Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Kwenye mafanikio, huwa hakuna jeshi la mtu mmoja kama baadhi ya watu wanavyopenda kujinadi. Huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote lile kwa juhudi zako binafsi pekee. Ndiyo unahitaji kuweka juhudi kubwa sana ili kufanikiwa, lakini pia mchango wa watu wengine unahitajika ili uweze kupata kile unachotaka.
Ukubwa wa mafanikio yako kwenye maisha unategemea ukubwa wa mtandao ulionao. Na mtandao wako ni watu unaowajua na wanaokujua wewe. Kwa umuhimu wa watu kwenye maisha na mafanikio, tunawajibika kujenga, kukuza na kutunza mtandao wetu ili kupata mafanikio makubwa.

NGUVU YA MTANDAO WAKO KWENYE KUWA MUUZAJI BORA NA KUKUZA MAUZO.
Mtandao wako binafsi una nguvu kubwa ya kukufanya wewe kuwa muuzaji bora na kukuza mauzo yako.
1. Mtandao wako unakusaidia kuwafikia watu wengi na kujua kuhusu uwepo wako na kile unachouza. Kadiri watu wengi wanavyokujua, ndivyo wengi zaidi nao wanakujua. Hiyo ni kwa sababu wale wanaokujua watakuwa wanakuongelea mara kwa mara, kitu kinachowafanya wengine nao wakujue.
2. Mtandao wako unarahisisha wewe kukamilisha mauzo kwa wateja, hasa wale ambao bado hawakuamini. Kama kuna mtu anayekujua na kukuamini, ambaye pia mtu unayemshawishi anunue anamjua, unaweza kumtumia huyo anayemjua kama ushuhuda wako. Watu wakishuhudiwa na wale wanaowajua wanaamini kuliko ukiwashuhudia wewe.
3. Mtandao wako unakuwezesha kupata wateja wapya ambao hawahitaji nguvu kubwa kwenye kuwashawishi. Hiyo ni kupitia kuomba rufaa kwenye mtandao wako, kwa kuwa watu wanakuamini, wanakuunganisha na watu wengine sahihi kwako.
4. Mtandao wako una nguvu ya kukutambulisha kwa watu wakubwa na muhimu ambao kwa nafasi zao usingeweza kuwafikia moja kwa moja. Lakini kwa kuwa na mtandao mkubwa ni rahisi kupata watu watakaokutambulisha kwa watu hao muhimu na nafasi ya kuwafikia ikawa rahisi kwako.
5. Kupitia mtandao wako unaweza kujifunza vitu vingi ambavyo peke yako usingeweza kuvijua. Ni kupitia wengine ndiyo unajifunza mambo mengi ambayo hukuwa unayajua.
SOMA; Njia 10 Za Kujenga Mtandao Wako Bila Kwenda Baa.
JINSI YA KUJENGA, KUKUZA NA KUTUNZA MTANDAO WAKO.
Ili kujenga, kukuza na kutunza mtandao wako, unapaswa kuchukua hatua zifuatazo;
1. Kuwa bora sana kwenye kile unachofanya. Ni kupitia wewe kuwa bora ndiyo utaweza kutoa thamani kubwa kwa wengine na sifa zako kusambaa kwa wengine wengi zaidi. Kabla ya kuhangaika na vitu vingine vya kukuza mtandao wako, hakikisha kwanza uko bora kwenye kile unachofanya.
2. Shiriki matukio mbalimbali yanayowaleta pamoja watu ambao unataka kuwa nao kwenye mtandao wako, yaani wakujue na wewe uwajue. Ni rahisi kujuana na watu kama unashiriki nao kwenye matukio yanayowaleta pamoja.
3. Kila anayekujua na unayekutana naye hakikisha anakujua wewe ni nani na unafanya nini. Anza kwa kuwakumbusha watu wako wa karibu ni nini unafanya na kinawasaidia watu wa aina gani. Kila unapokutana na watu wapya, jitambulishe jina lako na nini unafanya, kisha waulize na wao pia. Na kila unapojitambulisha mahali popote, eleza kile unachofanya. Rudia rudia kujitambulisha ili watu wakuelewe kwa kina.
4. Tumia fursa za kuongea, kufundisha au kushauri wengine kwa njia za kukutana, mawasiliano au vyombo vya habari ili kujulikana zaidi. Pale unapoongea kwenye matukio mbalimbali, kufundisha au kushauri, unaaminika zaidi na kujulikana na wengi zaidi.
5. Tumia fursa za mitandao ya kijamii na njia nyingine za kidijitali kujenga wafuasi na kuwafikia wengi zaidi, kitu kinachokuza mtandao wako zaidi.
Kujenga mtandao wako ni kitu kinachokutaka uweke juhudi na muda kufanikisha. Chukua hatua ulizojifunza hapa na nyingine kuhakikisha unajenga mtandao wenye manufaa kwako na kwa wengine.
MAMBO YA KUEPUKA KWENYE KUJENGA MTANDAO.
Kuna makosa ambayo watu wamekuwa wanayafanya kwenye kujenga mtandao na kuishia kuwagharimu. Hayo ni mambo ya kujua ili kuyaepuka.
1. Epuka ‘uchawa’. Kumekuwa na dhana ya uchawa ambapo mtu anasifia wengine hata kwa mambo ya uongo ili tu kukubalika. Njia hii huwa inaonekana kuwa na matokeo ya haraka, lakini mwisho wake huwa siyo mzuri. Epuka sana uchawa, kwa kuhakikisha kuna thamani kubwa unayotoa kwa wengine.
2. Epuka ‘kiki’. Kwenye zama hizi za mitandao na mambo kusambaa kwa kasi, mambo mabaya huwa yanasambaa kwa kasi zaidi. Hilo limewafanya wengi kuwa tayari kufanya mambo yasiyo sahihi ili tu taarifa zao zisambae. Hiyo ndiyo inaitwa ‘kiki’. Kiki pia huwa zinafanya mtu kufahamika haraka, lakini huwa na madhara kwa muda mrefu.
3. Epuka kupokea zaidi ya unavyotoa. Huwa kuna mlinganyo usio wa wazi kwenye kutoa na kupokea. Ili mahusiano yadumu, kutoa kunapaswa kuwa kukubwa kuliko kupokea. Unapojenga mtandao kwa kuangalia wewe unapata nini pekee, hautakuwa mtandao imara. Mtandao imara ni ule unaojengwa kwenye kutoa thamani kubwa zaidi kwa wengine.
4. Usitake umaarufu kwa ajili ya umaarufu. Watu wamekuwa wanakazana kujenga umaarufu kwa ajili tu ya kuwa maarufu. Kwa njia hiyo hujikuta wanafanya mambo ambayo baadaye yanakuwa kikwazo kwao. Wewe kazana kuwa maarufu kupitia vitu bora unavyofanya.
5. Epuka kujihusisha na kila kitu. Watu huwa ni rahisi sana kujisahau pale wanapopata mafanikio fulani kwa eneo fulani na kudhani wanaweza kushauri kwenye maeneo yote. Chagua eneo lako la ubobezi na lisemee hilo kwa uhakika ili usichanganye mambo na kuonekana unakosa umakini.
Ukubwa wa mafanikio yako unategemea sana ukubwa wa mtandao wako, kazana kujenga, kukuza na kutunza mtandao wako kwenye mauzo ili uwe muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Kazana kuwa bora sana kwenye kile unachofanya, toa thamani kubwa na wafikie watu wengi zaidi. Hayo yatakuwezesha kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa kupitia mtandao uliojenga, kukuza na kutunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.