3459; Uza Mafanikio.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mmoja wetu ni muuzaji.
Kwenye yale tunayofanya kila siku, yakishawahusisha tu watu wengine, tayari hayo ni mauzo.

Kwa sababu mauzo ni kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe.
Unapojihusisha na watu wengine, kuna vitu unakuwa unataka wakupe.
Unapokuwa muuzaji bora, unaweza kuwashawishi wakakupa vitu hivyo kwa namna unavyotaka.

Mauzo hayaishii hapo, bali yanakwenda mpaka ni nini unachouza.
Tunauza vitu mbalimbali, wafanyabiashara wanauza bidhaa na huduma, wataalamu wanauza utaalamu wao na viongozi wanauza sera zao.

Lakini ukija kuchimba ndani kabisa, unagundua wote tunauza kitu kimoja, ambacho ni mafanikio.
Chochote unachowapa watu, utakuwa na ushawishi kwao na kukubalika zaidi kama utawaonyesha jinsi kitakavyowapa mafanikio.

Hiyo ni kwa sababu kila mtu anakazana kuyafanya maisha yake kuwa bora zaidi ya pale yanapokuwa.
Hivyo kama wakiona kupitia kile unachowapa wanaweza kuboresha maisha yao zaidi, watashawishika na kukubali.

Hapa kuna mambo mawili unayopaswa kukubali na kuyaishi ili upate unachotaka.

Moja ni wewe ni muuzaji, hivyo mara zote kazana kuwa bora kwenye mauzo ili uwashawishi wengi na kupata unachotaka.

Mbili ni wewe unauza mafanikio, hivyo kila mara angalia ni namna gani unaweza kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

Uzuri ni kwamba, kila mtu ana kitu anachoweza kuboresha zaidi.
Hata kama mtu amefika juu kiasi gani, bado anaweza kwenda juu zaidi ya hapo.

Wajibu wako ni kuweza kuwaonyesha watu ni juu kiasi gani wanaweza kwenda na wewe unawezaje kuwasaidia kufika huko juu. Hilo litakuwezesha kupata kila unachotaka kwenye maisha yako.

Kuwa muuzaji bora na uza mafanikio, huwezi kushindwa kwenye maisha kama utabobea kwenye hayo mawili.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe