Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye kipengele hiki cha #HadithiZaKocha ujifunze kutoka kwenye kisa cha mtego wa nyani.

Mkulima wa shamba la karanga alikuwa akisumbuliwa sana na nyani. Alikuwa nyani mmoja ambaye alikuwa anachimba karanga kila zinapokomaa na kula.

Mkulima alijaribu kila aina ya mitego ya kumnasa nyani lakini yote ilishindwa. Aliweka midoli ya kumtisha nyani huyo ili asile karanga, lakini nyani huyo aliendelea kumtesa.

Mkulima alikata tamaa na kuona kama nyani amemshinda. Siku moja alikutana na mtu ambaye alimwelezea changamoto yake kuhusu nyani kumsumbua kwenye shamba la karanga.

Mtu yule alimwambia ana mtego ambao utaweza kumnasa nyani huyo bila ya shida kabisa. Mkulima alimwambia hadhani kama kuna mtego unaoweza kumnasa nyani, kwa sababu ameshajaribu kila kitu.

Mtu yule alimpa chungu maalumu ambacho kina mnyororo unaofungwa mahali. Alimwelekeza aweke karanga ndani ya chungu hicho kisha kufunga mnyororo kwenye eneo ambalo hauwezi kutoka.

Mkulima alikuwa na wasiwasi, akiona mtego huo ni mdogo sana kuliko mingi ambayo ameshaijaribu. Mtu huyo aliyekuwa anampa mtego aliona wasiwasi wake na kumwambia asimlipe chochote, yeye akajaribu mtego huo kama alivyomwelekeza. Kama mtego utamnasa nyani basi ndiyo atakuja kumlipa, kama hautamnasa basi asimlipe.

Kwa kupewa uhakika huo wa kutokuingia gharama yoyote, mkulima alichukua mtego na kwenda kufanya kama alivyoelekezwa.

Kama kawaida nyani alikuja kwenye shamba lile na kufurahi kuona karanga zimewekwa kwenye chungu. Aliingiza mkono wake kuchukua karanga zile na alipojaribu kutoa mkono kwenye chungu, haukuweza kutoka kwa sababu mdomo wa chungu ulikuwa mdogo huku nyani akiwa ameshikilia karanga kwenye mkono wake.

SOMA; #HadithiZaKocha; Kisa Cha Mbwa Na Kivuli.

Nyani alikazana sana atoe mkono wake kwenye chungu bila ya kuachia karanga alizoshika, lakini hakuweza kuutoa. Aliendelea kuhangaika pale mpaka mkulima akafika na kuweza kumkamata kirahisi kabisa.

Na huo ndiyo ukawa mwisho wa nyani aliyekuwa mjanja na msumbufu sana, aliweza kunasa kwenye mtego ambao ni mdogo sana.

Rafiki, tafakari yale unayojifunza kwenye kisa hicho cha mtego wa nyani na jinsi unavyokwenda kuyatumia kwenye maisha yako ili yawe bora zaidi. Kisha shirikisha kwenye maoni hapo chini hayo uliyojifunza kutoka kwenye kisa hiki.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimesimulia kisa hiki cha mtego wa nyani, karibu uangalie na kuweka maoni yako ya yale uliyojifunza na jinsi unavyokwenda kuyatumia ili kuboresha maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.