3481; Mapenzi ya muda mrefu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa huwa yanataka mapenzi ya muda mrefu.
Mafanikio hayo makubwa ni matokeo ya kupenda kitu unachofanya kwa muda mrefu bila kuchoka.

Ni mapenzi hayo ya muda mrefu ndiyo yanamfanya mtu kuweza kukabiliana na vikwazo na changamoto mbalimbali ambazo huwa zipo kwenye safari ya mafanikio.

Vikwazo na changamoto hizo ndiyo huwa vinawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa huwa wanaendelea kufanya licha ya hayo wanayokutana nayo.
Hivyo ndivyo wanavyoweza kuyavuka na kuzalisha matokeo makubwa.

Wanaoshindwa huwa wanaacha kufanya pale wanapokutana na hayo magumu.
Na safari yao inakuwa imeishia hapo.

Bila mapenzi makali kwenye kile ambacho mtu unafanya au matokeo unayotaka kupata, hutaweza kuvuka magumu unayokutana nayo na kuendelea kufanya.

Na bila mapenzi hayo kuwa ya muda mrefu, hutaweza kudumu kwenye ufanyaji.,

Kwa bahati mbaya sana mapenzi juu ya kitu hayawezi kufundishwa au kuigwa.
Ni kitu ambacho kinaanzia ndani ya mtu.

Uzuri ni tayari kila mtu kuna kitu ambacho ana mapenzi nacho ya muda mrefu.
Tatizo ni wengi huwa wanapuuza hilo na kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwao.

Kuwa na mapenzi makali na ya muda mrefu kwenye hicho unachofanya au matokeo unayotaka kufanya.
Hayo yatoke ndani yako kabisa na yasiwe ya kuiga au kuigiza.

Kabiliana na kila linalokuja mbele yako bila ya kukata tamaa wala kuishia njiani.
Tatua changamoto na vuka vikwazo vyote unavyokutana navyo kwenye safari yako.
Kwa kufanya hivyo, unaishia kuwa na mafanikio makubwa.

Kutoka kwa kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe