Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Maisha yetu hapa duniani huwa yanapitia mabadiliko makubwa ambayo huwa yanaathiri uwezo wetu wa kufanya shughuli za uzalishaji wa kipato. Tukiwa vijana huwa tunakuwa na nguvu za kuweka juhudi na kuingiza kipato kikubwa. Lakini muda unavyokwenda tunazeeka na nguvu zetu za kufanya kazi zinapungua.

Wakati uwezo wa kuingiza kipato ukiwa unapungua, matumizi yanakuwa yanaongezeka. Umri unapokwenda, gharama za maisha huwa zinapanda kwa sababu mbalimbali, binafsi na zinazohusisha wengine.

Kwa watu walio kwenye mfumo rasmi wa ajira huwa wanakatwa kwenye mishahara yao kwa ajili ya mafao baada ya kustaafu. Mpango wa kustaafu unaoendeshwa na taasisi za ustawi wa jamii umekuwa unahusisha mfanyakazi kuchangia kwa kipindi chote cha kazi yake. Ahadi ikiwa ni kwamba anapostaafu kazi yake, anakuwa na mafao yanayomwezesha kuendesha maisha yake.

Kwa nadharia mpango unakuwa hivyo na kuonekana ni mzuri na wenye manufaa. Lakini kiuhalisia mambo huwa ni tofauti kabisa na ilivyokuwa inategemewa. Wengi wamekuwa hawapati kiasi kikubwa cha fedha kama walivyotegemea na hivyo maisha yao kuathirika sana, hasa kwenye hicho kipindi ambacho hawawezi tena kuweka juhudi kubwa kwenye kazi.

Mabadiliko kwenye matokeo yanakuwa yametokana na kubadilika kwa sera mbalimbali za serikali kwenye kuendesha mifuko hiyo ya kijamii. Serikali imekuwa inaleta mabadiliko kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa namna ambayo wastaafu wanakuja kuhangaika sana.

Kumekuwa na mijadala na malalamiko mengi juu ya kikokotoo kinachotumika kwenye kuwalipa watu mafao yao. Utaratibu wa awali ulikuwa ni mtu anapostaafu kupewa sehemu kubwa ya mafao lakini hilo limebadilishwa na kuwa mstaafu kupata sehemu ndogo ya mafao yake.

Pia kumekuwa na mabadiliko kwenye kipindi ambacho mtu anaweza kuanza kutumia mafao ambayo amejiweka hata kama hajafikia kustaafu. Mabadiliko yamekuwa yanalenga kuanza kuwalipa watu baada ya kufika umri fulani.

Ukiangalia mabadiliko yote yanayofanywa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, nyuma yake yanasababishwa na kutokuwepo kwa fedha za kuwalipa wastaafu. Yaani mfuko unakuwa hauna fedha za kuwalipa wastaafu wengi kwa pamoja. Hivyo mabadiliko ya sheria na taratibu yanalenga kupunguza idadi ya wanaostahili kulipwa na hata kiasi cha kulipwa.

Mifuko ya hifadhi ya jamii inajikuta kwenye hali hiyo ya kushindwa kuwalipa wastaafu kwa sababu ya sera zisizo sahihi za uwekezaji. Mifuko hiyo imewekeza zaidi eneo la majengo, ambayo kwa sehemu kubwa ni ya shughuli za kijamii na marejesho ya uwekezaji huo siyo makubwa. Kwa mfano mifuko hiyo imewekeza kwenye kujenga majengo ya kupangisha kibiashara, lakini majengo hayo hayawi na wapangaji wa kutosha kuweza kurudisha gharama, kabla hata ya kuangalia faida.

Ili kuepuka changamoto hizi za kukwama kifedha wakati ambao umri wako umekwenda na uwezo wa kufanya shughuli za kipato umepungua, unapaswa kuwa na MPANGO BINAFSI WA KUSTAAFU. Mpango huo unahusisha kufanya uwekezaji ambao unaudhibiti wewe mwenyewe hivyo hakuna anayekupangia unapata kiasi gani na kwa wakati gani.

Mpango huo ni kwa watu wote, waliopo kwenye ajira rasmi ambapo wanakatwa michango ya mafao kwenye vipato vyao na kwa ambao hawapo kwenye ajira rasmi ambao hawana mifumo inayowalazimisha kukatwa michango ya mafao.

Lengo ni kwa kila mtu kuwa na uhakika wa kuwa na kipato cha kuyaendesha maisha yake hata kama hafanyi kazi ya kuingiza kipato moja kwa moja. Hili ni muhimu kwa watu wote, walio kwenye ajira na ambao hawapo kwenye ajira. Nasisitiza hilo kwa sababu walioajiriwa huona kwa sababu tayari wanakatwa, hawana haja ya kuwa na mpango wao binafsi. Ni mpaka unapofika wakati wa kupata mafao yao ndiyo wanagundua hawana uhuru nayo kama walivyodhani. Na kwa upande wa pili, ambao hawajaajiriwa huwa wanajisahau kwa kudhani wataweza kuendelea kuingiza kipato kwa kipindi chote cha maisha yao.

Hivyo tunachokubaliana ni kila mtu aliye hai anapaswa kuwa na mpango binafsi wa kustaafu ili kuwa huru pale anapokuwa hawezi au hataki tena kufanya shughuli za kuingiza kipato.

SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.

MCHAKATO WA KUTENGENEZA MPANGO BINAFSI WA KUSTAAFU.

Baada ya kukubaliana kwamba watu wote wanapaswa kuwa na mpango binafsi wa kustaafu, ufuatao ni mchakato wa kufuata kwenye kujitengenezea mpango huo.

1. Amua Umri Unaotaka Kuwa Umestaafu.

Kwa walioajiriwa, umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ni miaka 60. Hivyo unaweza kutumia huo iwe umeajiriwa au la, lakini pia unaweza kutumia umri mwingine, pungufu au zaidi ya huo.

Ukishachagua umri unaotaka kuwa umestaafu, kokotoa miaka iliyobaki kufika kipindi hicho. Kwa mfano kama unapanga kustaafu ukiwa na miaka 60 na sasa una miaka 40, miaka uliyobakiza ni 20, yaani 60 – 40.

2. Jua Gharama Za Maisha Kwenye Kipindi Hicho.

Kadiria gharama za maisha kuendesha maisha yako kwenye kipindi hicho cha kustaafu. Kwa sababu ya mfumuko wa bei ambao huwa unaendelea, thamani ya fedha ya sasa inakuwa imepungua kwa nusu kwa kipindi cha miaka 20. Yaani milioni 1 ya sasa inakuwa na thamani ya laki 5 miaka 20 ijayo. (Hii imekokotolewa kirahisi kwa kutumia kiwango cha mfumuko wa bei cha 4% kwa mwaka na kutumia kanuni ya 72 ya muda ambao thamani inakuwa mara mbili – 72/4 = 18).

Kwa mfano kama kwa sasa gharama za maisha ya mtu ni Tsh milioni 1, miaka 20 ijayo gharama za maisha zitakuwa Tsh milioni 2, hapo ni kama hajawa na mabadiliko makubwa kwenye mtindo wake wa maisha.

3. Jua Thamani Ya Uwekezaji Unaopaswa Kuwa Nao Kipindi Unastaafu.

Ili mtu kuweza kuingiza kipato cha kutosha kukidhi gharama za maisha na asimalize uwekezaji wake, anapaswa kuzidisha gharama zake za maisha mara 100. Hapa ni kwa makadirio kwamba mtu anaweza kupata marejesho ya angalau 1% ya uwekezaji aliona kwa mwezi.

Kwa mfano mtu ambaye gharama za maisha zitakuwa Tsh milioni 2, atapaswa kuwa na uwekezaji wenye thamani ya Tsh milioni 200 (2M x 100). Hicho ni kiwango ambacho mtu anapaswa kuwa tayari anacho pale anapostaafu ili aweze kuendesha maisha yake kwa kumudu gharama bila kulazimika kufanya kazi. Pia hatamaliza uwekezaji huo kwa kipindi chote cha maisha yake.

4. Kokotoa Kiasi Unachopaswa Kuwekeza Ili Kufikia Thamani Hiyo.

Baada ya kujia kiasi unachopaswa kuwa umefikia kwenye uwekezaji na muda uliobakisha mpaka kustaafu, unakokotoa kiasi gani unapaswa kuwekeza kila mwezi ili kufikia lengo. Anza kwa kukokotoa idadi ya miezi uliyonayo, kisha gawa uwekezaji unaopaswa kuwa nao kwa miezi hiyo.

Kwa mfano kwa miaka 20 ya kuwekeza, unapata miezi 240 (20 x 12 = 240). Kwa kiasi cha Tsh milioni 200 unayopaswa kuwa umewekeza, ukigawa kwa miezi unapata Tsh 833,333/=.

Kupata kiasi cha kuwekeza kila mwezi, gawa kiasi ulichopata kwa kuzidisha miaka ya kuwekeza kwa 2/10. Kwa miaka 20 ya kuwekeza, unazidisha miaka hiyo kwa 2/10 na kupata jibu la 4. Kisha unachukua Tsh 833,333/= na kugawa kwa 4, ambapo jibu unapata 208,333/=. Hicho kinakuwa ndiyo kiasi cha kuwekeza kila mwezi ili kufikia lengo.

5. Weka Mpango Wako Wa Uwekezaji.

Baada ya kujua kiasi unachopaswa kuwekeza kila mwezi, kinachofuata ni kuweka mpango wako wa uwekezaji.

Kwenye huu mpango binafsi wa kustaafu, kuna maeneo mawili tu ya kuwekeza.

Moja ni kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja inayosimamiwa na UTT AMIS. Hapa sababu ni urahisi wa kuwekeza na wingi wa mifuko ambayo mtu anaweza kuchagua. Kwa mfano unapofika muda wa kustaafu, unaweza kuhamisha fedha zako kutoka kwenye mifuko mingine na kupeleka kwenye mfuko wa BOND ambao una mpango wa kulipwa kila mwezi. Hapo unakuwa na uhakika wa kipato cha kila mwezi hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.

Mbili ni kuwekeza kwenye hatifungani za serikali za miaka 20 na kuendelea. Hapa sababu ni kiwango kizuri cha riba ambacho ni 15%, na hatari ndogo ya kupoteza kwenye uwekezaji huu.

Kuna aina nyingine nyingi za uwekezaji unazoweza kufanya na ukapata faida kubwa, lakini hizo utafanya kwenye mpango wako mwingine. Kamwe usiguse wala kuingilia mpango huu binafsi wa uwekezaji uliouweka .

Hata usikie kuna fursa nzuri kiasi gani, ifanye kwa utaratibu wako mwingine na siyo kuingilia mpango wako wa uwekezaji.

Kwa kuweka na kusimamia vizuri mpango wa uwekezaji, kila mtu, bila ya kujali kipato chake, anaweza kustaafu akiwa na uhuru wa kifedha.

Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2024 ambapo utakwenda kujifunza na kuweka mpango huu kwa vitendo kisha kusimamiwa kwenye kuutekeleza kwa msimamo bila kuacha. Tuma sasa ujumbe wenye maneno SEMINA 2024 kwenda namba 0713 604 101 upate nafasi ya kushiriki semina.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Kutoka sasa mpaka mwaka unaopanga kustaafu ni miaka mingapi?
2. Gharama za maisha kwa mwezi wakati umestaafu zitakuwa kiasi gani?

3. Ni thamani kiasi gani ya uwekezaji unapaswa kuwa nayo wakati unastaafu?

4. Ni kiasi gani unapaswa kuwekeza kila mwezi ili kufikia thamani hiyo?

5. Umepanga kufanya uwekezaji wako wapi?

6. Utajizuiaje usiache kuwekeza au kuingiliwa na tamaa nyingine na ukaharibu mpango wako?

7. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.