3493; Angalau unapenda.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Imekuwa inashauriwa sana mtu kupenda kile unachofanya ndiyo uweze kufanikiwa.

Watu wamekuwa wanachanganya hilo, wakidhani kinacholeta mafanikio ni yale mapenzi ambayo mtu anayo kwenye kile anachofanya.

Ndiyo maana inapotokea mtu akafanikiwa kwenye kitu asichopenda au akashindwa kwenye kitu anachopenda, inaonekana kama mapenzi hayana nafasi kwenye mafanikio.

Ukweli ni kwamba nafasi ya mapenzi kwenye mafanikio ya kile ambacho mtu unafanya ipo, lakini siyo ndiyo kisababishi kikuu.

Tunajua kazi ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya aina yoyote ile.
Yeyote anayeweka kazi kubwa na yenye tija, atafanikiwa, iwe anapenda au hapendi kile anachofanya.

Mapenzi yanakuja kuingia kama kichocheo, hasa kwetu sisi binadamu ambao tunaendeshwa na hisia kuliko mantiki.
Ndiyo maana pamoja na kuweka kazi, mapenzi kwenye kile tunachofanya yana nafasi yake.

Iko hivi rafiki, kujenga mafanikio makubwa kwenye kitu chochote kile ni kazi kubwa na ngumu.  Kuna maumivu na mateso makali. Na pia kuna kushindwa na kukatishwa tamaa.

Yaani pale tu unapoamua unayataka mafanikio makubwa, dunia nzima inakugeuka na kukushambulia kuhakikisha huyapati mafanikio hayo.

Kitu pekee kitakachokuwezesha kuyavuka yote hayo na kubaki imara ukipambana ni mapenzi ya dhati kwenye kile unachofanya.

Kama kukifanya tu kitu kunakuridhisha wewe, kwa kukufanya ujisikie amani licha ya magumu unayokuwa unapitia, utaweza kuendelea na mapambano bila ya kuacha.

Ni kuendelea kwako na mapambano bila kuacha ndiko kunakupa mafanikio kwa uhakika.

Kwa sababu mwisho wa siku, wa mwisho ndiye mshindi.
Anayedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye kile anachofanya ndiye anayepata mafanikio kwa uhakika.

Hivyo basi rafiki, fanya unachopenda na kubali hicho ndiyo kikuue.
Yaani kataa kabisa kuacha au kuishia njiani, hata kama unakutana na magumu kiasi gani.
Hivyo ndivyo unavyojipa uhakika wa mafanikio.

Kwenye safari yako ya mafanikio, nini unachopenda sana kufanya ambacho haupo tayari kukiacha kwa kipindi chote cha maisha yako?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe