Kwenye maisha na mauzo kiujumla ukiwa mkweli mara zote, mambo mengi utayafanikisha na utakutana na wateja ambao ni bora zaidi.

Ni kweli kila kitu kitu kina faida na hasara, lakini faida za kusema uongo ni chache sana ukilinganisha na ukweli.

Uongo utakupa ushindi kwa siku kwa siku moja na furaha bandia lakini ukweli utakupa ushindi wa muda mrefu na utulivu wa nafsi.

Biashara inayodumu kwa muda mrefu inahitaji wauzaji wanaosema ukweli kuhusiana na kile wanachouza.

Huduma nzuri kwa mteja inategemea imani unayojenga kwa mteja. Maana humuuzii siku moja tu, utamuuzia tena na tena.

Hivyo, sema ukweli kama ulivyo,
Ishi kwa uhalisia wako,
Ambatana na wale ambao wanaweza kuhimili ukweli na weka juhudi kubwa sana kwenye kila unachofanya. Kwa kuzingatia hayo, utaweza kujenga biashara imara na kupunguza msongo wa mawazo.

Huhitaji kuwa na elimu kubwa sana kuwa mkweli katika huduma yako bali unahitaji;

Kujiamini kwanza.
Unapojiamini, hata wateja unaowauzia wanakuamini pia.

Ipende biashara yako.
Ukiipenda biashara yako, hata wateja pia utawapenda. Hutashawishika kuwadanganya. Maana ukiwadanganya, utawapoteza.

Iamini bidhaa yako.
Maandiko ya dini yanasema, imani nikiwa na hakika na yajayo. Hii ikiwa na maana kuwa, bila kujali mapingamizi anayokupa mteja wakati wa mazungumzo na wateja ukisimamia uhalisia utauza.

Amini katika ushindi.
Wahenga wanasema, “aliwazalo mtu ndilo humtokea”. Ukiamini mteja fulani atanunua na ukaongeza juhudi kumshawishi atanunua tu, bila kujali itachukua muda gani.

Tumia maswali kama kinga yako kwa mteja.

Hii iambatane na kusikiliza zaidi ya kuongea. Wakati mwingine wateja wanaweza kuleta suluhu wenyewe wakipewa nafasi.

Kuwa mpole.
Katika uhudumiaji huwezi kutimiza hitaji la mteja, kuna wakati  upole ni muhimu. Wapo wateja wanaohitaji bidhaa tusizonazo, usiwadanganye, waeleze ukweli kuhusiana na huduma yako.

Mauzo sio uongo, bali ni kutoa huduma na bidhaa bora inayoleta suluhu kwa wateja wako.

Wako Wa Daima

Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo.

0767702659 / mkufunzi@mauzo.tz

Karibu tujifunze zaidi