3479; Makosa Mawili Kwenye Safari Ya Mafanikio.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaoyataka mafanikio ni wengi.
Lakini wanaoyapata hasa huwa ni wachache sana.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo na kila tasnia.

Kuna mengi ambayo yamekuwa yanawazuia watu wasifanikiwe.
Lakini makosa makubwa ambayo yamekuwa kikwazo cha mafanikio kwa walio wengi ni mawili.

Kosa la kwanza ni kutokuanza kabisa kufanya kile kinachopaswa kufanywa ili mafanikio yapatikane.
Mafanikio huwa hayatokei tu kwa sababu mtu unataka kufanikiwa.
Bali mafanikio huwa yanatengenezwa kupitia hatua ambazo mtu anachukua.

Watu wengi, pamoja na kusema wanataka kufanikiwa, bado wamekuwa hawafanyi yale wanayopaswa kufanya ili kufanikiwa.
Wanachosema na wanachofanya vinakuwa tofauti kabisa.

Dawa ya kosa hili la kwanza ni mtu kufanya. Chochote unachotaka, anza kwa kuchukua hatua za uhakika ili kuweza kukipata.
Usijidanganye kwamba mambo yatatokea tu yenyewe.
Badala yake fanya kuyatengeneza yale unayotaka yatokee.

Kosa la pili ni kuishia njiani.
Hapa unakuwa umevuka kosa la kwanza kwa kuanza kufanya.
Lakini huendi na ufanyaji huo mpaka kupata mafanikio makubwa unayokuwa unayataka.
Unaanza kufanya, lakini unaishia njiani.

Sehemu ambayo wengi wamekuwa wanaishia ni pale wanapoanza kukutana na magumu na changamoto.
Watu huwa wanapenda vitu viwe rahisi, wakikutana tu na ugumu au changamoto wanaona ndiyo mwisho wa kufanya.
Wanakata tamaa na kuacha kabisa kufanya.

Lakini pia kuna ambao wanaacha kuweka juhudi kubwa pale wanapopata mafanikio madogo.
Wanaridhika haraka na mafanikio madogo wanayokuwa wamepata na kudhani wameshamaliza kila kitu.

Hivyo ndivyo mafanikio madogo yamekuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa.
Watu wanaacha kufanya yale wanayopaswa kufanya pale wanapopata matokeo mazuri.
Hilo linazuia mtu kupata mafanikio makubwa zaidi.

Dawa ya kosa hili la pili ni kuendelea kufanya hata kama umeshafika juu kiasi gani.
Jua kwenye kila hatua ambayo mtu unakuwa umefikia, kuna hatua nyingine kubwa zaidi unazoweza kupiga.
Hivyo unapaswa kujitoa kuhakikisha unaendelea kufanya kwa muda mrefu bila kuacha.

Mafanikio makubwa ni sawa na kusukuma jiwe lipande mlima, ukiacha tu kusukuma, linarudi chini na kazi yako yote inakuwa imepotea.

Mafanikio pia ni kama kuendesha baiskeli, itakaa kwenye mwendo kama utaendelea kuchochea.
Ukiacha tu kuchochea, inashindwa kwenda na kuanguka.

Kikubwa tunachotoka nacho hapa ni ili ufanikiwe, unapaswa KUANZA KUFANYA na ukishaanza unapaswa KUENDELEA KUFANYA bila kuacha hata iweje.
Nenda na hayo mawili na hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe