3492; Bado Usingetoboa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wanatofautiana kwenye kitu kimoja tu, KUTAKA.

Wanaofanikiwa wanataka kufanikiwa na hivyo hawakubali kingine chochote isipokuwa mafanikio wanayoyataka.

Wakati wanaoshindwa wanakuwa wanatamani mafanikio, ila hawayataki hasa.

Pale kitu chochote kinapotokea kwenye safari ya mafanikio, wanaofanikiwa wanaendelea na safari kama vile hakuna kilichotokea.

Wakati wanaoshindwa wanatumia kama sababu ya kutokufanikiwa.

Unaona hapo rafiki, ni unataka nini ndiyo inaamua unapata nini.

Unakutana na mtu anakuambia hajafanikiwa kwa sababu hakuungwa mkono na watu wengine.

Kama kutokuungwa mkono na wengine kunatosha kukuzuia kufanikiwa, bado usingetoboa, hata ingekuwaje.

Sababu yoyote ile utakayotumia kushindwa kufanikiwa, ni kujiridhisha tu.
Lakini ukweli ni kwamba hukuyataka hasa mafanikio.

Kwa hiyo chochote tu kingekuondoa, hata kama siyo hicho unachosingizia.

Ni sawa na mtu mwenye UKIMWI, kuna ugonjwa utamuua, lakini hata usingekuwa ugonjwa huo, kuna mwingine ungemwondoa tu, maana tayari mwili wake una udhaifu.

Kama na wewe una udhaifu kwenye mafanikio, utaondolewa kirahisi sana kwenye hiyo safari.
Chochote kile kitakukwamisha usifanikiwe.

Hapo kikwazo siyo hicho cha nje, bali kile kilocho ndani yako wewe.

Je ni nini kinachoweza kukutoa wewe kwenye safari yako ya mafanikio?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe