Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Hongereni wote kwa kuendelea kukaa kwenye mchakato wetu wa programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo, kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.
Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.
Moja ya sababu ambazo watu wamekuwa wanazitumia kutokufanya uwekezaji kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha ni riba ndogo inayopatikana kwenye uwekezaji.
Kwa wastani, uwekezaji mwingi unazalisha faida kati ya asilimia 10 mpaka 15 kwa mwaka. Hiyo ina maana mtu akiwekeza milioni 10, kwa mwaka anategemea kupata milioni moja, kwa mwezi chini ya laki moja.
Na hapo ndipo wengi huwa wanaanzia na swali nikiwekeza kiasi fulani, kila mwezi naweza kupata faida kiasi gani? jibu linapokuja kwamba ni chini ya asilimia 1 ya uwekezaji wao ndiyo watapata kama faida kwa mwezi, huwa wanaona ni ndogo sana.

Wengi wanaona wakizungusha fedha hizo hizo walizowekeza, wanaweza kutengeneza faida kubwa zaidi. Na wapo sahihi kabisa kwamba ukizungusha kiasi chochote kile cha fedha, lazima utapata zaidi ya asilimia 1 kwa mwezi. Kwa uzoefu tu, kwa wengi wanaweza kupata zaidi ya asilimia 10 kwa mwezi.
Watu wengi wamekuwa wanatumia kigezo hicho kama sababu ya kutokuwekeza. Na wengi wameenda mbali zaidi na kuwashauri wengine watoe uwekezaji wao na kuingiza kwenye biashara ili wazalishe zaidi.
Sasa swali ni kwa nini mtu uendelee kuwekeza kwa msimamo bila kuacha, ili hali faida unayopata ni ndogo sana ukilinganisha na ambayo ungeweza kupata kwa kuzungusha fedha hizo mwenyewe?
Kwa sababu sisi washiriki watiifu wa programu ya NGUVU YA BUKU tumeamua kwamba tutawekeza kwa msimamo bila kuacha wala kutoa, tunahitaji kuwa na sababu za msingi ambazo tutajivunia nazo mbele ya yeyote.
Hapa tunashirikishana sababu hizo, tuzielewe na kuzitumia wakati wote ili tuendelee kuwekeza kwa msimamo bila kuacha.
MOJA; TUNATUMIA UWEKEZAJI KUFIKIA UHURU WA KIFEDHA.
Uhuru wa kifedha ni pale tunapoweza kuingiza fedha ya kutosha kuendesha maisha bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Ni rahisi kufikia hilo kupitia uwekezaji kuliko biashara. Kwa sababu biashara bado itahitaji maamuzi yako, hata kama una wafanyakazi, ila uwekezaji, hauhitaji chochote kutoka kwako, ni wewe kupokea tu faida, hata kama ni ndogo.
MBILI; TUNATUMIA UWEKEZAJI KUTUNZA UTAJIRI.
Biashara na shughuli nyingine tunazofanya ni kwa ajili ya kuingiza kipato. Kujenga utajiri kunafanyika kupitia uwekezaji. Hivyo sehemu ya kile tunachopata kwenye biashara na shughuli tunazofanya, tunakiwekeza kwa ajili ya kujenga utajiri.
TATU; TUNAPUNGUZA HATARI AMBAYO IPO KWENYE BIASHARA.
Pamoja na faida kubwa ambayo mtu unaweza kuingiza kupitia biashara, bado pia zina hatari kubwa ya kupoteza. Jambo lolote linaweza kutokea na biashara ikaingiza hasara kubwa na hata kufa kabisa. Kama kitu pekee unachokuwa nacho ni biashara, ukianguka itakuwa vigumu kwako kuinuka. Lakini ukiwa na uwekezaji, hata ukianguka kibiashara, una mahali pa kuanzia.

NNE; FEDHA TUNAYOWEKEZA TUNGEKUWA TUMESHAITUMIA.
Uwekezaji tunaofanya siyo kwamba tunatoa mtaji kwenye biashara na kwenda kuwekeza. Badala yake tunawekeza sehemu ya kile tunachojilipa kutoka kwenye biashara. Hivyo hata kama hatutawekeza, hicho kiasi tutakitumia tu. Tumeamua tujibane ili kujenga uhuru wa kifedha, haina mwingiliano wowote na biashara.
TANO; TUNATUMIA NYENZO NYINGINE KUPATA FEDHA ZA BIASHARA.
Tunapotaka kupata mtaji wa kukuza zaidi biashara zetu, kuna nyenzo nyingine nyingi tunazoweza kutumia, tena zinazotupa kiasi kikubwa cha mtaji na nidhamu kwenye kuusimamia. Kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha na kupata wawekezaji ni njia ambazo tunaweza kuzitumia kupata mtaji bila kuathiri uwekezaji wetu.
SOMA; Jinsi Ya Kujenga Utajiri Wa Mwendokasi.
SITA; TUNATAKA KUWA NA UKWASI.
Kuna nyakati biashara zinaweza zisiende vizuri na fedha ikawa ngumu kupatikana. Katika nyakati kama hizo, uwekezaji ambao unakuzalishia faida unakuwa mzuri. Lakini pia inapokuwa ni dharura na unahitaji fedha kwa haraka, uwekezaji unakusaidia. Hatutaki kudhalilika kwa kukosa ukwasi pale tunapokuwa na mahitaji makubwa.
SABA; TUNATAKA UTAJIRI WA KUMWAMBIA YEYOTE KAFIE MBALI.
Tunaposema tunajenga utajiri na uhuru wa kifedha, tunamaanisha kuwa huru kweli, kiasi kwamba hatuwezi kusumbuliwa na yeyote. Unapokuwa unategemea biashara kama njia ya kuingiza kipato, hata kama unapata faida kubwa, kuna nyakati utakutana na watu ambao wanakusumbua lakini huna namna inabidi uende nao tu. Inaweza kuwa ni wateja wakubwa lakini wanakupa wakati mgumu, wawekezaji ambao wanataka makubwa au wafanyakazi ambao wanakuwa kikwazo. Kwenye uwekezaji huhitaji kusumbuka na yeyote. Mtu yeyote akikusumbua unaweza kumwambia nenda kafie mbali, kwa sababu unajua pesa yako inaingia bila kuathiriwa na chochote.
NANE; TUNAJUA UTAJIRI NI KILE KISICHOONEKANA.
Shughuli nyingi tunazofanya na zinaonekana na wengine, siyo zetu peke yetu. Watu wengine nao wanajihusisha nazo, iwe tunataka au hatutaki. Mtu anaweza kufanya kazi kwa miaka mingi, akistaafu na kupata mafao, watu wa karibu watataka nao wanufaike na mafao hayo. Mtu akijenga nyumba kama sehemu ya uwekezaji, siku akitaka kuuza ageuze uwekezaji wake kuwa pesa, atahitajika kuhusisha watu wa familia. Yote hayo ni taabu kwako ambaye kwa miaka mingi ulifanya ili uje kunufaika. Kwa kuwekeza kwenye vitu visivyoonekana kama hisa, hatifungani na vipande, hakuna anayeona na hayupo wa kukusumbua kwenye matumizi ya uwekezaji huo.
TISA; TUNAJUA FAIDA YA UWEKEZAJI HAITOKANI NA KIASI BALI MUDA.
Kwenye biashara, faida inakuwa kubwa, lakini inahusisha kuweka kazi kubwa. kwenye uwekezaji, faida ni ndogo, lakini kadiri muda unavyokwenda, faida inakua zaidi. Yaani faida kubwa ya uwekezaji haitokani na kiasi kilichowekezwa, bali urefu wa muda. Unaweza kuona milioni moja kukupa laki moja kwa mwezi ni ndogo, lakini ukikusanya hizo laki 1 kila mwezi kwa miaka 10, ni kiasi kikubwa sana cha fedha.
KUMI; UWEKEZAJI TUNAOFANYA HAUTUSUMBUI KWA CHOCHOTE.
Uwekezaji tunaofanya, hasa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU ni uwekezaji ambao hautuhitaji kufanya chochote. Yaani tunawekeza na kusahau, huku tukiendelea na shughuli zetu nyingine. Sasa kweli unataka pesa unayowekeza bila kufanya chochote ilete faida sana na ile itakayokusumbua? Bado tutaendekea kusumbuka na hizo kazi na biashara, lakini pia tunajenga ambacho kitatuingizia fedha bila kuhangaika, ambacho ni uwekezaji.
Matajiri wawekezaji, hizo ndizo sababu 10 zinazotufanya tutembee vifua mbele tukifanya uwekezaji kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha. Tuzielewe kwa kina na tuzitumie kwetu wenyewe na kwa wengine wanaotaka kutushawishi tuachane na uwekezaji.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala juu ya hili na washiriki wameweza kutoa maoni yao mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili kujifunza kwa kina zaidi.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;
1. Umewahi kujishawishi au kushawishiwa na wengine kwamba ni bora uzungushe pesa kuliko kuiwekeza? Ulivukaje hilo na kuweza kuendelea na uwekezaji?
2. Zipi sababu zako ambazo utakuwa unazitumia kutetea mpango wako wa uwekezaji kwa msimamo bila kuacha?
3. Kadiri uwekezaji wako unavyokua, ndivyo utakavyopata tamaa ya kutoa na kupeleka kwenye maeneo mengine, je utajizuiaje kwenye hilo?
4. Pale utakapokuwa unahitaji fedha kwa ajili ya kukuza shughuli zako, utatumia njia zipi kupata ili usiingilie uwekezaji wako?
5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.
Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.