3484; Kama unataka utajiri, usiwe mbinafsi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kasumba ya watu wengi kudhani kwamba ili kupata utajiri basi wanapaswa kuwa na ubinafsi mkubwa.
Yaani wajijali wao wenyewe tu na kutokuhangaika na mambo ya wengine.

Hivyo ndivyo masikini wengi wanadhani matajiri walivyo na huenda ndicho kinawazuia masikini hao wasipate utajiri.

Njia ya uhakika kwa mtu yeyote kupata utajiri ni kutokuwa mbinafsi.
Na hii haimaanishi kugawa kile ulichonacho kwa wengine ili uonekane ni mtoaji.

Bali inamaanisha kuwapa watu wengine kile ambacho wanakitaka sana.
Ni kawaida ya binadamu kutokupenda kuwa na deni.
Hivyo unapowapa watu kile wanachotaka, wanajiona wakiwajibika kukupa wewe kile unachotaka pia.

Kwenye utajiri, kwa kuwa unachotaka ni fedha, unachopaswa kufanya ni kuwasaidia watu kupata fedha zaidi.

Kwa chochote unachofanya, angalia ni kwa namba gani unawawezesha watu wengine wengi zaidi kupata fedha nyingi.

Chochote unachowauzia, waonyeshe jinsi ambavyo kinaenda kuwaongezea kipato chao au kuwapunguzia gharama zao.

Na hilo lifanyike kwa uhakika, watu waone kabisa pesa ambazo wamepata kwa kujihusisha na wewe.
Hapo watakuwa tayari kukupa wewe fedha pia.

Kwa chochote unachofanya, hakikisha umetoa thamani kubwa sana kwa watu wengine.
Kadiri unavyotoa thamani kubwa, ndivyo pia na wewe unapokea thamani kubwa kutoka kwa wengine.

Ili uweze kutoa thamani kubwa na kuwawezesha wengine kupata fedha zaidi ili nao wakupe sehemu ya fedha hizo ni lazima uweke kazi kubwa sana.

Unapaswa kuweka kazi kubwa kuliko wengine wengi wanavyoweka.
Lazima uwaguse watu kwa namna ambayo hawajawahi kuguswa na wengine.

Na hayo yote yatarudi kwako kwa faida kubwa zaidi.

Wengi huhofia kwamba wakiwapa watu thamani kubwa, hawatarudisha thamani hiyo na hivyo kuwa wamepoteza.

Ukweli ni kwamba huwezi kupoteza kabisa. Ndiyo kuna wachache watachukua na wasikulipe, lakini kuna ambao watakulipa zaidi.

Asili huwa haipendi deni, hivyo inahakikisha unalipwa kwa kadiri ulivyotoa.
Lakini ni lazima wewe uanze kwa kutoa ndiyo upate na siyo kusubiri upate ndiyo utoe.

Wawezeshe wengine kuwa matajiri na wewe utakuwa tajiri bila shaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe