3495; Ni Ujuzi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Uzuri mmoja kuhusu mafanikio ni kwamba, yapo wazi kwa watu wote.
Hilo linadhihirishwa na jinsi ambavyo kila aina ya watu, pamoja na kutofautiana sana, bado wanafanikiwa.
Wenye umri mdogo wanafanikiwa, wakati pia wenye umri mkubwa wanafanikiwa.
Wenye akili nyingi wanafanikiwa, wakati pia wasio na akili nyingi wanafanikiwa.
Jinsi ambavyo baadhi ya watu kwenye kila kundi wanafanikiwa, huku wengine wengi wakishindwa kimekuwa ni kitendawili ambacho wengi hawajaweza kukitegua.
Lakini jibu la kitendawili hicho ni rahisi sana.
Mafanikio ya aina yoyote ile, ni ujuzi tu.
Ujuzi ikiwa na maana ni kitu ambacho mtu anajifunza au kufundishwa.
Kwa maneno mengine siyo kitu ambacho mtu anazaliwa nacho.
Na hizo ni habari njema sana kwa kila mpenda mafanikio, kwa sababu hakuna cha kukuzuia kufanikiwa isipokuwa wewe mwenyewe.
Ni wewe tu uamue mafanikio gani unayoyataka, kisha ujue ujuzi unapaswa kuwa nao ili kupata mafanikio hayo.
Pale unapomuona mtu yeyote amefanikiwa kuliko wewe, jua kuna kitu anajua ambacho wewe hujui.
Wajibu wako ni kujenga ujuzi ambao utakupa mafanikio unayoyataka kwenye maisha yako.
Kulingana na ukubwa wa mafanikio unayoyataka, ujuzi unaopaswa kujenga utakuwa tofauti pia.
Kama unataka mafanikio makubwa, lazima uwe tayari kujenga ujuzi mkubwa.
Ambao utakutaka ufanye kazi sana na kwa muda mrefu.
Utalazimika kufanya mambo ambayo huyajui na utashindwa kwenye kuyafanya.
Lakini kadiri unavyoendelea kujifunza na kufanya, ndivyo unavyozidi kuimarika kwenye ujuzi huo na kupata mafanikio makubwa.
Rafiki, ni ujuzi gani unaoona unahitajika kujijengea ili upate mafanikio makubwa unayoyataka?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili tushauriane namna bora ya kujijengea ujuzi huo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe