Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kuwa muuzaji bora kunaanza na kuwa mtu bora. Na kuwa mtu bora ni matokeo ya kujiendeleza binafsi. Huzaliwi ukiwa mtu bora, bali unajijenga kuwa mtu bora, kupitia kufanyia kazi eneo la maendeleo binafsi.

Ili uweze kupata matokeo ambayo hujawahi kupata, lazima uwe mtu ambaye hujawahi kuwa na ufanye mambo ambayo hujawahi kufanya. Kuwa mtu wa tofauti na kufanya mambo ya tofauti ni kitu ambacho kinakuja na hatari ya kushindwa.

Pale kunapokuwa na hatari ya kushindwa, hofu huwa inajengeka na mtu kutokuwa tayari kufanya. Hiyo ndiyo imekuwa sababu ya watu kubaki kwenye mazoea yao na kushindwa kupiga hatua kubwa.

Hofu huwa ni kitu ambacho hakipo, ni kitu cha mtu kujitengenezea yeye mwenyewe. Kwa mfano mtu anaposhindwa kufanya kwa sababu ya kuhofia kushindwa, bado anakuwa hajashindwa. Na hata kama atafanya na akashindwa, matokeo huwa siyo mabaya kama anavyokuwa anadhania.

Ili kupata matokeo ya tofauti kwenye kila eneo la maisha yetu, tunapaswa kuvuka hofu ya kushindwa inayotuzuia kuchukua hatua za tofauti. Na hapo ndipo ujasiri unapokuwa unahitajika sana kama sifa muhimu ya maendeleo binafsi na mafanikio kwa ujumla.

Ili uweze kuwa mtu bora, lazima kwanza uwe jasiri. Kwa bahati nzuri sana, ujasiri ni kitu ambacho mtu unaweza kujijengea wewe mwenyewe. Siyo kitu ambacho mtu unazaliwa nacho au kama hukuzaliwa nacho basi huwezi kukipata.

HATUA ZA KUJIJENGEA UJASIRI.

Kujenga ujasiri ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukifanya. Hilo linawezekana kwa kufuata hatua hizi;

Hatua ya kwanza ni mtu kujitambua mwenyewe, kwa kujua uimara na madhaifu yako. Ukishajua maeneo ambayo una uimara, unafanya mambo yaliyo zaidi kwenye maeneo hayo. Na kwa maeneo ambayo una udhaifu unatafuta wengine wanaoweza kuyafanyia kazi vizuri. Kwa njia hii unapata matokeo mazuri na kuepuka kujikwamisha wewe mwenyewe kwa madhaifu unayokuwa nayo.

Hatua ya pili ni kufanya mambo ambayo unahofia kuyafanya. Huwa wanasema dawa ya hofu ni kufanya mambo unayohofia kufanya. Ni kupitia kufanya yale unayohofia ndiyo hofu inakosa nguvu ya kukuzuia. kama ambavyo tumeona, hofu ni kitu ambacho hakipo, ni hadithi ya kutungwa ambayo inakutisha. Kama hutachukua hatua, hadithi hiyo inazidi kupata nguvu na kukutisha. Lakini unapochukua hatua, matokeo huwa ni tofauti na hofu unayokuwa nayo. Unaweza usishindwe kama ulivyotegemea, lakini hata ukishindwa, mambo huwa hayawi mabaya kama ulivyodhania. Kufanya yale unayohofia kufanya ndiyo hatua muhimu sana ya kujijengea ujasiri na kuishinda hofu.

Hatua ya tatu ni kutumia historia yako mwenyewe kujipa moyo wa kuendelea kufanya makubwa na ya tofauti uliyopanga. Kila mmoja wetu kuna hatua amewahi kuchukua huko nyuma na zikampa matokeo ya tofauti. Tunapaswa kutumia hiyo historia kupata msukumo wa kuendelea kufanya. Tumia kila ushindi ambao umeshaupata huko nyuma, hata kama ni mdogo kiasi gani, kupata msukumo wa kufanya makubwa zaidi. Jipe moyo kwamba kama umeweza kufanya hayo uliyofanya mpaka sasa, unaweza kufanya mengine makubwa zaidi.

Kwa kujitambua wewe mwenyewe na kuwa mtu wa kufanya, huku ukitumia matokeo yako ya nyuma, utaweza kuwa jasiri na kufanya makubwa. Tufuate hatua hizo tatu za kujijengea ujasiri ili tuwe watu bora na kufanya mauzo makubwa.

SOMA; Unahitaji Huu Ujasiri Ili Uweze Kukamilisha Mauzo Makubwa Zaidi.

JINSI UJASIRI UNAVYOKUWEZESHA KUUZA ZAIDI.

Hatua muhimu sana inayohitajika ili mtu uweze kufanya mauzo makubwa ni kuwakabili watu. Unahitajika kuwakabili watu ambao huwajui na hawakujui, hivyo nafasi ya kukataliwa huwa ni kubwa. Lakini pia unahitajika kuwakabili watu wakubali kukupa fedha zao, ambazo wamezipata kwa taabu.

Kuwafikia watu wapya na kuwataka watu wakupe fedha ni hatua ambazo zina hatari kubwa ya kukataliwa. Hayo ndiyo maeneo makubwa mawili yenye hofu kwenye mauzo na yanayowakwamisha wauzaji wengi kufanya mauzo makubwa.

Hofu ya kukataliwa huwa ni kubwa kwenye kuwakabili watu ambao hatuwajui na kwenye kuwatenganisha watu na fedha zao, yaani kuwataka walipie kile tunachowauzia. Ndiyo maana wauzaji wengi hupenda kufuatilia wale wateja ambao tayari wanawajibu vizuri na wapo tayari kulipia wenyewe bila ya kusubiri kuambiwa walipiwe.

Huwezi kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa kwa kufuatilia wateja wale tu ambao tayari wanakukubali, huwa ni wachache sana. Na kusubiri watu wawe tayari kukulipa wao wenyewe kunakuzuia kufanya mauzo makubwa, kwa sababu watu huwa wanachelewa sana kufanya maamuzi kwenye kutumia fedha zao.

Ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa ni lazima uwe na ujasiri wa kuwakabili watu wa aina zote. Uweze kuvuka hofu ya kukataliwa na watu ambao huwajui na hawakujui, kwa kuwa tayari kuwafikia na kuwaeleza kile unachouza. Utaishinda hofu hiyo kwa kuwafikia watu wengi zaidi, ukijua hata wakikataa, hawajakukataa wewe kama mtu, bali wamekataa kile unachowaambia. Unajua kwa kuongea na wengi zaidi, kuna ambao watakataa, lakini pia kuna ambao watakubali, wewe unachoangalia ni wale wanaokubali.

Kuwatenganisha watu na fedha zao kwa kuwataka walipie kile unachouza ni hatua ya mwisho na muhimu kwenye kukamilisha mauzo. Hatua hiyo ina hatari ya mtu kukataa hivyo mtu kuwa na hofu kwenye kufanya hivyo. Kwa kuwa jasiri na kufanya, inakuweka kwenye nafasi ya kuuza zaidi. Pale unapofika hatua ya kukamilisha mauzo na kuwaambia wateja walipie ili kupata kile unachowashawishi, unaongeza nafasi ya kukamilisha mauzo zaidi kuliko kuwaacha wateja waamue wenyewe kama watalipia au la. Kwa kumwambia kila mteja alipie ili kupata unachouza, kuna ambao wataonekana hawapo tayari, lakini pia kuna wengi watakubali na kulipia. Mara nyingi sana wateja huwa wanawategemea wauzaji wawaelekeze nini cha kufanya. Kuwa na ujasiri wa kuwaambia wateja walipie kunakuweka kwenye nafasi ya kuuza zaidi.

Muuzaji bora kuwahi kutokea, ujasiri siyo kutokuwa na hofu kabisa, bali ni kufanya licha ya kuwa na hofu. Ujasiri ni kuchagua kuchukua hatua kwenye yale unayohofia kufanya, ukijua upande wa pili wa hofu ni matokeo makubwa na mazuri. Kwa kujitambua wewe mwenyewe kwenye uimara na madhaifu yako na kutumia historia yako mwenyewe kwa matokeo ambayo umeshayapata mpaka sasa, unapata msukumo wa kuchukua hatua licha ya hofu unazokuwa nazo. Ukishaweza kuchukua hatua kwenye jambo lolote lile, hofu zote ulizokuwa nazo juu ya jambo hilo zinapotea kabisa. Fanya yale unayohofia kufanya, utaishinda hofu na kuwa jasiri zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.