Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kwenye maisha huwa kuna makundi matatu ya watu inapokuja kwenye kutoa na kupokea.

Moja ni watoaji ambao huwa wanatoa kile walichonacho bila hata ya kuangalia ni nini wanachoweza kupokea. Hawa kipaumbele chao kikubwa ni kutoa.

Mbili ni wapokeaji ambao huwa wanapokea kile wanachotaka kutoka kwa wengine. Hawa kipaumbele chao kikubwa ni kupotea.

Tatu ni wale wa nipe nikupe, hawa huwa wanatoa pale tu wanapopokea. Hawa husubiri kwanza mpaka wapokee ndiyo na wao wawe tayari kutoa.

Ukiangalia kwenye  makundi hayo matatu, unaweza kusema ni kundi lipi linalopata zaidi?

Jibu siyo wapokeaji bali ni watoaji. Ni wale ambao wanatoa kwanza ndiyo huwa wanaishia kupata zaidi. Hiyo ni kwa sababu utoaji huwa unatengeneza pengo ambalo lazima lizibwe.

Ili uweze kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea na ufanye mauzo makubwa, unapaswa kuwa mtoaji. Ni kupitia kutoa ndiyo unatengeneza hali ya deni ambalo lazima lilipwe.

Falsafa ya kuwapa wengine wanachotaka ili upate unachotaka.

Kwenye maisha huwa kuna falsafa nyingi ambazo watu wanajihusisha nazo. Moja ya falsafa bora kwenye mafanikio ni hii; UNAWEZA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA KWENYE MAISHA YAKO KAMA UTAWASAIDIA WENGI ZAIDI KUPATA KILE WANACHOTAKA.

Hii ni falsafa rahisi na ambayo kila mtu anaweza kuifuata na kunufaika nayo. Huhitaji kujua siri nyingi sana za mafanikio. Unachohitaji ni kujua watu wengine wanataka nini na kuwapa, halafu na wewe utapata unachotaka.

Tunaona hapa kwamba wewe ndiye unayeanza kutoa kisha kupotea, kwa sababu unapotoa unatengeneza pengo ambalo lazima litazimwa.

Kama muuzaji, ifanye hii kuwa falsafa yako ya maisha, kuwapa wengine wengi kile wanachotaka ili na wao wakupe unachotaka.

SOMA; Kuwa Bora Kwenye Majadiliano Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

Faida za kutoa kwanza kabla ya kupokea.

Falsafa hii ya kutoa kwanza kabla hujapokea ina faida nyingi, baadhi ya hizi ni;

1. Kutengeneza hali ya utupu ambayo lazima izibwe. Asili huwa haipendi utupu, hivyo huchukua hatua ya kuziba haraka. Unapotoa, palipobaki wazi huwa panajazwa.

2. Kutengeneza deni ambalo lazima lizibwe. Unapowapa watu kitu kabla wewe hujawapa chochote huwa inatengeneza hali ya deni ambalo watu huona wanalazimika kulipa.

3. Kutoa fursa ya kuonyesha thamani kabla mtu hajafanya maamuzi. Mara nyingi wateja huwa hawajui ni thamani gani wanayoenda kuipata pale wanaponunua. Kwa kutoa kabla, watu wanaonyesha thamani waliyonayo na jinsi inavyowafaa wengine.

Kila muuzaji anapaswa kuwa na kipaumbele kukubwa kwenye kutoa kabla ya kupokea ili aweze kuwa bora na kufanya mauzo makubwa.

Jinsi ya kutumia utoaji kufanikiwa kwenye mauzo.

Kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa ndiyo matokeo tunayoyataka kupata ili kufanikiwa kwenye mauzo. kwa kutumia falsafa ya kutoa kabla ya kupokea tunaweza kufanikiwa sana kwenye mauzo.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili kutumia utoaji kufanikiwa kwenye mauzo.

1. Ijue biashara yako na wateja unaowalenga.

Huwezi kuanza tu kutoa na kudhani utapokea. Ni lazima kwanza uijue biashara yako vizuri na kuwajua wateja unaowalenga. Kwenye kuijua biashara yako unajua ile thamani unayoitoa. Kwenye kuwajua wateja unaowalenga unajua mategemeo yake.

2. Angalia vitu unavyoweza kutoa ambavyo havina gharama kubwa.

Angalia vitu ambavyo unaweza kuvitoa kwenye biashara bila ya kuingia gharama kubwa kwenye utoaji wake. Ni kweli tunahitaji kutoa bila kuangalia tunachopokea, lakini lazima tuepuke kuzalisha gharama kubwa kwenye hilo.

3. Toa bila kuangalia nini unapokea.

Ukishajua thamani unayotoa na mahitaji ambayo wateja wanayo, anza kuwapa watu vitu vyenye thamani kwao bila ya kutegemea kupokea chochote kutoka kwao. Unawapa thamani uliyoandaa kwa ajili ya utoaji, bila ya kuangalia ni nini hasa unachopata kutoka kwao.

Ni kutoa kwa moyo mkunjufu ndipo manufaa huwa yanaonekana. Huwa yanakuja yenyewe kabla hata hayajalazimishwa.

Changamoto za kutoa kabla ya kupokea.

Pamoja na nguvu kubwa ya kutoa kabla ya kupokea kwenye kufanya mauzo makubwa, huwa kuna changamoto zake. Changamoto hizo ndizo huwakatisha watu tamaa na wasitumie njia hii kuwa bora na kufanya mauzo makubwa.

Baadhi ya changamoto na utatuzi wake ni kama ifuatavyo;

1. Kukutana na wapokeaji wasiotoa.

Moja ya vitu vinavyowafanya wauzaji wengi wasiwe watu wa kutoa kabla ya kupokea ni kufikiria watu ambao huwa wanapokea lakini siyo watoaji.

Hili lisikusumbue sana, kwa sababu hutegemei wote wanaopokea wakupe ndiyo ufanikiwe. Badala yake unahitaji watu wachache wawe tayari kulipa baada ya kupokea.

Kwa mfano kama katika watu 10 unaotaka kuwauzia ni mmoja pekee anayekubali kununua. Kama ukitumia njia ya kutoa kabla ya kupokea, watatu wakakubali kununua kati ya 10 ni ushindi mkubwa sana.

Hivyo usiangalie wote unaowapa kulipa, bali angalia wachache ambao wanafanya hivyo na hilo linaongeza matokeo.

2. Kuingia gharama kubwa na hivyo kukosa faida.

Kutoa kabla ya kupokea inaweza kuonekana kuongeza gharama na hivyo kupunguza faida. Kwa sababu kuna ambao watapewa na hawatalipa hivyo kile kilichotolewa kuwa kimepotea.

Kwanza kabisa lazima tuelewe kinachotolewa siyo chenye gharama kubwa. Watu hawahitaji kupokea kitu chenye gharama kubwa ndiyo wajione wana deni. Badala yake wanapaswa kuona wamepata thamani nzuri.

Hivyo cha kuangalia ni thamani gani unaweza kuwapoa wateja ambayo haiingizi gharama kubwa kwenye biashara. Mfano kuwapa wateja mafunzo na ushauri ni kitu chenye thamani kwao lakini hakina gharama kwenye biashara.

Angalia thamani unayoweza kutoa kwa wateja lakini isiyo na gharama kwenye biashara na ufanye hivyo.

3. Kutokuwa na cha kutoa.

Wauzaji wengi huwa wanaona hawana kitu cha kuwapa wateja kabla hawajawauzia walichonacho.

Hii pia ni kama changamoto iliyopita, usiangalie tu kile unachouza, bali angalia mahitaji ambayo mteja anayo na namna ya kumsaidia kuyapata. Inaweza kuwa ni kumfundisha au kumshauri jambo lenye manufaa kwake. Lakini pia inaweza kuwa ni kumuunganisha na watu ambao watakuwa na manufaa kwake.

Kumbuka kilicho muhimu siyo nini unachotoa, bali jinsi mteja anakipokea na kikawa na manufaa kwake. Huwezi kuwa kwenye biashara halafu ukose kitu cha kutoa chenye manufaa kwa wateja.

Sisi binadamu kwa asili ni wabinafsi, huwa tunaangalia tunapata nini kwanza kabla hatujatoa. Ukiwa mtu wa kutoa kabla ya kupokea, ukijali maslahi ya wengine na kuyatimiza, utatengeneza pengo na deni linalowasukuma wengine kutaka kukulipa. Kwa wewe kuwa mtoaji kabla ya kuangalia nini unapata utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wateja wako, kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.