga kuiuza nyumba hiyo ili uvune utajiri huo? Jibu ni hapana, huwezi kuuza kwa sababu ndiyo unaishi.
Utetezi mwingine utakaokuwa nao ni kwamba unaweza kutumia nyumba kupata mkopo ambao utautumia kwa shughuli nyingine za uwekezaji. Hilo ni kweli, lakini huo mkopo utahitaji kuufanyia kazi na kufanya marejesho, kazi lazima iwekwe.
SOMA; Jinsi Ya Kujenga Utajiri Wa Mwendokasi.
Swali ni je watu wasiwe na nyumba? Jibu ni hapana, kuwa na nyumba kulingana na mipango yako. Mimi binafsi nina nyumba na nashauri kila anayeweza awe na nyumba.
Lakini nataka nikupe tahadhari kubwa, kwa thamani ile ile ambayo umewekeza kwenye nyumba yako ya kuishi, hakikisha pia unaiwekeza kwenye maeneo mengine yanayoweza kuzalisha faida bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.
Ninachomaanisha ni kama una nyumba yenye thamani ya milioni 50, basi hakikisha una uwekezaji mwingine wa milioni 50 ambao unakuingizia faida bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Utawekeza wapi hiyo milioni 50 nyingine ni juu yako, lakini muhimu ni uweze kuingiza kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja.
Na kama hujui wapi pa kuwekeza, basi nikushauri uwekeze kwenye masoko ya mitaji, yaani hisa, vipande na/au hatifungani. Huko kunakupa marejesho bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Na japo marejesho yanakuwa madogo, lakini kwa muda mrefu unajenga utajiri mkubwa huku ukiwa unaendelea na mambo yako mengine.
Najua hili ulilojifunza hapa litakufanya usijisikie vizuri, kwa sababu kwa maisha yako yote umekuwa unaaminishwa nyumba ya kuishi ni uwekezaji. Fanyia kazi hili ulilojifunza hapa, kama tayari una nyumba ya kuishi, basi fanya uwekezaji wenye thamani sawa na nyumba hiyo ili ujiweke mahali pazuri.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua zaidi hali hiyo ya nyumba ya kuishi kutokuwa uwekezaji na hatua za wewe kuchukua. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kujiweka vizuri kwenye eneo la fedha.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.