3466; Ni rahisi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanaona hatua za kujenga biashara zinazowapa mafanikio na utajiri ni ngumu.

Wamekuwa wanaangalia vitu ambavyo wamejaribu kufanya na kushindwa huko nyuma, kisha wanahitimisha kwamba mafanikio kwao ni magumu.

Ukweli ni kwamba, kujenga biashara inayokupa mafanikio na utajiri ni rahisi.
Mchakato huo una hatua tatu za msingi kabisa.

Hatua ya kwanza ni kujua tatizo ambalo watu wanalo na wapo tayari kulipia kulitatua.
Watu wana matatizo mengi na kati ya hayo wana ambayo wapo tayari kulipa fedha ili kuyatatua.
Hayo yanaweza kuwa ndiyo muhimu zaidi au yanayowaumiza zaidi.
Kwenye hatua hii unaweza kuanza hata wewe mwenyewe, kwa kutatua tatizo ambalo limekuwa kinakusumbua zaidi na upo tayari kulipia suluhisho lake.
Hapo ukijua kama ni kitu kinachokusumbua wewe, kitakuwa kinawasumbua na wengine pia.

Hatua ya pili ni kutatua tatizo ulilochagua. Hapo ndipo penye kazi yenyewe, kwa sababu unapaswa kuwapa watu suluhisho ambalo ni bora kabisa na hawawezi kulikataa au kusubiri.
Kwa maneno mengine ni unawapa watu thamani ambayo hawawezi kuikataa, kwa sababu hawajawahi kuipata mahali pengine popote.
Wape watu matokeo ya uhakika ambayo hawajawahi kuyapata na hawawezi kusubiri bali kuyapata mara moja.

Hatua ya tatu ni kuifanya kazi kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.
Mafanikio na utajiri ni kitu kinachojengwa kwa muda mrefu wa kuweka juhudi bila kuacha.
Watu wengi huwa wana mtazamo wa mafanikio ya haraka na matokeo yake wamekuwa wanajikuta wakipoteza hata kidogo wanachokuwa wamepata.
Ukishapata kanuni inayofanya kazi, kinachobaki ni wewe kukifanyia kazi bila kuacha.
Tatua tatizo ulilochagua kwa ukubwa na ubora ili wengi zaidi kupata suluhisho na wewe kunufaika zaidi.

Hizo ndizo hatua tatu ambazo mtu yeyote akizifanyia kazi kwa uhakika, lazima apate mafanikio na utajiri anaoutaka.
Ni kutatua tatizo ambalo watu wanalo na wapo tayari kulilipia kisha kuweka kazi kubwa kwa muda mrefu.

Usijihangaishe na njia za mkato za kupata mafanikio na utajiri.
Maana njia hizo matokeo yake yamekuwa hayadumu.
Fuata njia sahihi na jipe muda, utaweza kupata chochote unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe