USIKUBALI KUACHWA NYUMA NA MAPINDUZI HAYA YA KIFEDHA YANAYOKUJA TANZANIA.
Habari njema Matajiri wawekezaji,
Ni nafasi nyingine nzuri kwetu kuendelea kupata masomo ya uwekezaji na kwenda kuyaweka kwenye vitendo ili kujenga utajiri kwa uhakika.
Kama ilivyo kauli mbiu ya programu yetu ya NGUVU YA BUKU, KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu ya mifano halisi iliyopo.
Lakini pia tunapata moyo sana kutokana na mwenendo uliopo na viashiria vya yale yajayo.
Ni ukweli usiopingika kwamba eneo la fedha, hasa uwekezaji kwenye masoko ya mitaji linapitia mapinduzi makubwa kwa sasa.
Kwa muda mrefu ushiriki wa watu kwenye uwekezaji wa masoko ya mitaji umekuwa chini.
Watu wamekuwa wanaamini zaidi kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo kwa kuona ni salama zaidi.
Uwekezaji kwenye masoko ya mitaji umekuwa unaoneokana ni hatari na wenye faida kidogo.
Pamoja na ukweli kwamba uwekezaji kwenye ardhi ni salama zaidi na uwekezaji wa masoko ya mitaji kuwa na faida ndogo, bado uwekezaji kwenye masoko ya mitaji ni muhimu.
Hiyo ni kwa sababu uwekezaji kwenye masoko ya mitaji unampa mwekezaji ukwasi, yaani urahisi wa kupata fedha pale unapokuwa na uhitaji nazo.
Imekuwa ni jambo la kusikitisha sana watu unakuta wana uwekezaji wenye thamani zaidi ya bilioni kwenye ardhi na majengo, lakini wakipata shida ya milioni 10 hawawezi kuipata kwa haraka.
Hiyo ni kwa sababu uwekezaji kwenye ardhi na majengo siyo rahisi kuugeuza kuwa fedha taslimu kwa haraka pale unapotaka.
Kutokana na elimu zinazoendelea kutolewa, kumekuwa na mwamko mkubwa wa watu kuwekeza kwenye masoko ya mitaji kitu ambacho kinaonyesha ishara nzuri.
VIASHIRIA VYA MAPINDUZI YA KIFEDHA TANZANIA.
Kumekuwa na viashiria vya mapinduzi mazuri ya kifedha hapa Tanzania. Baadhi ni kama ifuatavyo;
1. Ongezeko la makampuni kwenye soko la hisa la Dar es salaam (DSE). Soko la hisa la Dar halina miaka mingi lakini limeweza kuwa na makampuni 28. Miaka ya karibuni makampuni mapya kama 5 yameingia sokoni. Makampuni mengi zaidi, hasa ya kampuni za simu yanatarajiwa kuingia kwenye soko. Hivyo fursa zaidi za uwekezaji kupatikana.
2. Ongezeko la hatifungani nyingi, kuanzia za serikali kuu, mabenki na manispaa. Hatifungani hizo zimekuwa na hatari ndogo kwenye uwekezaji.
3. Ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji. Kwa muda mrefu tumekuwa na taasisi moja tu inayotoa mifuko ya pamoja, ambayo ni UTT. Lakini kwa sasa mifuko mingine miwili imeshaandikishwa ambayo ni FAIDA FUND na TIMIZA FUND. Hii inaleta uwanja mpana zaidi wa uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja.
4. Uwepo wa soko la bidhaa (mercantile exchange) ambapo bidhaa mbalimbali za mazao zinauzw na kununuliwa kama sehemu ya uwekezaji. Hii inatoa fursa ya watu kutawanya uwekezaji wao.
5. Ongezeko la bima za maisha zenye mipango mizuri. Kipindi cha nyuma bima ya maisha ilikuwa inaitwa BIMA YA KIFO, kwamba unakata bima hiyo ili ukifa wategemezi wako wapate fidia. Hii ilifanya mapokeo yake yasiwe mazuri, kwa wengi kuona kukata bima hiyo ni uchuro. Lakini kwa sasa bima za maisha zimeboreshwa na zina manufaa mengi na siyo mpaka kifo. Bima za maisha zimekuwa sehemu ya uwekezaji ambao unampa mtu manufaa pamoja na chanzo cha kipato pale kipato cha mtu kinapoathiriwa kwa namna yoyote ile.
Maeneo hayo matano, ambayo ni baadhi tu ya mengi yanayoendelea, ni kiashiria kizuri cha mapinduzi ya kifedha Tanzania.
HAKIKISHA HUACHWI NYUMA.
Mapinduzi ya aina yoyote ile huwa yanazalisha watu wa aina mbili.
Moja ni wale wanaonufaika na mapinduzi na mbili ni wale wanaoachwa nyuma na mapinduzi.
Ili unufaike na haya mapinduzi, zingatia yafuatayo;
1. Jifunze kuhusu uwekezaji kwa msimamo na mwendelezo. Kila siku jifunze kitu kuhusu uwekezaji na kamwe usijione umeshajua kila kitu. Jifunze bila kuacha kwa sababu mabadiliko ni makubwa na yanaendelea.
2. Fanya uwekezaji kwa muda mrefu na msimamo bila kuacha. Kujifunza pekee haitoshi, ni lazima ufanye uwekezaji kwa vitendo ili kunufaika.
3. Chagua uwekezaji wako mkuu ambao ndiyo utakaoubobea kwenye kujifunza na kuufanya. Hakikisha uwekezaji huo uliouchagua unaujua kwa kina na kuufanya kwa manufaa makubwa.
4. Chagua uwekezaji wako mbadala ambao utaufanya ili kutawanya hatari ya kutokuweka mayai yako kwenye kikapu kimoja. Jifunze pia kuhusu uwekezaji huo na ufanye kwa mpango utakaokuwa nao.
5. Kaa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU bila kutoka. Kwenye programu hii unajifunza na kuambatana na wengine kwenye safari ya uwekezaji hivyo kupata moyo wa kuendelea.
6. Ingia kwenye programu ya UHURU WA KIFEDHA pale unapokuwa umeshafanya uwekezaji mzuri na unataka kupiga hatua kubwa zaidi. Kwenye programu hiyo unaongozwa kufanya uwekezaji mkubwa zaidi na wenye faida kubwa zaidi.
Tuzingatie hayo ili tunufaike na mapinduzi haya ya kifedha yanayoendelea hapa Tanzania.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo ushirikishe uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Taja viashiria vya mapinduzi ya kifedha Tanzania.
2. Ni uwekezaji upi mkuu uliouchagua kwako na unahakikishaje unajifunza na kufanya kwa msimamo bila kuacha?
3. Ni uwekezaji upi mbadala uliochagua kufanya ili kupunguza hatari? Ni kiasi gani cha uwekezaji unafanya kwenye uwekezaji huo mbadala?
4. Unahakikishaje unakaa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU kwa msimamo bila kutoka au kukosa nafasi?
5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na ushuhuda kutokana na somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Tuma majibu ya maswali hayo kama sehemu ya mjadala wa somo na kuthibitisha kusoma, kuelewa na kwenda kuweka kwenye matendo.
Kutoka kwa rafiki yako, Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
NGUVU YA BUKU,
Kila Mtu Anaweza Kuwa Tajiri.
