3499; Sababu haijulikani.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa hatuwezi kutulia kama hatujajua sababu ya kitu kutokea.
Hivyo kama kuna kitu kimetokea na hatujajua sababu, huwa tunatafuta sababu yoyote itakayotufaa.
Tunachotaka tu ni kuwa na utulivu kwa kujua sababu ya kila kitu.
Hilo la kutaka sababu ya kila kitu huwa linatupoteza mara nyingi kuliko kutusaidia.
Hiyo ni kwa sababu tunajikuta tukiwa na sababu nyingi ambazo siyo za kweli.
Matokeo yake ni hatujifunzi kutokana na sababu hizo na hivyo hazitusaidii.
Zaidi ni sababu zisizo sahihi zinatupoteza zaidi.
Chukua mfano wa mtu ambaye amefariki dunia ghafla.
Watu wanakuwa hawajui sababu ya mtu huyo kufariki ghafla.
Hivyo wanaanza kutafuta sababu na kujua kuna mtu hakuwa na maelewano naye.
Hapo wanapata sababu kwamba huyo ambaye hakuwa na maelewano naye amemloga.
Hapo wanaridhika na sababu, lakini siyo ya kweli na wala haiwasaidii.
Huenda mtu huyo alikuwa na ugonjwa sugu ambao watu hawakuwa wanajua.
Wangejua sababu halisi wangejifunza ili nao watunze afya zao.
Ni vyema pale ambapo hatujui sababu ya uhakika kuacha kutafuta sababu zetu wenyewe.
Bora tuwe tayari kujiambia kwamba sababu haijulikani kuliko kujipa sababu ambazo siyo sahihi.
Tuwe tayari kukosa utulivu wa kutokujua sababu kuliko kujifariji na sababu zisizokuwa sahihi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
0678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com