Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Hongereni wote kwa kuendelea kukaa kwenye mchakato wetu wa programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo, kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Kwenye uwekezaji kuna aina na njia mbalimbali ambazo mtu unaweza kutumia. Kila njia inaweza kukufikisha kwenye lengo la UTAJIRI na UHURU WA KIFEDHA, japo namna ya kufanya hivyo inatofautiana.

Uwekezaji upo wa mali, kama ardhi, majengo, bidhaa, sarafu, madini na vitu vingine vya thamani. Uwekezaji huu unakuwa ni wa vitu vinavyoonekana na kushikika.

Pia uwekezaji upo wa masoko ya mitaji, ambapo huwezi kuuona kwa macho wala kuushika uwekezaji wako. Huu unahusisha hisa, vipande, hatifungani na akaunti maalumu za akiba.

Kila mtu kwenye maisha yake anaweza kuwa na mipango yake ya uwekezaji kwa kuzingatia aina na kiasi. Inapokuja kwenye mahitaji ya maisha na malengo, watu tunatofautiana.

Lakini kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU, tunataka kitu ambacho kinaweza kutuleta wote pamoja. Tunapokuwa na kitu cha pamoja, inakuwa rahisi kuambatana na kusukumana kwa kila mmoja kupata matokeo mazuri.

Katika aina nyingi za uwekezaji ambazo zipo, kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja ya uwekezaji, mfuko mkuu ukiwa wa UMOJA unaosimamiwa na UTT AMIS.

Lengo letu kwa pamoja ni kuwekeza kiasi kidogo kidogo kila wiki kwa angalau miaka 10 bila kuacha wala kutoa uwekezaji huo. Unaweza kwenda zaidi ya hapo, lakini siyo pungufu. Kila wiki lazima uwekeze angalau elfu 7, ikiwa ni elfu moja uliyotenga kila siku.

Hii ni changamoto ambayo tumejipa ili kujenga tabia ya uwekezaji kuwa sehemu ya maisha yetu. Lakini pia kupitia tabia tunayokuwa tumejenga, tunakuza uwekezaji wetu na kuweza kufikia UTAJIRI NA UHURU WA KIFEDHA.

Kuwa kwenye NGUVU YA BUKU haikuzuii kuwekeza maeneo mengine, ila hakikisha uwekezaji mwingine wowote unaoufanya, haukwamishi mpango wako wa uwekezaji kwenye NGUVU YA BUKU.

Mpango wako wa uwekezaji kwenye NGUVU YA BUKU ndiyo kipaumbele namba moja kwa kila aliye ndani ya programu hii. Mipango mingine inaendelea baada ya kutekeleza huu mkuu.

SOMA; Uwekezaji Kwenye Mifuko Ya Pamoja Ya UTT AMIS.

Tumechagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kwa sababu ni rahisi kwa kila mtu kuwekeza na haihitaji mlolongo wowote wa ziada. Huhitaji hata kufuatilia soko linaendaje. Wewe ni kuwekeza kisha kuendelea na shughuli zako. Mifuko ina wasimamizi ambao wanafanya mengine yote kwa ajili yako.

Na tumechagua mfuko wa UMOJA wa UTT AMIS kwa sababu ndiyo mfuko mkongwe na ambao kwa karibu miaka 20 umekuwa unafanya vizuri. Hilo linaonyesha kwamba ni mfuko mzuri na ambao una fursa ya kuendelea vizuri zaidi.

Kwenye FAMILIA YA KISIMA CHA MAARIFA, tunashirikishana maarifa mengi na ya uwekezaji wa aina mbalimbali. Hilo halikulazimu wewe ufanye kila uwekezaji unaoshirikishwa. Kama tayari unawekeza kwenye mfuko wa pamoja na una mpango wa kuwekeza kwa msimamo bila kuacha au kutoa kwa muda mrefu, tayari upo pazuri.

Huhitaji kuhangaika na mengine kama bado hujaweza kufanya uwekezaji mzuri kupitia mifuko ya pamoja. Weka fokasi yako ya uwekezaji kwenye mfuko wa pamoja uliochagua kwanza mpaka uwe na kiasi kizuri cha uwekezaji ndiyo uanze kutawanya kwenye aina nyingine za uwekezaji.

MABORESHO KWENYE PROGRAMU YA NGUVU YA BUKU.

Katika kuhakikisha programu inaendelea kuwa bora na kuwasaidia watu wote wenye nia ya kujenga utajiri bila ya kumtenga yeyote, tunakwenda kuwa na maboresho madogo. Maboresho hayo ni kama ifuatavyo;

1. Utaratibu wa kutuma salio kila siku ya Ijumaa tunauondoa, badala yake salio litakuwa linatumwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi. Salio litaombwa kwa njia ya email kutoka UTT na kisha kutumwa kwenye namba ya wasimamizi wa programu. Salio halitawekwa tena kwenye kundi wazi. Tukumbuke lengo la kutuma salio ni kuwajibika ili usitoe uwekezaji wako kwa sababu zozote zile.

2. Masomo ya wiki itakuwa mara moja badala ya mara mbili kama sasa, somo litakuwa siku ya Ijumaa na kila mshiriki atapaswa kusoma na kushiriki mjadala wa somo.

3. Kupata nafasi kwenye programu ya UHURU WA KIFEDHA, ambapo unasimamiwa kwa karibu zaidi kwenye uwekezaji, itategemea ufanisi wako kwenye programu ya NGUVU YA BUKU. Ni kama umeweza kutekeleza vizuri utaratibu wa NGUVU YA BUKU ndiyo unaweza kupata nafasi kwenye UHURU WA KIFEDHA.

Taratibu nyingine za programu zitaendelea kama zilivyo, uwekezaji wa lazima kufanya na kutuma ushahidi ni siku ya Jumatatu, kiasi kisichopungua elfu 7. Unaweza kwenda zaidi ya hapo kadiri uwezavyo. Pia unaweza kuwekeza kila siku au mara kwa mara kadiri ya mpango wako na kutuma kwenye kundi kama sehemu ya kupata uwajibikaji.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Orodhesha aina zote za uwekezaji unazojua na zinazoweza kufanyika Tanzania.
2. Kwa nini kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja?

3. Kwa nini kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua mfuko wa UMOJA wa UTT kuwa ndiyo uwekezaji kipaumbele kwetu?

4. Tofauti na uwekezaji unaofanya kwenye NGUVU YA BUKU, je kuna uwekezaji mwingine unaofanya? Kama ndiyo eleza ni uwekezaji wa aina gani na unaufanya kwa mpango gani.

5. Kama bado hujaanza uwekezaji nje ya NGUVU YA BUKU, ni uwekezaji upi mwingine ambao unapanga kufanya? Umepanga kuanza wakati gani au ukishafika ngazi gani?

6. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.