3468; Maamuzi Magumu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni ugumu.
Pale mambo yanapokuwa rahisi, kila mtu anaonekana akiweza kufanya vizuri.
Ni pale mambo yanapokuwa magumu ndiyo tofauti za watu zinapoonekana. Kwani wengi sana wanakuwa hawawezi kuhimili ugumu, hivyo huacha na kwenda kutafuta mengine rahisi.
Wanaofanikiwa kwenye eneo lolote lile ni wale ambao wakikutana na ugumu wanaendelea nao bila kuacha.
Kwani wanajua ugumu una kazi ya kuwaondoa wale ambao hawajajitoa hasa.
Wanajua upande wa pili wa ugumu ni mafanikio makubwa. Hilo linawafanya wakazane kuuvuka huo ugumu na kupata matokeo makubwa.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ufanyaji wa maamuzi.
Kufanya maamuzi rahisi ni rahisi na kila mtu anapenda kufanya maamuzi hayo rahisi.
Ni maamuzi magumu ndiyo huwa magumu sana kufanya.
Na wale wanaoweza kufanya maamuzi magumu, ndiyo wanaopata mafanikio makubwa.
Kufanya maamuzi magumu ndiyo kunawatofautisha viongozi na wafuasi.
Wafuasi wanaweza kufanya maamuzi rahisi bila ya shida yoyote.
Ni maamuzi magumu ndiyo yanawafanya wawaangalie viongozi, ambao wanayafanya vizuri na wao kufuata.
Uwezo wa kufanya maamuzi magumu na yakaenda vizuri ndiyo unawatofautisha viongozi na wafuasi.
Ndiyo pia unaopelekea malipo yatofautiane kati ya viongozi wa juu na watu wa chini.
Watu wa chini wanaweza kuwa wanafanya kazi ngumu kuliko watu wa juu, lakini bado hao wa juu wakawa ndiyo wanaolipwa zaidi.
Sababu ni watu wa juu wanafanya maamuzi magumu na muhimu ambayo wa chini hawawezi kuyafanya.
Uzuri ni kufanya maamuzi magumu ni ujuzi ambao kila mtu anaweza kujijengea.
Japo unajengwa kwa kufanya makosa, lakini kwa kuboresha na kufuatilia kwa karibu mtu unazidi kuwa vizuri kwenye kufanya maamuzi.
Anza kuyaendea maamuzi magumu kila unapokutana nayo. Usiogope wala kukimbia unapokabiliana na maamuzi magumu, badala yake yakabili kwa usahihi ili uwe imara na kuweza kufanya maamuzi hayo kwa usahihi.
Kadiri unavyofanya maamuzi magumu mara kwa mara, ndivyo unavyozidi kuwa bora kwenye kuyafanya maamuzi hayo.
Kamwe usiyakimbie maamuzi magumu kwa sababu ya uguku wake, bali yakabili na uyafanye ili uweze kufanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe