Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Hatua ya kwanza na muhimu ya kuwatengeneza wateja wapya tarajiwa ni kupata taarifa zao. Yaani kuwajua ni nani, wako wapi, wanafanya nini na mawasiliano yao ni yapi.

Kwa kuwa na taarifa hizo za msingi kuhusu wateja wapya tarajiwa, inakuwa rahisi kuwafikia na kuweza kuwachuja kama wanafaa kuwa wateja wa biashara au la.

Huwa kunakuwa na orodha mbalimbali ambazo zinatunza taarifa za watu na biashara zilizopo kwenye eneo fulani au sekta fulani. Orodha hizo huwa zimeandaliwa kama njia ya watu kupata taarifa muhimu wanazohitaji kupata kuhusu watu, biashara na taasisi kwenye eneo au sekta husika.

Uwepo wa orodha hizo unatoa nafasi ya kuweza kuwafikia watu hao na kuona kama wanafaa kuwa wateja wa biashara. Hivyo basi, orodha mbalimbali zilizopo ni njia nzuri ya kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa kwa wingi.

AINA YA ORODHA ZINAZOWEZA KUTUMIKA KUWAFIKIA WENGI.

Kuna orodha nyingi ambazo zipo na zenye taarifa za watu wengi waliopo kwenye eneo au tasnia fulani. Baadhi ya orodha hizo ni kama ifuatavyo;

1. Orodha ya namba za simu za watu waliopo kwenye eneo au sekta fulani. Japo hii ilikuwa ya zamani, mpaka sasa bado huwa kuna orodha ya namba za simu za watu walio kwenye eneo au tasnia fulani. Kwa kuanza na orodha hiyo unaweza kuwafikia wengi.

2. Orodha za biashara, kampuni na taasisi zilizopo kwenye eneo au tasnia fulani. Zipo orodha ambazo zinatunza taarifa za biashara, kampuni na taasisi zilizopo kwenye eneo au tasnia fulani. Ni mahali pazuri pa kupata wateja tarajiwa wengi.

3. Orodha ya watu waliopata huduma kwenye taasisi fulani, hasa za kiserikali. Baadhi ya taasisi, hasa za kiserikali huwa zinaweka orodha ya watu waliopata huduma kwao. Mfano mamlaka ya kodi (TRA), mamlaka ya kusajili makampuni (BRELA), Mahakama, ofisi za serikali n.k. Hizo ni sehemu ambazo zikifuatiliwa vizuri taarifa za wateja tarajiwa zinapatikana.

4. Watu wanaoandaa na kukodisha au kuuza orodha mbalimbali. Kuna watu au biashara ambazo huwa zinaandaa orodha za watu na taasisi mbalimbali kisha kuzikodisha au kuuza kwa wale wenye uhitaji nazo. Kwa njia hiyo pia unaweza kupata wateja tarajiwa wengi.

5. Orodha za wataalamu wa aina mbalimbali. Taaluma mbalimbali huwa zinakuwa na orodha za wataalamu walio kwenye taaluma hizo. Kwa mfano madaktari, walimu, wahasibu, wanasheria, wahandisi n.k. Kupitia orodha hizo unaweza kuwafikia wale unaowalenga.

6. Maeneo ambayo watu wanaingia kwa kujiandikisha. Kuna sehemu ambazo watu huwa wanaingia kwa kujiandikisha mfano majengo na ofisi, iwe ni kwa kuandika kwenye daftari au kwa njia nyingine. Kwa kuwa na ushawishi na kuweza kupata taarifa hizo, zinaweza kutumika kufikia watu wengi na kuona kama wanafaa kuwa wateja tarajiwa wa biashara.

Popote penye fursa ya kupata taarifa za watu, kuna fursa ya kufikia watu wengi na kuwachuja wale wanaoweza kuwa tarajiwa kwenye biashara yako.

SOMA; Tumia Kampeni Maalumu Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

HATUA ZA KUCHUKUA KWENYE ORODHA ILI KUTENGENEZA WATEJA TARAJIWA WENGI NA KUKUZA MAUZO.

Ili kukuza mauzo, tunahitaji kutengeneza wateja tarajiwa wengi ambao wana sifa za wateja wanaolengwa na biashara. kwenye kutumia orodha mbalimbali kuwafikia wengi, hatua zifuatazo ni za kuzingatia ili kuweza kutengeneza wateja tarajiwa wenye sifa wengi na kukuza mauzo.

1. Jua sifa za wateja walengwa wa biashara.

Kabla ya kutumia orodha yoyote, anza kwa kujikumbusha sifa za wateja walengwa wa biashara unayofanya. Siyo kila mtu anaweza kuwa mteja, bali kuna watu wenye sifa za aina fulani ndiyo wanaofaa kuwa wateja. Jikumbushe sifa hizo za wateja walengwa mara zote.

2. Chagua orodha zenye watu wenye sifa za wateja walengwa.

Baada ya kujua sifa za wateja ambao biashara inawalenga, unakwenda kuchagua orodha ambazo zinaweza kuwa na watu wenye sifa zinazoendana na wateja walengwa wa biashara. orodha zipo nyingi na zinazotofautiana, wewe chagua zile ambazo wateja unaowalenga wapo ndani yake.

3. Chagua watu utakaoanza nao.

Orodha huwa zinakuwa na watu wengi na siyo wote watakaoweza kuwa wateja tarajiwa wenye sifa kwa biashara yako. Hivyo ukishachagua orodha, kinachofuata ni kuchagua watu gani ambao utaanza nao. Hapo unaanza na sifa za msingi za wateja unaowalenga ili kuwatenga wale ambao huhitaji hata kuwafikia kwa sababu hawana sifa kabisa.

4. Anza mawasiliano na wale uliowachagua.

Baada ya kuchagua watu utakaoanza nao, unaanza kufanya nao mawasiliano ya kuwachuja kama wana sifa za kuwa wateja wa biashara yako. Kwenye mawasiliano ya awali utayatumia kuendelea kuwajua na kuona kama wanafaa kuwa wateja. Kama hawafai wanawekwa pembeni na kama wanafaa wanaendelea kufuatiliwa mpaka wawe wateja kamili.

5. Endelea kuboresha taarifa kadiri ya unavyozipata.

Orodha nyingi huwa zina taarifa fupi kuhusu watu, ambazo haziwezi kutosha kwa mtu kufanya maamuzi. Lakini pia wakati mwingine taarifa zinazokuwa kwenye orodha zinaweza zisiwe sahihi au zilizopitwa na wakati. Hivyo kadiri unavyoendelea kuwasiliana na wale waliotolewa kwenye orodha, taarifa zao zinapaswa kuboresha ili ufuatiliaji uwe rahisi na wenye ushawishi zaidi.

Moja ya orodha ambazo biashara nyingi zinaweza kutumia kwa Tanzania ni orodha ya biashara. Hiyo imekusanya taarifa za biashara nyingi kwa maeneo na sekta. Uzuri ni orodha hiyo inaweza kufikiwa kwa njia ya mtandao. Kuifikia ingia; https://ncd.co.tz kisha tafuta kwa sifa unazoangalia, yaani aina ya biashara na eneo.

Orodha mbalimbali zilizopo, ambazo tayari zina taarifa za watu wengi, ni njia rahisi ya kuweza kuwafikia wengi na kutengeneza wateja tarajiwa wenye sifa kwa wingi. Kila biashara inapaswa kutumia orodha zilizopo ili kutengeneza wateja tarajiwa wengi na ambao watafuatiliwa kwa karibu na msimamo mpaka wawe wateja kamili. Hilo litawezesha mauzo ya biashara kukua na malengo yaliyopo kufikiwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.