3467; Umewafundisha wewe mwenyewe.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Chochote ambacho watu wanakufanyia, ni wewe mwenyewe umewafundisha wafanye hivyo.
Watu hawawezi kukufanyia kitu chochote ambacho hujawaruhusu na kuwafundisha jinsi ya kukifanya.
Wanachokifanya watu kwako, wanaanza kwa kuiga vile unavyojifanyia wewe mwenyewe.
Watu wakikudharau, ni kwa sababu wewe mwenyewe unakuwa umejidharau.
Hakuna anayeweza kukudharau kama wewe mwenyewe hujidharau na kuwaruhusu wengine nao wakudharau.
Watu wanaiga mfano wako mwenyewe kwenye kila wanalofanya kwako.
Na kama hakuna mfano, wanajaribu halafu wanaangalia unapokeaje kile walichofanya.
Ukikubaliana na walichofanya, wanaendelea kufanya.
Lakini kama hutakubaliana na walichofanya, hawatafanya tena.
Hiyo ndiyo maana ni muhimu sana mtu uweke mipaka mapema kwenye kila eneo la maisha yako.
Mipaka hiyo inaeleza wazi nini unakubaliana nacho na nini hukubaliani nacho.
Unaweka mipaka kwa sifa ambazo unakuwa umejijengea kwa watu wengine. Kile ambacho umekuwa unafanya au kukubaliana nacho, ndiyo watu watafanya kwako pia.
Unajenga sifa kupitia uadilifu wako. Yale ambayo unayafanya kwa msimamo bila kuacha, ndiyo yanakuwa sifa yako. Sifa haitokani tu na maneno, bali matendo yako.
Uadilifu wako unajengwa na kujiheshimu kwako mwenyewe. Pale unapopanga kitu na kisha kupanga kama ulivyofanya ni kiashiria cha kujiheshimu wewe mwenyewe. Kama unapanga kitu halafu hukifanyi, unakuwa hujiheshimu wewe mwenyewe. Na kama hujiheshimu wewe mwenyewe, wengine pia hawakuheshimu.
Unajiheshimu pale unapokuwa na viwango vyako binafsi na kuvisimamia mara zote bila kuvunja viwango hivyo. Watu hawatasikiliza viwango vyako, bali wataangalia jinsi unavyosimamia viwango hivyo. Kama unafuata viwango vyako mara zote, watu pia wanajisukuma kuvifikia viwango hivyo. Lakini kama utavunja viwango hivyo, watu hawataviheshimu.
Hayo yote yanaleta kwenye hitimisho kwamba watu wataheshimu yale unayoheshimu wewe na kudharau unayodharau.
Wewe ndiye unayewafundisha na kuwaruhusu watu wafanye yale wanayokufanyia.
Kama kuna namna huridhiki na vile watu wanakuchukulia au kukufanyia, tambua ni wewe mwenyewe umesababisha yote hayo.
Unaweza kuchukua hatua sahihi na kubadili chochote ambacho hukubaliani nacho kwako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe