3498; Umasikini na Aibu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Umasikini na aibu ni vitu ambavyo havipaswi kukaa mahali pamoja.
Hiyo ina maana kwamba kama ni masikini, basi hupaswi kuwa na aibu.
Kwa sababu aibu yako itakudidimiza kwenye kina kirefu zaidi cha umasikini wako.
Unapokuwa masikini, unapaswa kuwa tayari kufanya chochote ambacho siyo kinyume na sheria wala maadili, ili upate pesa.
Ukianza kujiwekea vigezo na hadhi, wakati huna pesa, haitakusaidia.
Ukiwa huna pesa, halafu ukaamua kuweka aibu pembeni, ni rahisi sana kupata pesa.
Unachohitaji ni kuchagua kitu chochote na kukiuza moja kwa moja kwa watu.
Na jinsi ya kukiuza ni kupitia;
Kubisha mlango kwa mlango kukutana na watu na kuwashawishi wanunue. Ukibisha milango 50 kwa siku, hutakosa 5 wa kuwauzia.
Kupiga simu kwa watu kuwashawishi wanunue. Ukipiga simu 100 kwa siku, hutakosa 10 wa kuwauzia.
Kutuma jumbe kwa njia mbalimbali kwa watu kuwashawishi wanunue. Ukituma jumbe 1000 kwa siku, hutakosa 10 wa kuwauzia.
Unaweza kuniambia nini kitakuzuia kuchukua hizo hatua hapo juu kama siyo kuona aibu?
Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kukuza biashara yako.
Hata kama huna mtaji mkubwa au wafanyakazi, ondoa aibu na fanya kile unachoweza katika kuwafikia wateja wengi zaidi.
Pesa hazitakufuata zenyewe na aibu yako. Ni lazima wewe uzipambanie ndiyo ziweze kuja kwako.
Weka aibu pembeni ili uweze kutengeneza pesa kadiri ya unavyotaka.
Rafiki, umeruhusu aibu ya nini kukukwamisha kutengeneza kipato kikubwa zaidi ya unachopata sasa?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili uweze kuvuka aibu hiyo na ufanye makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe