3504; Hawawezi kufanya kama wewe.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawapa watu hofu kwenye safari ya mafanikio ni kuigwa na wengine.
Watu hukazana kuficha mawazo yao na kuwa na siri kali kwenye yale wanayofanya kwa kuhofia wengine wakijua watawaiga na kuleta ushindani mkali kwao.
Ni kweli kwamba kuna watu wengi watakuiga kwenye kile unachofanya, hasa pale kitakapoonyesha mafanikio.
Lakini hilo halipaswi kukusumbua hata kidogo.
Kwa sababu watu wanaoiga, huwa wanakwama mahali pamoja, wanakuwa wameona kitu kwa nje ila uhalisia wa ndani hawaujui.
Wakiona kwa nje wanadhani ni rahisi.
Mpaka wanapoingia kufanya ndiyo wanagundua jinsi ilivyo vigumu kufanya kitu husika.
Na hata ikiwa rahisi kufanya, bado kunakuwa na changamoto nyingine, wanakuwa hawana msukumo mkubwa ndani yao wa kufanya.
Wanajikuta wakifanya tu kwa sababu ya kile walichoona kwa nje, lakini msukumo wa ndani wanakuwa hawana.
Hivyo wanapokutana na magumu na changamoto, ambavyo ni sehemu ya safari, huwa hawadumu kwa muda mrefu.
Lakini wewe ambaye kitu kimeanzia ndani yako kweli, unakuwa na msukumo mkubwa wa kukifanya.
Hata unapokutana na magumu na changamoto, unaendelea kufanya mpaka unayavuka na kufanikiwa.
Hili linakupa masomo makubwa mawili kuhusu mafanikio;
Moja ni kamwe usiige yale wanayofanya wengine. Badala yake anzia ndani yako mwenyewe. Unapoiga unakuwa na msukumo wa nje ambao hauna nguvu. Ila inapoanzia ndani yako, unakuwa na msukumo wa ndani wenye nguvu ya kuvuka kila changamoto.
Mbili ni wapuuze wale wanaokuiga, usihangaike hata kujua wanafanyaje, jua tu kwamba hawatadumu kwa muda mrefu. Na hata wakidumu, bado hilo halipaswi kukusumbua, kwa sababu wewe unaendelea kuwa bora kwenye hicho unachofanya.
Tambua kwamba hayupo anayeweza kufanya kile unachofanya kama unavyokifanya wewe.
Hivyo ushindi wa uhakika ni kuwa wewe kwenye kila unachofanya, kwa kuwa hakuna aliye kama wewe.
Rafiki, ni kwa namna gani umechagua kuwa wewe kwenye kile unachofanya sasa ili usisumbuliwe na wanaokuiga?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uweze kuwa wewe na kujitofautisha na wengine wote, kitu kitakachokuhakikishia mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe