3497; Kinga ya Kushindwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hofu ya kushindwa imekuwa kikwazo kikubw kwa wengi kupata mafanikio makubwa wanayoyataka.
Hofu hiyo ya kushindwa imekuwa inaweza kuwazuia hata wale ambao wangeweza kufanya makubwa sana.
Hofu hiyo inawazuia hata kuchukua hatua, ambazo zingeweza kuwapa mafanikio kwa uhakika.
Hofu ni sehemu yetu binadamu, hatuwezi kuondokana nayo kabisa.
Hivyo tunapaswa kuwa na kitu kinachotuwezesha kufanya, licha ya hofu tunayokuwa nayo.
Na kitu tunachoweza kukitumia vizuri kuwa na kinga ya kushindwa.
Yaani tunajikinga kabisa kushindwa.
Pamoja na hofu ya kushindwa tunayokuwa nayo, tunakuwa tunajua kabisa kwamba hatuwezi kushindwa, kwa sababu tayari tunayo kinga.
Kinga ya kushindwa ina vipengele vifuatavyo;
Kwanza ni utayari kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa na kutokuishia njiani.
Wewe unachagua kuweka kazi na kazi unaiweka hasa.
Kwa kuwa kazi ndiyo msingi mkuu wa mafanikio, huwezi kushindwa kama hutaacha kuweka kazi.
Mbili ni kuwa mbele zaidi ya wengine wanaofanya kile unachofanya.
Hapa unahakikisha unawazidi ujanja, kwa kuwa na vitu unavyofanya ambavyo wao hawawezi kufanya.
Unajipa upekee wako kwa unayofanya na kupelekea watu kuja kwako kwa sababu vile unavyowapa hawawezi kupata mahali pengine.
Hebu fikiria utashindwaje kama watu wanategemea kitu ambacho wanakipata kwako tu?
Tatu ni kuweka mbele maslahi ya wateja wako, wale wanaopokea kile unachofanya au kutoa. Wape thamani kubwa sana ambayo hawawezi kuikataa. Kwa sababu wanaona wananufaika sana kupitia wewe.
Unapojipa wajibu wa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora kupitia unachofanya, hakuna namna utashindwa.
Nne ni kutaka mafanikio makubwa. Ukubwa wa mafanikio unayotaka utachangia kwenye msukumo utakaopata kwenye kuyafikia. Ukitaka mafanikio kidogo, msukumo unakuwa mdogo na hofu inakushinda kirahisi.
Ukitaka mafanikio makubwa sana, msukuko nao unakuwa mkubwa ambao utaweza kuishinda hofu.
Taka mafanikio makubwa na jione ukiwa umeyapata na hutaweza kushindwa.
Tano ni shauku kubwa kwenye mambo yote unayoyafanya. Hofu na shauku haviwezi kukaa mahali pamoja. Shauku kubwa inaiweka hofu pembeni.
Kwa kuwa na shauku ya mafanikio na kwa yote unayofanya, mafanikio yanakuwa uhakika kwako.
Rafiki, haya yote yapo ndani ya uwezo wako kuyatumia.
Swali ni je utakwenda kuyatumia ili mafanikio yawe uhakika kwako?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe