3460; Kujiamini na Kiburi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio yanataka mtu ujiamini kupitiliza. Yaani ujiamini sana, kwa sababu safari ya mafanikio siyo rahisi.

Ni safari iliyojaa vikwazo na changamoto za kila aina, kama mtu utakuwa hujiamini, utakata tamaa haraka na kuacha.

Lakini pia huwa kuna hali ya kiburi ambayo watu huwa wanakuwa nayo kwa kudhani ndiyo kujiamini.
Kiburi ni sumu kubwa ya mafanikio na kimepelekea wengi kupata anguko kubwa baada ya kupiga hatua fulani.

Kuna tofauti kubwa sana ya kujiamini na kiburi ambayo kila anayetaka mafanikio anapaswa kuijua ili asijikwamishe au kuanguka.

Kujiamini ni pale unapokuwa na matamanio makubwa na yenye kusudi, ambayo mtu unayafanyia kazi ukiwa na uhakika kwamba utayafikia.
Hilo linakupa mtu nguvu ya kuendelea kupambana licha ya yale unayokutana nayo.
Kujiamini kunakupa mafanikio.

Kiburi ni pale mtu unapoamini kwamba huwezi kushindwa. Pale unapojiona kama wewe ni maalumu sana kiasi kwamba hakuna kinachoweza kukusumbua.
Kiburi kinakufanya uingie kwenye mambo ambayo huna uelewa nayo na kupata anguko kubwa.
Pia kiburi kinakufanya mtu usiwe tayari kujifunza, kwa kuona tayari unajua kila kitu.
Hilo linapelekea mtu kufanya makosa ambayo yanakugharimu sana.

Umejionea tofauti hapo, kujiamini ni kuamini utafanikiwa na kupambana ili ufanikiwe.
Wakati kiburi ni kuamini huwezi kushindwa na hivyo kufanya mambo yanayokukwamisha kufanikiwa.

Jitathmini uko upande gani, wa kujiamini au kiburi kisha chukua hatua sahihi.
Hilo ni jibu unalojua mwenyewe, maana kwa nje kila anayejiamini anaweza kuonekana ana kiburi.
Ni ndani ya mtu ndipo penye majibu sahihi na kutakapopelekea mtu kufanikiwa au kushindwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe