3480; Kujaribu na Kusubiri.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kujaribu na kusubiri ndiyo maneno pendwa ambayo wengi sana huwa wanayatumia.
Na hayo ndiyo yamekuwa kikwazo sana kwa wengi kupata mafanikio makubwa wanayoyataka.
Watu wanapokuwa na kitu cha kufanya, kwanza huwa wanapenda kusubiri.
Wanaweza kujipa sababu mbalimbali za kusubiri, lakini huwa hakuna yenye msingi.
Sababu pekee ya watu kusubiri wasifanye kile wanachopaswa kufanya ni kutokutaka kufanya.
Lakini wanakuwa hawapo tayari kusema wazi kwamba hawataki, hivyo wanajificha nyuma ya kusubiri.
Inapokuwa kwamba hawawezi tena kutumia sababu ya kusubiri, basi husema wanajaribu. Hapo kwenye kujaribu ni kutokutaka tu kujitoa na kufanya kitu kwa uhakika.
Pale sababu za kusubiri zinapokosekana na watu kulazimika kufanya ndiyo huwa wanasema wanajaribu.
Kwa kuwa majaribio huwa yana kufanikiwa na kushindwa, huwa wanashindwa makusudi kwa sababu hawakuwa wanataka kufanya.
Hakuna mafanikio makubwa ambayo yamewahi kujenga kwa watu kusubiri au kujaribu.
Mafanikio ni matokeo ya watu kuwa tayari kufanya na kujitoa mazima kwenye ufanyaji.
Wakishajua kile wanachotaka na wanachopaswa kufanya ili kupata wanachotaka, wanaanza kufanya mara moja.
Hawasubiri mpaka kila kitu kiwe sawa, badala yake wanaanza na kwenda wakiboresha.
Pia hawafanyi kwa kujaribu, bali wanafanya kwa uhakika.
Tunajua maisha tuliyonayo hapa duniani ni tuliyonayo sasa.
Hata tukisubiri, hakuna maisha ya tofauti yanayokuja.
Na pia tukijaribu, maisha hayatusubiri.
Namna pekee ya kuyatumia na kunufaika na maisha ni kuyaishi kwa ukamilifu wake.
Hakuna kusubiri wala kujaribu, ni kufanya kwa uhakika na kujitoa mazima.
Chochote unachofanya, ingia mazima. Hapo hakuna kitakachoweza kukuzuia usifanikiwe.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe