Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Hongereni sana wote kwa kuendelea kuwepo kwenye mafunzo ya mauzo ya CHUO CHA MAUZO. Mafunzo haya yana lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi. Matokeo yanayotegemewa yakiwa ni kila muuzaji na kila biashara kukuza mauzo mara mbili ndani ya mwaka mmoja.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi na kuwafuatilia wateja wote kwa ukaribu na msimamo. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wateja wengi, tumekuwa na mchakato wa kuwagusa angalau wateja 100 kila siku kwa kila muuzaji. Mchakato huo una njia mbalimbali za kuweza kuwagusa wateja na kuwa njia nzuri ya kuwafuatilia kwa karibu.

Msimu wa CHUO CHA MAUZO ambao tupo sasa ulianza wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2023 na unakwenda kuisha wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba 2024. Hiyo ina maana kwamba tupo kwenye robo ya mwisho kwenye msimu huu.

Kwenye kumalizia robo hii ya mwisho ya msimu wa CHUO CHA MAUZO, tunakwenda kuwa na changamoto ya 100 kwa 100. Kwenye changamoto hii, kila muuzaji anapaswa kugusa wateja wasiopungua 100 kila siku kwa siku 100.

Lengo la changamoto hii ni kujisukuma kwa kila muuzaji, kuwafikia wateja wengi na kuweza kukuza mauzo kwa uhakika.

Njia za kufikia wateja hao 100 inahusisha mchakato wa kufikia wateja 100 kila siku ambao upo kwenye namba tunazofanyia kazi kila siku. Mchakato huo na maelezo yake viko hapo chini.

MCHAKATO WA KUFIKIA  WATEJA 100 KILA SIKU

Kugusa wateja wasiopungua 100 kila siku inafanyika kwa njia zifuatazo;    

1         RUFAA ZILIZOPIGIWA NA KUWA NA SIFA

Hapa unaomba rufaa kwa wateja waliopo kwenye biashara au kwa watu wa karibu kisha kuwasiliana na rufaa hiyo kuona kama ina sifa. Pale unapokuwa umepewa rufaa na kweli ikawa na sifa, yaani inaweza kuwa mteja wa biashara, ni mteja ambaye umemgusa.

2         WATEJA WALIOTEMBELEWA NA KUKUTWA

Hawa ni wateja waliotembelewa kule walipo na kuweza kukutwa. Hapa wanahesabika wale uliokutana nao na kuongea nao kuhusu biashara yako.

3         SIMU ZILIZOPIGWA NA MAONGEZI KUFANYIKA

Hapa zinahesabiwa simu ambazo zimepigwa na maongezi kufanyika, yaani kuongea na mteja kuhusu biashara yako. Kama simu haikupokelewa au imepokelewa na kukatwa au kuahidiwa kuwatafuta baadaye, haitahesabika. Kwenye kuhesabu, simu zitakazochukuliwa ni zile zenye mazungumzo ya zaidi ya sekunde 30, chini ya hapo haitahesabiwa ni simu iliyokamilika, labda kama mteja amenunua.

4         MESEJI ZA SIMU ZILIZOJIBIWA

Hapa zinahesabiwa meseji za kawaida ambazo wateja wamejibu. Kama meseji zimetumwa ila wateja hawajajibu, hazitahesabiwa.

5         MESEJI ZA WASAP ZILIZOJIBIWA

Hapa zinahesabiwa meseji za wasap ambazo wateja wamejibu. Kama wametumiwa na hawajajibi, hazitahesabiwa.

6         STATUS + BROADCAST ZA WASAP ZILIZOJIBIWA

Hapa zinahesabiwa jumbe ambazo wateja wamejibu kupitia status na broadcast ambazo zimewekwa. Kama watu wameangalia lakini hawajajibu au kuuliza chochote, haitahesabiwa.

7         BARUA PEPE ZILIZOJIBIWA

Hapa zinahesabiwa jumbe za barua pepe ambazo wateja wamejibu au kutuma. Kama wateja wametumiwa barua pepe ila hawajajibu, haitahesabiwa.

8         MAONI YALIYOWEKWA KWENYE MAUDHUI

Hapa yanahesabiwa maoni ambayo wateja wameweka kwenye maudhui yaliyotolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii au njia nyinginezo kama makala kwenye blogu. Kuangalia pekee au kuweka like bila kuandika maoni yoyote haitahesabiwa.

9         WALIOCHUKUA HATUA KWENYE MATANGAZO

Hapa wanahesabiwa wale waliochukua hatua kwenye tangazo ambalo limelipiwa, iwe ni kubonyeza na kuja kwenye wasap, kupiga simu, kutuma ujumbe au kuja moja kwa moja, inahesabiwa hivyo.

10       WALIOKUJA/KUKUTAFUTA WENYEWE

Hapa wanahesabiwa wale wateja ambao wamekuja au kukutafuta wenyewe. Unakuwa hujafanya chochote kwa upande wako wewe kuwafikia, ila wao ndiyo wanaanzisha kukufikia wewe. Watahesabiwa kwamba wamefikiwa.

SOMA; Ukiweza Kufikia Idadi Hii Ya Wateja Kila Siku, Utafanya Mauzo Makubwa.

CHANGAMOTO YA 100 KWA 100.

Kwa siku 100 za kazi (Jumatatu mpaka Jumamosi) kuanzia Jumatatu ya tarehe 15/07/2024 kila muuzaji atapaswa kuwagusa wateja wasiopungua 100.

Kila muuzaji atachagua njia zake za kugusa wateja katika hizo 10 kulingana na aina ya biashara anayofanya na njia inayofanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kisha mwisho wa kila siku ya kazi, kila muuzaji anatuma kwenye kundi la CHUO HA MAUZO taarifa yake fupi ya kuwagusa wateja 100 kwenye siku hiyo.

Ushahidi wa wateja walioguswa utatumwa kwenye kundi la biashara ambayo mshiriki anakuwepo. Ushahidi utakuwa unapitiwa kuhakikisha taarifa zilizotumwa ni sahihi.

Taarifa hiyo itakuwa kwenye mfumo ufuatao;

CHANGAMOTO YA 100 KWA 100.

1. Tarehe; ….

2. Siku ya …./100

3. Jina la muuzaji; ….

4. Jina la Biashara; ….

5. Idadi ya wateja waliofikiwa kwa kutembelewa; ….

6. Idadi ya wateja waliofikiwa kwa maongezi ya simu; ….

7. Idadi ya wateja waliofikiwa kwa kujibu jumbe za aina zote; ….

8. Jumla ya wateja wote walioguswa; …..

9. Jumla ya wateja walionunua; ….

10. Kiasi cha mauzo yaliyofanyika; ….

Taarifa hii fupi itatumwa kila siku ya kazi na kila muuzaji kwenye kundi la CHUO CHA MAUZO.

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.