Hisia ni mimemko ambayo binadamu hupata kutokana na mazingira au hali tofauti kulingana na mahitaji yao.
Asilimia zaidi ya 80% ya wateja wananunua bidhaa kwa hisia kuliko mantiki.

Hawanunui kitu kwa sababu ni cha maana sana, kinafanya kazi vizuri sana, ni bora, bali hununua kutokana na hisia walizo nazo kwa wakati huo.
Ndiyo maana machinga wengi hupenda sana kutotoa nafasi ya mteja kufikiri mara mbili.
Wanaamini mteja akiwa wa moto ni rahisi kufanya manunuzi, kuliko akipoa au akitoka katika eneo la biashara.
Ukweli ni kuwa, hisia zikiwa juu kiwango cha kufikiri kinakuwa chini. Kadhalika, hisia zikiwa chini kiwango cha maamuzi kinakuwa juu.
Angalia vitu ulivyonunua kwa akili yako mwenyewe tulivu na vitu ulivyonunua wakati hujatulia vizuri kuna utofauti.
Maeneo ya Kariakoo kuna mteja aliuziwa viatu vya mguu mmoja, baada ya kupanda daladala akili imetulia, anakuta vyote vya mguu mmoja. Akashuka, kurudi, jamaa hayupo. Kweli, mjini shule.
Tuangalie hisia tatu muhimu katika kukabiliana na wateja;
Hisia ya kwanza ni tamaa;
Mfano mzuri upo kwenye michezo ya kubahatisha. Utaratibu wao, ni kumtangaza mshindi akiwa anapewa hela.
Baada ya hapo mshindi hutoa neno namna alivyoshinda. Kwa kuwa pesa ni tamanio la kila mmoja. Washiriki huingiwa tamaa na kucheza.
Kwenye biashara unachofanya ni kuibua tamaa kwa kumweleza faida anazopata kutoka kwenye bidhaa yako.
Pia, unaweza kumpatia ushuhuda, ili aone kuna wateja walionunua kabla yake.
Hisia ya pili ni aibu.
Mfano mzuri ni wa muuza karanga. Hasa pale anapomaliza kukuojesha, wengi wetu tunaona aibu kuondoka bila kununua kidogo.
Hapa unachofanya ni kumpatia mteja mfano au ajaribu. Kama ni nguo, kiatu anavaa. Gari pikipiki au baiskeli anaendesha.
Mwishowe anaona aibu kuondoka bila kununua. Ukifanya kwa wateja 10 ukapata mmoja sio mbaya. Inasogeza mauzo yako. au unakaa na mtu kwa muda mrwfu lazima uwe na aibu kuondoka bila kuchukua kitu…
Hisia ya tatu ni hofu.
Hapa unachozingatia ni kumpatia mteja ofa zenye ukomo na uhaba.
Hivyo, anaona asipochukua atakosa bidhaa husika. Hii inamchochea kuweza kulipia bidhaa.
Kitu muhimu kuzingatia ni usikivu, umakini na fokasi mbele ya mteja. Mpe maelezo katika hali ya utulivu huku ukimpatia nafasi ya kujielezea kuliko kuwa muongeaji.
Hatua za kuchukua leo; Jifunze vema kucheza na hisia za wateja, ili uwahudumia vizuri na kuwashawishi kununua.
SOMA;Ishinde Hofu Leo Kwa Kufanya Hili Zoezi.
Je, ni bidhaa ipi ulinunua ukiwa wa moto au hisia zikiwa juu baadaye ukagundua haikuwa inakufaa kwa wakati huo?
Wako Wa Daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Tanzania.
0767702659 /mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi