Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Lengo kuu la usakaji kwenye biashara ni kuwafikia wateja kule walipo na kupata njia ya kuwashawishi kuja kwenye biashara. Mahali popote penye watu, pana fursa ya kufanya usakaji. Pia njia zozote zinazotuwezesha kuwafikia watu, ni sahihi kuzitumia kwenye kufikia wateja na kuwashawishi kununua.

Televisheni na Video ni moja ya njia zinazotumika kufikisha habari na burudani kwa watu wengi. Watu huwa wanafuatilia maudhui yanayotolewa kwa njia ya TV na video. Na kwa zama hizi, siyo lazima mpaka mtu awe kwenye TV ndiyo aweze kuona maudhui, bali kwa kutumia simu na vifaa vingine, watu wanaweza kufuatilia maudhui mbalimbali yanayotolewa kwa mfumo wa video.

NGUVU YA VIDEO.

Video zina nguvu kubwa ya kuwafikia na kuwashawishi watu wengi, hasa kwenye zama hizi ambazo mambo mengi yapo kidijitali.

Nguvu ya video kwenye kuwafikia watu wengi inatokana na sababu zifuatazo;

1. Umakini wa watu kwenye video.

Tofauti na njia nyingine za kutoa maudhui, video zinataka mtu aweke umakini wake wakati wa kufuatilia. Kwenye sauti mtu anaweza kusikiliza akiendelea na mambo mengine, hivyo umakini wake wote unakuwa haupo pale. Kadhalika kwenye kusoma, mtu anaweza kukatisha na kwenda na mengine. Ila kwenye video, mtu analazimika kuweka umakini wake kwenye kile anachotazama ili kuelewa. Hilo linafanya ujumbe kufika kwa uhakika na kuwa na ushawishi.

2. Kuona kunaaminisha zaidi.

Watu wanaposikia kitu huwa hawaamini kama wanapoona kitu hicho. Video inatoa fursa kwa watu kujionea wenyewe kuhusu kitu husika. Kitu kikielezewa tu kwa maneno, kinaweza kisieleweke. Lakini kitu hicho hicho kikionyeshwa kwa vitendo, kinaeleweka na kuwa na ushawishi. Video inatoa fursa ya kuonyesha vitu kwa vitendo.

3. Kuwezekana kwenye vifaa vingi.

Video zinaweza kuangaliwa kwenye vifaa vya aina nyingi, kuanzia tv, kompyuta na simu za mkononi. Pia video zinaweza kusambazwa kwa kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii. Hayo yote yanafanya usambaaji wa video kuwa rahisi na kwa ukubwa zaidi.

4. Mitandao inatoa kipaumbele.

Mitandao mingi ya kijamii kwa sasa inatoa kipaumbele kikubwa kwenye video, hasa ambazo ni fupi fupi. Pale video inapowavutia watu wengi, inazidi kuonyeshwa kwa walio wengi zaidi. Video vinazoandaliwa vizuri zina nafasi ya kusambaa kwa kasi kubwa kwa sababu ya mitandao kutoa kipaumbele kwenye video.

5. Urahisi wa kutangaza.

Kuandaa matangazo kwa njia ya video ni rahisi kutangaza kupitia televisheni na mitandao mbalimbali. Kuna mitandao ambayo inabeba video peke yake, kama youtube, lakini karibu mitandao mingine yote inaruhusu video. Kwa nafasi hiyo kubwa ambayo video zinapewa, ni rahisi kutangaza kwa kutumia video kuliko njia nyingine. Matangazo pia yanakuwa ya gharama rahisi pale mitandao inapotumika.

Kwa jinsi njia hii ya TV na Video ilivyo na nguvu, kila biashara na kila muuzaji anapaswa kutumia njia hiyo kuwafikia watu wengi zaidi.

SOMA; Tumia Redio Na Sauti Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA TV NA VIDEO KUFIKIA WATU WENGI ZAIDI.

Ili kutumia televisheni na video kuwafikia watu wengi na kuwashawishi kuwa wateja wa biashara, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.

1. Video za matangazo na za maudhui.

Ili kuwafikia wengi na kuwashawishi, unapaswa kuandaa video za aina mbili. Moja ni matangazo, hayo yanakuwa mafupi na yenye hatua za watu kuchukua moja kwa moja. Mbili ni maudhui, hapo video zinatumika kufikisha maudhui yenye elimu mbalimbali. Kwa watu kujifunza kupitia video, huwa wanaamini na kuwa rahisi kushawishika kwenye mambo yanayoendana na masomo haya.

Hatua ya kuchukua; andaa video za matangazo na maudhui na uwe unazisambaza kwa watu wengi zaidi. Hilo litajenga ushawishi mkubwa kwa wale wanaofikiwa.

2. Video ziwe kwenye ubora wa hali ya juu.

Watu wanaangalia video pale inapokuwa na ubora wa hali ya juu. Video zilizoandaliwa kwa ubora, kwenye picha na sauti huwa hazichoshi kuangalia. Mpangilio wa video nzima unapaswa kuwa ambao unawafanya watu washawishike kuendelea kuangalia bila kuacha.

3. Kuwepo kwa matukio yanayonasa umakini wa watu.

Ubora wa video ni jambo jingine, matukio yaliyopo kwenye video husika ni jambo jingine muhimu zaidi. Iwe ni video ya tangazo au maudhui, kunapaswa kuwa na matukio ambayo yanawafanya watu waache mengine wanayokuwa nayo na kupeleka umakini wao wote kwenye kile wanachoangalia. Kwenye tangazo hili ni muhimu zaidi, kwa sababu watu wameshajifunza kuruka matangazo au kutokuyasikiliza kabisa. Lakini pale kunapokuwa na matukio ya kuvutia, watu wanaweka umakini wao wote kwenye matukio hayo.

4. Kutumia mitandao na vipindi vyenye wateja walengwa kwa wingi.

Njia kuu mbili za kufikia wengi kwa video ni televisheni na mitandao ya kijamii. Kote, mpango sahihi unapaswa kuwekwa ambao unahakikisha mitandao inayotumika ni ile yenye walengwa kwa kiasi kikubwa. Kadhalika kwenye vipindi vya televisheni, kituo na muda vinapaswa kuzingatiwa ili kufikia watu sahihi na kuwashawishi kuwa wateja.

5. Kulipia matangazo ya video ili kuwafikia wengi.

Video zinapokuwa za maudhui, zinaweza kusambaa kwa wengi kama zina vitu vya tofauti na vinavyovutia. Pamoja na hilo, bado matokeo yanaweza yasiwe mazuri sana. Hivyo inahitajika njia ya kuwafikia wengi iwezekanavyo kwa njia ya video. Na hapo ndipo matangazo ya kulipia ya video yanapokuwa na umuhimu. Matangazo ya video yanapolipiwa, iwe ni kwenye TV au mitandao ya kijamii, inawafikia wengi zaidi. Kwa majukwaa yote ambayo unayatumia kuwafikia wengi kwa video, hakikisha unalipia matangazo ili kuwafikia wengi zaidi.

Video ni njia yenye nguvu ya kuwafikia wengi na kuwashawishi kuwa wateja. Ni rahisi kwa kila biashara na kila muuzaji kuwafikia wengi kwa video, hasa urahisi ulioletwa na mitandao ya kijamii. Tumia njia ya video kuweza kuwafikia wengi zaidi na kuwashawishi kwa ukubwa kupitia maonyesho unayoweza kufanya kwa kutumia video.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.