3500; Udhibiti uko wapi?

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Angalia wanafunzi hawa wawili, kisha uniambie ni yupi ana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa;

Mwanafunzi A; Kama mwalimu akitunga mtihani vizuri, nitafaulu.

Mwanafunzi B; Nimejiandaa vya kutosha, mtihani wowote utakaokuja nitafaulu.

Umeshapata picha ni mwanafunzi yupi atakuwa na nafasi kubwa ya kufaulu?

Iko wazi, ni mwanafunzi B.
Hiyo ni kwa sababu mwanafunzi B  ana udhibiti wa ndani wa mafanikio yake.
Wakati mwanafunzi A ana udhibiti wa nje.

Turudi kwako, udhibiti wako kwenye mafanikio uko wapi? Nje yako au ndani yako?

Kwa kuwa unajua udhibiti wa ndani ndiyo una mafanikio, unaweza kujidanganya kwamba una udhibiti wa ndani.

Wacha nikupe kipimo kimoja ambacho ukijijibu kwa uaminifu utaujua ukweli.

Turudi kwenye mfano wa wanafunzi.
Wamefanya mtihani, na wote wamefeli.
Mwanafunzi A anasema, mwalimu alitunga mtihani mgumu zaidi, ndiyo maana nimefeli.
Mwanafunzi B anasema, nilijiandaa vizuri, lakini siyo kwa viwango vilivyohitajika, wakati mwingine nitajiandaa vizuri zaidi.

Nadhani unapata picha nzuri hapo.
Turudi kwako, kumbuka matokeo mabaya ya mwisho kupata.
Iwe ni hasara kwenye biashara, kufukuzwa kazi, mahusiano kuvunjika n.k.
Je unatoa sababu gani ya kupata matokeo hayo mabaya?

Kama unasema wengine ndiyo sababu ya wewe kupata matokeo hayo mabaya, una udhibiti wa nje na huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Kama unasema wewe ndiye sababu ya wewe kupata matokeo hayo mabaya, una udhibiti wa ndani na utapata mafanikio makubwa.

Wajibika kwa kila kitu kwenye maisha yako, utakuwa na udhibiti wa ndani na kuweza kufanya makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com