Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Pamoja na kila mtu kuwa na UWEZO WA KUWA TAJIRI, bado ni wachache sana wanaokuwa matajiri. Huku wengi wakibaki kwenye maisha ya umasikini licha ya kuwa na kila fursa ya kutajirika.

Inaweza kudhaniwa kwamba kutokujua ndiyo kunawakwamisha watu kujenga utajiri. Lakini bado wapo wengi wanaojua nini wanapaswa kufanya ili kujenga utajiri, na bado hawafanyi.

Wale wanaotuzunguka, ambao tunatumia nao muda wetu mwingi huwa wana athari kubwa sana kwenye mambo tunayofanya au kutokufanya. Huwa tunawaamini na kuwasikiliza sana wale ambao tuko nao karibu, hata kama hawapo sahihi.

Na hilo ndiyo limekuwa chanzo cha wengi kubaki kwenye umasikini, kwa sababu wanawasikiliza wale ambao hawajajenga utajiri na wala hawana mpango wowote wa kujenga utajiri.

Tunajua kwamba kufanya uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo kwa muda mrefu kunajenga utajiri. Lakini pale tunapozungukwa na watu ambao hawaamini kwenye hilo, wanatushawishi na sisi tusiamini.

Hivyo kama kweli tumedhamiria kujenga utajiri, lazima tujue wazi ni watu wa aina gani ambao hatupaswi kamwe kuchukua ushauri wao kwenye uwekezaji.

1. Wanaotafuta utajiri wa haraka.

Watu wanaofikiria kupata utajiri wa haraka, siyo watu sahihi kuwasikiliza. Watakupeleka kwenye mambo yasiyokuwa sahihi kwa tamaa zao.

2. Wanaotaka utajiri bila kufanya kazi.

Wanaotaka utajiri bila kufanya kazi huwa ni rahisi kuingia kwenye njia zisizo sahihi. Waepuke watu hao kwa sababu chochote watakachokuambia siyo sahihi.

3. Wanaokimbizana na fursa mpya kila wakati.

Kuna watu ambao kila mara wanakuwa na fursa mpya ambayo wanaamini inalipa zaidi. Watu hao ni wa kuwaepuka kwa sababu wanatafuta urahisi ambao haupo.

4. Ambao hawajawahi kuwekeza.

Mtu anapokuambia usiwekeze kwa sababu labda ni hatari au hailipi, angalia kwanza kama yeye mwenyewe anawekeza. Kama hafanyi uwekezaji, ushauri wake hauwezi kuwa sahihi.

5. Wasio na ushahidi na wanachoongea.

Kuna watu huwa wanashauri mambo na ukiwataka wakuonyeshe ushahidi wanakuwa hawana. Kwa kila jambo ambalo watu wanakushauri watake wakuonyeshe ushahidi na kama haupo basi usiwasikilize.

SOMA; Biashara Na Uwekezaji; Kwa Nini Uwekeze Wakati Unaweza Kuzalisha Faida Kubwa Zaidi Kupitia Biashara?

6. Wanaoshauri mambo ya kawaida.

Kuna ule ushauri wa jumla jumla ambao wengi huwa wanautoa, mfano kitu fulani kinalipa sana. Huo ni ushauri ambao kila mtu tayari anakuwa anaujua, hupaswi kuusikiliza. Hiyo ni kwa sababu ushauri huo unakuwa hauna kitu cha tofauti kinachoweza kukusaidia.

7. Wanaolipwa kupitia wewe kufanya wanachokushauri.

Kama mtu anakushauri kitu ambacho ukikifanya analipwa, jua ushauri wake hautakuwa sahihi, bali atavutia upande wake. Hapa ni mfano wa madalali wa aina fulani za uwekezaji ambao wakikushawishi ukawekeza wanalipwa kamisheni. Hapo watakushawishi uwekeze hata kama haina faida kwako.

8. Wanaoahidi faida kubwa ambayo kiuhalisia haiwezekani.

Kuna faida ambazo huwa zinaahidiwa, ambazo kiuhalisia haziwezekani. Kwa mfano faida inayokua mara mbili kila mwezi na kwa msimamo bila kuyumba. Uwekezaji wowote ule huwa una kupanda na kushuka, kama unaahidiwa matokeo yaliyonyooka tu, kuwa na wasiwasi, unadanganywa.

9. Ambao wapo usipotaka kuwa.

Wale wanaokushauri, angalia kwanza wako wapi au wanaelekea wapi, kama walipo au wanakoelekea siko unakotaka kufika wewe, usichukue ushauri wao. Kwa sababu ukichukua ushauri wa waliopo usipotaka kuwa, utaishia kuwa kama wao. Usidanganyike kwamba usikilize maneno yao na siyo kufuata matendo yao, maneno yao ndiyo yamewafikisha walipo, kama hutaki kuwa hapo, yaepuke.

10. Fursa unayoambiwa inakupita usipochukua hatua mara moja.

Fursa nzuri hazijawahi kuwa na ukomo wala mwisho, ikikupita moja, kuna nyingine nzuri inakuja. Unaposhawishiwa uchukue hatua kwenye uwekezaji haraka la sivyo utaikosa fursa ambayo huwezi kuipata tena, kuwa na wasiwasi, hapo unaingizwa kwenye kitu kisichokuwa sahihi. Kwa kuchelewa kuchukua hatua kwenye fursa fulani unaweza kukosa faida ambayo ungepata, lakini haikukoseshi fursa nyingine nzuri.

Kwa orodha hii, utaona wazi kwamba watu wengi kama siyo wote wanaokuzunguka hupaswi kuchukua ushauri wao inapokuja kwenye uwekezaji.

Swali linakuja ni tuwasikilize watu gani sasa kwenye uwekezaji?

Jibu ni tujielimishe sisi wenyewe kwa kutafuta maarifa sahihi na kisha kuchukua hatua na kujitathmini kadiri tunavyokwenda.

Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tunashirikisha na maarifa sahihi ya uwekezaji, tuyatumie hayo kuwa imara. Pia tufuatilie vyanzo vya uwekezaji sahihi ili kupata taarifa kama soko la hisa (https://dse.co.tz/), UTT AMIS (https://www.uttamis.co.tz/) na BOT kwa hatifungani (https://www.bot.go.tz/)

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala juu ya watu hawa wa kuepuka kwenye ushauri wa uwekezaji, sikiliza hapo chini.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Umewahi kupewa ushauri usio sahihi, ukaufuata na ukakugharimu? Ulikuwa ushauri gani na ulikugharimuje?
2. Umewahi kupewa ushauri usio sahihi, ukaukataa na kuepuka kupoteza? Nini kilifanya ukatae na uliwezaje kuvuka ushawishi wa waliokuwa wanakupa?

3. Katika aina hizi za watu wa kuepuka kuchukua ushauri wao kwenye uwekezaji, ni aina ipi ambao wamekuzunguka sana? Unahakikishaje hawawi kikwazo kwako?

4. Ipi umechagua kama njia sahihi kwako kupata taarifa, maarifa, mafunzo na ushauri sahihi wa uwekezaji? Unahakikishaje unakaa kwenye hiyo bila kutetereka?

5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.