Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Mahali popote penye watu wengi, pana fursa ya biashara kuweza kuwafikia kwa urahisi wakaijua na kuweza kuwashawishi kununua.
Moja ya njia za kuwafikia wateja ambazo kila biashara na kila muuzaji anaweza kutumia ni matukio maalumu.
Matukio maalumu ni ambayo yanawaleta watu pamoja kwa sababu fulani. Kwa kuwa watu hao tayari wapo mahali pamoja, kuwafikia inakuwa rahisi.
Kutumia matukio maalumu kuwafikia wateja wengi ni moja ya njia za kuwasaka na kuwafuatilia wateja zenye nguvu ya kuwafikia wengi kwa urahisi na kuwa na ushawishi mkubwa kwao.

AINA ZA MATUKIO MAALUMU YANAYOFAA KUWAFIKIA WATEJA WENGI.
Kuna matukio mengi ambayo yanawaleta watu pamoja, lakini ya msingi kabisa ambayo yanaweza kutumiwa kwa manufaa makubwa ni haya yafuatayo.
1. Makongamano.
Hii ni mikutano mikubwa inayowakutanisha watu wengi kwenye eneo moja na wakati mmoja. Ni fursa nzuri ya biashara kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja na ana kwa ana.
2. Matukio ya kujenga mtandao.
Haya ni matukio yanayoandaliwa kwa ajili ya kujenga mtandao baina ya washiriki. Lengo ni washiriki kujuana na kuona njia wanazoweza kushirikiana. Muuzaji anaweza kutumia matukio haya kupata watu wanaoweza kuhitaji kile anachouza.
3. Matukio yanayofanyika kwa njia ya mtandao wa intaneti.
Mtandao wa intaneti umekuwa unatoa nafasi ya watu wengi kuweza kukusanyika na kushiriki kwenye tukio fulani kwa wakati mmoja. Yanaweza kuwa mafunzo au mkutano unaowaleta watu pamoja. Kwa uwepo wa watu hao pamoja kupitia mtandao, ni fursa ya kuwafikia.
4. Matukio ya uzinduzi wa kitu kipya.
Uzinduzi wa kitu kipya, iwe ni biashara yenyewe, bidhaa au huduma, na hata mpango fulani ni njia ya kuwaleta watu pamoja na kuwafanya waijue biashara na kushawishika kununua.
5. Maonyesho ya biashara.
Maonyesho ya biashara ni matukio yanayoandaliwa na kuzileta biashara pamoja. Watu wengi hutembelea maonyesho hayo kujua biashara zilizopo na hata kununua moja kwa moja. Kwa biashara kushiriki maonyesho ya biashara inapata fursa ya kuwafikia wateja wengi kwa wao wateja kutembelea banda la biashara.
Kuna matukio mengi ambayo biashara inaweza kuyatumia kufikia wateja, popote penye watu ni fursa inayoweza kutumiwa vizuri.
SOMA; Tumia Sikukuu Na Siku Maalumu Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
KWA NINI MATUKIO MAALUMU YANA NGUVU KWENYE KUWAFIKIA WENGI.
Matukio maalumu huwa yana nguvu kwenye kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kununua kwa sababu zifuatazo;
1. Uwepo wa watu pamoja.
Kitendo cha watu kuwa pamoja kwenye tukio, iwe ni ana kwa ana au mtandaoni kinakuwa na nguvu kwa sababu wote wanafanya kitu kwa wakati mmoja. Tofauti na unapomfikia kila mtu kwa wakati wake, anaweza asichukue hatua mara moja.
2. Kukutana na watu ana kwa ana.
Matukio yanayowaleta watu pamoja yanakuwa na nguvu kwa sababu ya kuweza kukutana na watu ana kwa ana na hivyo kujenga ushawishi mkubwa zaidi. Hata matukio yanayofanyika kwa njia ya mtandao wa intaneti, kuna hali ya kama ni ana kwa ana kwa sababu ya kuzungumza pamoja na hata kuonana kwa njia ya video. Hilo linakuwa na ushawishi zaidi.
3. Kutoa maelekezo ya moja kwa moja.
Kwenye matukio yanayowaleta watu pamoja, maelekezo ya hatua za kuchukua yanaweza kutolewa pamoja kwa watu wote na wao kuweza kuchukua hatua. Hiyo inarahisisha zoezi zima la kutoa maelekezo kwa watu tofauti na kutoa kwa njia nyingine. Mtu anaweza kuuliza pale ambapo hajaelewa na kufafanuliwa zaidi.
4. Kuwaelimisha wale wanaofikiwa.
Faida kubwa ya kutumia matukio ni kuweza kuwaelimisha wale wanaokuwepo kwenye matukio hayo. Kwa kupata elimu sahihi na wakaelewa, wanaweza kushawishika zaidi kuliko wangekutana tu na tangazo la kitu.
5. Urahisi wa ufuatiliaji.
Watu ambao wameijua biashara au muuzaji kwenye tukio ni rahisi kufuatiliwa kwa sababu taarifa zao nyingi zinakuwa zinajulikana. Kwenye matukio kunakuwa na njia za kukusanya taarifa nyingi za washindani ambazo zinaweza kuwatumika wakati wa kuwafuatilia na kurahisisha zoezi hilo la ufuatiliaji.
Kwa nguvu hii ya matukio ya pamoja kwenye kuwafikia wengi, ni njia inayopaswa kutumiwa na kila biashara pamoja na kila muuzaji.
MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA MATUKIO MAALUMU KUWAFIKIA WATEJA.
Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia kwenye kutumia matukio maalumu kuwafikia wateja ili kupokelewa vizuri, kukumbukwa na kuwa na ushawishi.
1. Kuwa na maandalizi mazuri kabla ya tukio husika ili kulitumia vizuri.
2. Fanya lengo lako kuu la kuweka au kushiriki tukio ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa. Hilo linapokuwa lengo unaweza kutumia fursa mbalimbali kulikamilisha.
3. Kama tukio unaandaa mwenyewe, wafikie wale wenye sifa ya kuwa wateja wa biashara yako. Na kama tukio unashiriki ambalo wanaoandaa ni wengine, chagua tukio ambalo linawafikia wale wenye sifa ya kuwa wateja wako.
4. Weka mkakati wa jinsi ya kuwafikia watu waliopo kwenye tukio na kukusanya taarifa zao ili kuweza kuwafuatilia baada ya tukio.
5. Watu wote wanaoshiriki matukio ya kuwafikia wateja wanapaswa kuwa na mafunzo sahihi ya kuchangamana na watu vizuri na kukamilisha lengo la ushiriki wa tukio husika.
6. Jiandae kutoa mafunzo yenye thamani kubwa kwenye matukio ambayo biashara inaandaa au kushiriki ili watu watoke na kitu watakachokumbuka kwa muda mrefu.
7. Taarifa za wateja zinazokusanywa wakati wa tukio zigawanywe kwa aina ya wateja na sifa zinazowafanya wawe sahihi. Pia uharaka wa kutaka kile kinachouzwa unapaswa kupimwa na kuzingatiwa.
8. Jiandae kuuza moja kwa moja wakati wa tukio ili wateja wanaposhawishika na kuchukua hatua waweze kuhudumiwa vizuri.
9. Weka mpango wa kuwafuatilia wateja baada ya tukio na kuhakikisha unatekelezwa. Kila mteja aliyepatikana kwa tukio anapaswa kufuatiliwa ndani ya masaa 24, kisha kuendelea kufuatiliwa kwa karibu mpaka kununua na kuendelea kuwa sehemu ya biashara.
10. Weka vigezo vya kupima mafanikio kwa kuandaa au kushiriki tukio, kwa kulinganisha gharama zilizotumika na wateja waliopatikana pamoja na mauzo yanayofanyika kwa wateja hao waliofanyika. Muhimu ni kuhakikisha wateja wanaofikiwa kwenye tukio wanafanya manunuzi, hata kama ni baada ya tukio.
Mkakati wa kuwafuatilia wateja baada ya kushiriki tukio unapaswa kuhusisha njia mbalimbali za mawasiliano kama kupiga simu, kutuma jumbe za simu kwa njia ya kawaida au kwa wengi (BULK SMS). Pia njia za mtandao kama mitandao ya kijamii na barua pepe ni njia nyingine za kuwafikia wateja baada ya kushiriki tukio.
Matukio yana nguvu kubwa ya kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja na yana ushawishi mkubwa kwao kwa sababu ya kukutana pamoja na elimu inayotolewa. Biashara na wauzaji wanaoandaa au kushiriki kwenye matukio wanapaswa kujiandaa vyema ili kutumia fursa hiyo kuwafikia wengi na kwa ushawishi, kupitia kutoa elimu sahihi ya kile wanachouza. Kuwafuatilia wateja baada ya tukio ndiyo hatua yenye nguvu zaidi, kwa sababu wengi hawatanunua wakati wa tukio, ila wanapofuatiliwa kwa karibu inakuwa rahisi kwao kununua.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.