3503; Rasilimali zenye thamani.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Huwa tunahangaika na mambo mengi sana kwenye maisha.
Lakini rasilimali zenye thamani kubwa zaidi kwenye maisha yetu huwa hazibadiliki.

Kuwa na afya imara ni rasilimali ambayo thamani yake haitakuja kupungua kamwe.

Kuwa na mahusiano bora na watu wote unaojihusisha nao ni rasilimalu ambayo thamani yake inazidi kuwa kubwa kadiri muda unavyokwenda.

Kuwa huru kuyaishi maisha yako vile unavyotaka, kwa kuwa na uhuru wa kifedha ni rasilimali ambayo itaendelea kuyafanya maisha yako kuwa huru.

Kuwa na kusudi la maisha, linalokusukuma kuamka kila siku na kwenda kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora ni rasilimali itakayokuchochea mara zote.

Inashangaza sana pale tunapoharibu rasilimali hizi ambazo thamani yake haiishi, kwa kuhangaika kupata rasilimali ambazo thamani yake haidumu.

Kwa chochote tunachofanya kwenye maisha, tunapaswa kuhakikisha rasilimali hizo muhimu tunazilinda kwa gharama yoyote ile.

Hizo ni rasilimali ambazo tukizipoteza, hakuna tutakachopata ambacho kitakuwa na thamani zaidi ya rasilimali hizo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com