Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kuna njia nyingi za kutengeneza wateja wapya tarajiwa kwenye biashara, njia ambazo zinatufikisha kwa wateja moja kwa moja. Njia kama kutembelea wateja na kuwapigia simu huwa zina nguvu ya kutengeneza wateja wapya tarajiwa.

Mtandao wa intaneti ni njia inayoweza kutumika kuwafikia watu wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa. Hilo linawezekana kwa pande mbili.

Upande wa kwanza ni kwa biashara kuweka taarifa zake kwenye mtandao wa intaneti, kupitia kuwa na tovuti, blogu na kurasa kwenye mitandao ya kijamii.

Upande wa pili ni kutafuta taarifa za watu na biashara nyingine kwenye mtandao huo wa intaneti na kuzitumia kuwafikia na kuwachakata ili kuona kama wanafaa kuwa wateja tarajiwa.

Kwenye masomo ya nyuma na kwenye kitabu cha CHUO CHA MAUZO tumeshajifunza sana upande wa kwanza wa biashara kuweka taarifa zake kwenye mtandao wa intaneti ili kupatikana na wale wanaotafuta taarifa mbalimbali zinazoendana na biashara.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza upande wa pili ambao ni kutafuta taarifa za biashara nyingine kwenye mtandao wa intaneti na kuzichakata ili kupata wateja wapya tarajiwa.

MCHAKATO WA KUTUMIA MTANDAO WA INTANETI KUTENGENEZA WATEJA WAPYA TARAJIWA.

Mchakato wa kutumia mtandao wa intaneti kutengeneza wateja wapya tarajiwa una hatua saba kama ifuatavyo;

Hatua ya kwanza; tafuta tasnia husika.

Ingia kwenye mtandao wa intaneti, sehemu ya kutafuta taarifa mbalimbali kisha tafuta watu na biashara zilizopo kwenye tasnia unayotafuta wateja wapya tarajiwa. Unapotafuta andika jina la tasnia na eneo ambalo unataka kuwapata wateja tarajiwa.

Mfano; kama unafanya biashara inayowalenga wauzaji wa vifaa vya ujenzi na upo Arusha, ingia kwenye mtandao wa google na andika; Wauzaji wa vifaa vya ujenzi Arusha, kisha tafuta. Kama kutafuta kwa Kiswahili hakutakupa majibu mazuri, tafuta kwa Kiingereza, kwa mfano huo hapo utatafuta; Hardwares in Arusha.

Hatua ya pili; chagua majibu 10 ambayo unaona yanakufaa zaidi.

Hatua ya kwanza hapo juu itakuletea majibu mengi ya watu na biashara zilizopo kwenye tasnia na eneo ulilotafuta. Utayapitia majibu yote ambayo yameorodheshwa na kuchagua majibu 10 ambayo yanakufaa zaidi. Taarifa zitakazoonekana ni za jina la mtu au biashara na njia za kuwasiliana nao, ikiwepo tovuti, kurasa za mitandao, barua pepe, namba za simu na eneo ambapo biashara ipo.

Kwa biashara ambazo zina ukurasa wa google, utaonyeshwa kwenye kutafuta na huo huwa una taarifa nyingi mpaka maelekezo ya mahali biashara ipo. Kwa kupitia taarifa zinazopatikana, utapata njia nyingi za kufikia biashara hizo.

Hatua ya tatu; tumia mawasiliano uliyopata kuwafikia wale uliowachagua.

Kwa majibu uliyochagua, ambayo unaona yanakufaa zaidi, tumia mawasiliano uliyopata kuweza kuwafikia. Mawasiliano ya kwanza kutumia kama yanapatikana ni namba ya simu. Kama hiyo haijapatikana unaweza kutumia barua pepe kutuma ujumbe.

Unapowasiliana na mtu au biashara ambayo umepata mawasiliano yake mtandaoni, mara nyingi utafikia kwa watu wa mapokezi au wasaidizi ambao siyo wafanya maamuzi unaowalenga. Hivyo unahitaji kuwa na mkakati mzuri ili uweze kuwafikia wahusika. Njia nzuri ya kufanya hivyo ni kujitambulisha wewe mwenyewe kisha kumuulizia mtu anayehusika na kile unachouza.

Mfano; Habari, naitwa John kutoka ABC, wewe ni…? Vizuri …. (taja jina lake alilojitambulisha nalo), ningependa kujua nani anayehusika na …. (taja eneo linalohusiana na kile unachouza). Kwenye hatua hii epuka kuonekana kama kuna kitu unataka kuwauzia, badala yake onekana una taarifa muhimu ambazo unataka kuwashirikisha ili wanufaike. Na hii siyo kudanganya, bali ni kuhakikisha unavuka kikwazo ambacho wauzaji wengi hukwama mwanzoni kabisa.

SOMA; Tumia Orodha Mbalimbali Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

Hatua ya nne; mfikie mtu sahihi.

Kwa kufanya mazungumzo kwa usahihi na uliyempata kwenye mawasiliano ya awali, utaweza kupata jina na mawasiliano ya mtu anayehusika na kitengo kinachoendana na unachouza wewe. Wakati mwingine, hasa kwa wateja wa mwisho unayewasiliana naye anakuwa ndiye mhusika mkuu.

Ukishawapata watu sahihi omba miadi ya kuwatembelea au kuwasiliana nao kisha kamilisha miadi hiyo kama ulivyopata. Kwenye miadi utajitambulisha kwa ukamilifu kama muuzaji na kuanza mchakato wa mauzo ambapo utamwonyesha mhusika fursa nzuri uliyonayo kwa ajili yao.

Kuendelea kupata taarifa zaidi kwenye hatua hii;

1. Kama umepata jina la mhusika unayetaka kumfikia lakini hujapata mawasiliano yake, nenda hatua ya tano inayofuata hapo chini.

2. Kama hujapata jina wala mawasiliano ya mhusika weka biashara hiyo kwenye mpango wa kuendelea kufuatilia zaidi na endelea na wengine kwenye orodha uliyochagua.

3. Kwa biashara ambazo hujaweza kuwafikia watu sahihi, utaendelea kukusanya taarifa zake na kila wiki kuendelea kuwasiliana nao kwa namna tofauti mpaka umfikie mtu sahihi ambaye utaendelea naye kwenye mchakato wa mauzo.

Hatua ya tano; tafuta mawasiliano ya watu sahihi uliowapata.

Kama kwenye hatua ya nne hapo juu umepata jina la mhusika unayetaka kumfikia lakini hujapata mawasiliano yake, tumia hatua hii kutafuta mawasiliano ya kuweza kumfikia. Fuata mchakato huu kwenye kupata mawasiliano ya watu sahihi unaotaka kuwafikia;

1. Nenda sehemu ya kutafuta mtandaoni na andika jina la mtu na kampuni aliyopo kisha tafuta.

2. Matokeo yatakayokuja yatakuwa na taarifa za mtu huyo, hasa za mitandao ya kijamii anayotumia na kwenye maeneo mengine ambapo taarifa zake zinapatikana mtandaoni.

3. Ingia kwenye maeneo yenye taarifa zao na kama mawasiliano yao yanapatikana, yatumie kuwafikia moja kwa moja.

4. Kama mawasiliano yao hayapo moja kwa moja, ila kurasa zao za mitandao ya kijamii zipo, watumie ujumbe moja kwa moja kwenye mitandao hiyo ya kijamii wanayotumia kwa kufuata utaratibu wa kujitambulisha na kuomba miadi kama tulivyojifunza hapo juu.

5. Kama utayakosa mawasiliano kwenye kuwatafuta watu hao mtandaoni, rudi kuwasiliana na ofisi kwa mawasiliano uliyopata awali mpaka uweze kupata mawasiliano ya mhusika.

6. Pia unaweza kuwafuatilia watu hao kwenye mitandao ya kijamii na kuendelea kukusanya taarifa zao ili kuona njia bora ya kuweza kuwafikia.

Hatua ya sita; Mawasiliano au utembeleaji bila miadi.

Kama hatua zote za kutafuta mawasiliano ya wahusika na kuweka miadi zimeshindwa kuleta matunda, unapaswa kufanya bila ya miadi. Hapo unawasiliana na wahusika moja kwa moja baada ya kupata taarifa zao. Na kama hujapata mawasiliano, basi unatembelea eneo ambapo wanapatikana ili kukutana nao ana kwa ana, bila kuwa na miadi. Kwa kujua jina la mtu unayetaka kumfikia, unaweza kufika eneo wanalopatikana na kusema unataka kuonana nao, kwa kuonyesha una umuhimu wa kukutana naye, unaweza kupata nafasi.

Kama juhudi za kuwafikia wahusika moja kwa moja zitashindikana, unaweza kujiweka kama mteja wa biashara hiyo na kuomba kukutana na mtu wa mauzo. Kupitia mtu wa mauzo unaweza kumfikia yule unayemlenga, hasa kwa kuweka oda au kuomba mpango ambao mtu wa mauzo hawezi kuidhinisha mpaka mhusika unayemlenga ahusishwe.

Muhimu; unapotumia njia ya mtu wa mauzo epuka kudanganya kwamba unataka kununua ili tu umfikie mhusika. Badala yake fanya manunuzi ya kweli, kwa lengo la kumfikia mtu sahihi.

Hatua ya saba; Kuwa na ufuatiliaji wa msimamo.

Njia hii ya kuwafikia wateja kwa kutafuta taarifa zao mtandaoni na kuwatafuta huwa ina kukataliwa kwa ukubwa. Njia pekee ya kuvuka hilo na kupata matokeo mazuri ni kuwa na ufuatiliaji wa msimamo. Kama mtu unayemlenga ni mteja tarajiwa mwenye sifa, mweke kwenye ufuatiliaji endelevu bila ya kuchoka wala kukata tamaa.

Kadiri unavyofuatilia kwa muda mrefu zaidi, ndivyo fursa nzuri za kuwafikia na kuwashawishi zinavyopatikana. Utaweza kukusanya taarifa nyingi zinazowahusu na njia bora za kuwafikia.

Unahitaji kuwa na ubunifu kwenye utekelezaji wa mpango huu wa kutafuta wateja mtandaoni na kuwafuatilia ili uweze kupata matokeo mazuri. Kuwa imara pia ili kuvuka kukataliwa bila kukata tamaa ni hitaji muhimu kwenye njia hii.

Hatua za kuchukua.

Kwa kufuata mchakato huu wa kutumia mtandao wa intaneti kufikia wateja wengi, chukua hatua hizi;

1. Kila siku ya wiki chagua tasnia ambayo utatafuta watu na biashara zilizopo kwenye eneo fulani.

2. Chagua biashara na/au watu 10 ambao kwa taarifa za kutafuta unaona wanaendana na wateja tarajiwa unaowahitaji.

3. Fuata mchakato wa kuwasiliana kwa njia zinazopatikana mpaka kuhakikisha umeongea na watu wasiopungua 5.

4. Kwa mawasiliano ambayo umepata fuata mchakato wa kuwafikia watu sahihi na hakikisha unawafikia wasiopungua 3 kwa siku.

5. Weka miadi ya kukutana au kuwasiliana na watu sahihi na kuendelea na mchakato wako wa mauzo.

Fanyia kazi mpango huu kwa uhakika na utaweza kufikia watu wengi zaidi, kutengeneza wateja tarajiwa wenye sifa na kuwafuatilia mpaka kuwa wateja kamili.

Unapokuwa unaanzia chini na huna wateja wengi tarajiwa wa kuwafuatilia ili kukuza mauzo, huku pia ukiwa huwezi kumudu gharama za njia nyingine za kupata wateja kama matangazo, njia hii ya kutafuta mtandaoni inaweza kukupa matokeo mazuri. Unachopaswa ni kuifanyia kazi vizuri ili kupata wateja tarajiwa wenye sifa na kuweza kuwafuatilia kwa msimamo ili kukuza mauzo.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.