3491; Dawa ya wasiwasi wa mafanikio.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna wasiwasi ambao unaambatana na kila hatua ambazo mtu unapiga.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyokuwa na wasiwasi mkubwa.
Unaona kama hukustahili hayo unayoyapata.
Pia unadhani kuna kitu kinaweza kutokea na ukapoteza kila ambacho umepata.
Kitu kimoja ninachotaka kukuambia ni kwamba huo wasiwasi hautakuja kuisha.
Kadiri unavyopiga hatua, ndivyo wasiwasi huo unazidi kuwa mkubwa.
Njia pekee ya kuukabili wasiwasi wa mafanikio unaokuwa nao ni kulipa gharama.
Wasiwasi wa kupoteza huwa ni mkubwa zaidi pale unapokuwa umepata mafanikio makubwa kuliko gharama ambayo umelipa.
Kwa mfano kama umepewa upendeleo wa nafasi fulani na upendeleo huo ukachangia wewe kufanikiwa, utakuwa na wasiwasi sana.
Wasiwasi wako utakuwa ni kama upendeleo huo utaondolewa, basi utapoteza kila kitu.
Unapokuwa umelipa gharama ya kukipata kitu, yaani umeweka kazi kubwa mpaka kupata matokeo, wasiwasi huwa siyo mkubwa sana.
Unajua ni juhudi zako zimeleta matokeo na hata ukipoteza, utaweza kuweka tena juhudi.
Hivyo basi rafiki, kama unapatwa na wasiwasi kwa kuona unaweza kupoteza ulichopata, suluhisho ni rahisi; lipa gharama, jitoe mhanga, weka juhudi kubwa ya kazi na kazana kuwa bora zaidi ya ambavyo upo.
Ni kupitia kufanya hayo ndiyo wasiwasi ulionao utatulia na wewe kuweza kuwa na utulivu wa kupambana kufanikiwa zaidi?
Rafiki, ni wasiwasi gani umekuwa unakupata kwenye hatua unazopiga?
Unakwenda kuukabilije wasiwasi huo ili uendelee kufanya makubwa?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe