3502; Acha kuhangaika na usumbufu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kuna vitu ambavyo watu huwa tunahangaika navyo na havina tija kabisa.

Zaidi vinakuwa ni usumbufu kwetu kwa sababu vinatutoa kwenye mambo ambayo ni muhimu zaidi kwetu.

Huwa kuna mjadala wa glasi yenye maji nusu, kwamba mtu anaona nini.

Je anaona glasi iliyojaa maji nusu?
Au anaona glasi ambayo iko tupu nusu?
Mjadala huo ni wa kupima kama mtu ana mtazamo chanya au hasi.

Kiuhalisia kuona glasi ina maji nusu au iko tupu nusu ni kujisumbua kwa jambo lisilo na tija.

Mjadala wenye tija ni;
Je maji yaliyo kwenye glasi yanafaa kutumia?
Je unawezaje kuijaza glasi hiyo?

Hapo sasa unakuwa unafikiria vitu ambavyo vinaweza kuleta matokeo ya tofauti.

Somo kubwa la kuondoka nalo hapa ni kuhakikisha hupotezi muda wako kwenye mijadala isiyokuwa na tija, hata kama inaonekana ni mizuri kiasi gani.

Kama mjadala wa iwapo unafikiria ndani au nje ya boksi, ondokana na hilo boksi kabisa, au litumie kwa matumizi yenye tija.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com