Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Lengo kuu la usakaji kwenye biashara ni kuwafikia wateja kule walipo na kupata njia ya kuwashawishi kuja kwenye biashara. Mahali popote penye watu, pana fursa ya kufanya usakaji. Pia njia zozote zinazotuwezesha kuwafikia watu, ni sahihi kuzitumia kwenye kufikia wateja na kuwashawishi kununua.
Vyombo vya habari vya sauti, yaani redio njia ya kuwafikia wateja ambayo imekuwa inatumika kwa muda mrefu. Redio imekuwa njia kongwe na inayoaminiwa na watu wengi kwenye kupata taarifa za mambo yanayoendelea.

NGUVU YA REDIO.
Licha ya redio kuwa ndiyo njia kongwe ya kupata habari na kuja kwa njia nyingine kama TV na mitandao ya kijamii, bado redio imekuwa na nguvu kwenye kuwafikia watu wengi zaidi.
Nguvu hiyo ya redio inatokana na sababu zifuatazo;
1. Uwezo wa redio kuwafikia watu wengi zaidi.
Njia nyingi za habari huwa zina vikwazo kwenye wingi wa watu ambao wanaweza kufikiwa. TV inataka watu wawe na TV ambayo ni gharama kuliko redio. Na mitandao inataka watu wawe na vifaa vinavyoweza kuingia kwenye mitandao. Lakini redio inahitaji kifaa ambacho ni rahisi kwa watu kuwa nacho.
2. Imani kubwa ambayo watu wanayo kwenye redio.
Watu wamekuwa wanategemea redio kwenye kupata taarifa za msingi. Hilo limekuwa linapelekea watu kuamini taarifa wanazopata kupitia redio. Hivyo hata matangazo wanayoyapata kupitia redio, huwa wanayaamini pia.
3. Uwezo wa kurudia rudia kwa muda mrefu.
Watu huwa wanasikiliza redio huku wakiwa wanaendelea na shughuli zao nyingine. Hivyo umakini wao wote unakuwa haupo kwenye kitu kimoja. Kutokana na umakini wa wasikilizaji kutokuwa eneo moja, kitu kinapaswa kurudiwa rudiwa mara nyingi ndiyo watu wakipate. Uzuri ni redio huwa zinarudia rudia vitu mpaka watu kuvipata na kuelewa.
SOMA; Tumia Magazeti, Majarida Na Machapisho Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE MATUMIZI YA REDIO NA SAUTI.
Ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi kwa kutumia redio na sauti, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.
1. Chagua Kituo Na Muda Sahihi.
Vituo vya redio na muda wa matangazo huwa vinatofautiana. Unapaswa kuchagua kituo sahihi ambacho wateja unaowalenga ndiyo wanakisikiliza zaidi. Na kwenye kituo hicho, unapaswa pia kuchagua muda sahihi ambao ndiyo wateja unaowalenga wanasikiliza zaidi.
Hili unapaswa kulijua au kushauriwa vizuri na vituo vya redio unavyokuwa unaongea navyo kabla ya kurusha matangazo.
2. Tangazo Liandaliwe Kwa Usahihi.
Ili taarifa iweze kuwafikia watu na wachukue hatua, tangazo linapaswa kuandaliwa kwa usahihi.
Kwanza tangazo linapaswa kuwa fupi, kati ya sekunde 30 mpaka sekunde 60.
Pili tangazo linapaswa kunasa umakini wa msikilizaji, kugusa maslahi yake, kuibua tamaa na kueleza hatua ya kuchukua.
Tatu hatua za kuchukua zielezwe kwa usahihi na kurudia, mfano kama mteja anapaswa kupiga namba ya simu, basi itajwe kwa usahihi na kwa kurudia.
Kwa kuzingatia hayo kwenye kuandaa tangazo, linakuwa na ushawishi mkubwa.

3. Tangazo Lirudiwe Rudiwe Kwa Muda Mrefu.
Watu huwa wanasikiliza redio wakiwa wanaendelea na mambo yao mengine, hivyo umakini wao wote haupo kwenye kile kinachoendelea kwenye redio. Ili tangazo liweze kuwafikia watu na wachukue hatua, linapaswa kurudiwa rudiwa kwa muda mrefu. Tangazo linapaswa kurudiwa mara nyingi kwenye siku na hata kwenye kipindi na kurushwa kwa siku nyingi.
Wakati mwingine watu wanaweza wasichukue hatua zinazoelekezwa kwenye tangazo, lakini wakawa wamejua kupitia tangazo hilo na kuchukua hatua kwa namna nyingine. Hivyo usiache kutangaza kwa sababu hujaona matokeo kwa haraka.
4. Weka Matangazo Ya Sauti Maeneo Yenye Watu Wengi.
Matangazo ya sauti yanaweza kuwekwa maeneo ambayo yana watu wengi. Mfano kwenye vituo vya usafiri na kwenye vyombo vya usafiri. Ndani ya vyombo vya usafiri tangazo linaweza kuwekwa kwenye redio na watu kusikia. Na kwenye vituo vya usafiri matangazo yanaweza kuwekwa kwenye spika zinazowekwa maeneo hayo na kurudia rudia matangazo hayo.
5. Pima Ufanisi Na Boresha.
Ili kupata matokeo mazuri, lazima uwe unafanya tathmini kwenye kila hatua unazochukua. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye matangazo ya redio na sauti. Pima matokeo yanayopatikana kulingana na hatua zilizochukuliwa. Kisha boresha kulingana na matokeo yanayopatikana.
Maboresho yanayoweza kufanyika ni kuanzia kwenye tangazo lenyewe, pale hatua zinazochukuliwa na wateja walengwa zinapokuwa tofauti na ilivyolengwa. Pia kuboresha maeneo ambayo matangazo yanarushwa na muda wa matangazo pia inaweza kuhitajika kulingana na matokeo yanayopatikana.
Redio na sauti ni njia ya watu kupata habari ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na bado ina nguvu kwenye zama hizi kwa sababu ya uwezo wake wa kufikia wengi zaidi. Kwa kuandaa matangazo kwa usahihi na kuyasambaza kwa njia sahihi inakuwezesha kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kuchukua hatua kitu ambacho kitaleta ukuaji wa mauzo.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.