Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Muda ni moja ya rasilimali muhimu sana kwenye maisha yetu. Ni kupitia muda ndiyo tunaweza kufanya na kupata yote tunayoyataka. Tunachoweza kusema ni kwamba muda ndiyo maisha yenyewe.
Lakini pia muda ndiyo rasilimali yenye uhaba mkubwa. Muda ukishaenda haurudi tena na ukipoteza muda huwezi kuupata tena. Jinsi tunavyotumia muda wetu inachangia kufanikiwa au kushindwa kwenye yale tunayofanya.
Pamoja na umuhimu mkubwa wa muda na uhaba wake, watu wengi wamekuwa wanatumia muda wao kwenye mambo yasiyokuwa na tija. Wamekuwa wanawapa watu muda wao na kujinyima wao wenyewe muda huo ambao wanauhitaji sana.

Ili kuwa mtu bora na hatimaye kuwa muuzaji bora, tunapaswa kuwa na usimamizi na udhibiti mzuri wa muda wetu. Na hilo linaanza kwa mtu kutenga muda kwa ajili yako mwenyewe.
Unaweza kusema kwani muda wote si wako? Ndiyo unaweza kusema muda wote ni wako, lakini jinsi unavyoutumia huwa ni rahisi kuwapa wengine na kujinyima wewe mwenyewe.
Hivyo ili kuhakikisha kweli unanufaika na muda wako, unapaswa kuwa na mpango wa makusudi wa kutenga muda kwa ajili yako mwenyewe. Huo ni muda ambao unautenga kwenye siku yako, ambapo humpi mtu mwingine yeyote nafasi isipokuwa wewe mwenyewe.
Unaweka kabisa miadi ya kukutana na wewe mwenyewe kwenye muda huo na kuhakikisha hakuna kinachoingilia na kuvuruga ratiba hiyo ya kuwa na mkutano na wewe mwenyewe.
Muda mzuri wa kutenga muda kwa ajili yako ni asubuhi na mapema kabla siku haijaanza au usiku kabla ya kumaliza siku yako. Japo upo huru kutenga muda kwa ajili yako kwenye muda wowote wa siku yako.
Kiasi cha muda wa kutenga kwa ajili yako pia kinategemea na mtu mwenyewe, lakini kwa wastani, saa moja kwenye masaa 24 ya siku inapaswa kuwa ni kwa ajili yako.
SOMA; Tumia Muda Wako Vizuri.
Ukishaweka utaratibu wa kuwa na muda wako mwenyewe, kuna mambo ya msingi unayopaswa kuyafanya kwenye muda huo. Mambo makubwa kabisa ambayo hupaswi kuacha kuyafanya kwenye muda wa peke yako ni NDOTO, TATHMINI na KUJIBORESHA.
Muda unaotenga kwa ajili yako unapaswa kuutumia kwa ajili ya kujikumbusha NDOTO kubwa ulizonazo kwenye maisha yako. Jikumbushe maono makubwa uliyonayo, sisitiza kusudi la maisha yako na andika malengo makubwa unayoyapambania. Kwa kujikumbusha haya ya msingi unaendelea kuyafanyia kazi bila kuacha.
Unapaswa kutumia muda kwa ajili yako kujifanyia TATHMINI ya mambo yote unayoyafanya. Unajipima kwa kule ulikotoka, ulipo sasa na unakokwenda. Unapima yale yote unayoyafanya, kwa juhudi unazoweka na matokeo unayopata. Kwa kulinganisha matokeo unayopata na yale unayotaka utaweza kuona ni maeneo gani ya kuboresha ili kupata matokeo bora zaidi.
KUJIBORESHA ni zoezi endelevu ambalo unapaswa kulifanya bila ukomo. Kwenye muda unaotenga kwa ajili yako, unapaswa kuendelea kujiboresha wewe mwenyewe. Unaboresha akili yako kupitia usomaji na kujifunza, unaboresha roho kwa kusali na kutahajudi. Pia unaboresha afya yako kwa ulaji sahihi, kufanya mazoezi na kupumzika.
Kupata muda imekuwa ni kitu kigumu sana kwenye zama hizi ambazo mambo ya kufanya ni mengi lakini muda ni mchache. Namna pekee ya kupata muda kwa ajili yako ni kuutenga mapema kabisa na kutoruhusu uingiliwe na kitu chochote. Tenga muda huo kwenye nyakati ambazo usumbufu wa wengine siyo rahisi, asubuhi na mapema au usiku sana ni muda mzuri.
Kwa kuwa umekuwa unawapa wengine muda wako, hakikisha na wewe pia unajipa muda kwa ajili yako na kuutumia kujikumbusha NDOTO zako kubwa, KUJITATHMINI kwenye yale unayofanya na KUJIBORESHA ili uweze kufika kule unakotaka kufika. Muda wako ndiyo maisha yako, utumie vizuri ili uweze kujenga maisha unayoyataka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.