3475; Ugumu siyo ugumu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu aliye makini na mafanikio anajua kabisa kwamba kazi inahitajika ili kujenga mafanikio.
Mafanikio ni zao la kazi kubwa ambayo mtu anakuwa ameiweka kwenye kitu anachofanya.

Kazi ambayo mtu anapaswa kufanya ili aweze kufanikiwa ni kazi ngumu.
Hiyo ni aina ya kazi ambayo wengi wanakwepa kufanya na hivyo ushindani kutokuwa mkubwa sana.

Hiyo ina maana kwamba kama utaweza kufanya kazi ngumu, kitu ambacho wengi wanakikwepa, safari yako ya mafanikio itakuwa rahisi zaidi.

Kinachofanya kazi iwe ngumu kufanya siyo ugumu wake, bali wingi wa siku ambazo unapaswa kuifanya kwa msimamo bila kuacha.

Kila mtu anaweza kufanya kazi ngumu, mara chache. Ni kufanya kwa mwendelezo ndipo wengi wanaposhindwa.
Na hapo ndipo mafanikio makubwa yalipojificha.

Kusema hapana kwa vitu ambavyo unaweza na unapenda kufanya, lakini havina mchango kwenye mafanikio yako ni kitu kingine kigumu kwenye safari ya mafanikio.
Hili huwa linazidi kuwa gumu kadiri mtu anavyopiga hatua na kuweza kumudu kufanya chochote anachotaka.

Mtu anapokuwa anaanzia chini kabisa kuna vitu vingi anavyokuwa anapenda kufanya ila hawezi kumudu kufanya.
Hivyo mtu hasumbuki navyo sana.
Tatizo linaanza pale mtu anapopiga hatua na kuweza kumudu kufanya mengi anayopenda kufanya.
Hapo ndipo ugumu mwingine unapoanzia, kuweza kusema HAPANA kwenye mambo unayopenda ila hayana mchango kwenye mafanikio unayoyataka.

Tunaposema mafanikio yanahitaji kazi ngumu, hatumaanishi tu ule ugumu wa kazi yenyewe, bali kuifanya kwa msimamo bila kuacha na kusema Hapana kwenye mengine yote ambayo hayachangii kwenye mafanikio.

Kila mtu anaweza kufanya mambo makubwa sana mara moja moja. Ndiyo maana unapokutana na hatari yoyote, huwa unakuwa tayari kuchukua hatua za haraka kujinusuru.
Lakini ukiambiwa urudie hatua hizo hizo kukiwa hakuna hatari, unashindwa.
Sasa mafanikio ni kuweza kurudia hatua ngumu kwa msimamo bila kuacha.

Tuangalie mfano ili tuelewane vizuri.
Ukiwa unapita zako njiani na ghafla mbwa wakali wakaanza kukufukuza, utajikuta ukiweza kupanda ukuta mkubwa ili tu kujinusuru.
Lakini ukiambiwa upande ukuta huo huo bila ya kuwepo kwa hatari, unashindwa kabisa.
Sasa mafanikio ni kuweza kupanda ukuta huo kila siku bila kuacha. Ukiweza hilo, mafanikio uneyaweza.

Weka kazi ngumu kwa msimamo bila kuacha na sema hapana kwa yote yasiyo mchango kwenye mafanikio makubwa na mafanikio kwako linakuwa swala la muda tu.
Kufanikiwa inakuwa uhakika kwako kama ukiyaweza hayo mawili kwa muda mrefu.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe