3505; Majuto na Shauku.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio na neno hapana ni vitu vinavyokwenda pamoja mara zote.

Kama unataka mafanikio makubwa, unapaswa kulipenda neno hapana.
Kwa sababu neno hilo litakuwa linajirudia rudia sana kwenye maisha yako.

Neno hilo hapana lina sehemu mbili, kusema na kusikia.

Ili ufanikiwe unapaswa kuwa tayari kusema hapana bila ya majuto.
Ni lazima ukatae vitu vingi sana ili uweze kubaki na vichache vyenye tija kwako.

Kuwaambia wengine hapana siyo kitu rahisi, huwa kuna hali ya majuto huwa inaambatana na neno hilo.

Watu huwa siyo wazuri kwenye kupokea hapana, hivyo watakufanya ujione kama mkosaji sana kwa kuwakatalia kwenye yale wanayotaka.

Kama hutaweza kuvuka hali hiyo ya hatia ambayo watu wanakutengenezea, hutaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kuwa tayari kuwaambia watu hapana bila ya kuwa na hali yoyote ya majuto.
Hilo litakuepusha na mengi yanayokupoteza kwenye safari yako ya mafanikio.

Ili ufanikiwe, unahitaji kusikia hapana bila kupoteza shauku yako.
Kwenye safari yako ya mafanikio, utaambiwa sana neno hapana.

Mengi utakayokuwa unayataka kwa wengine, watakuambia hapana.
Kama utapoteza shauku yako pale unaposikia neno hapana, hutaweza kufanya makubwa.

Ukishakitaka kitu, unapaswa kung’ang’ana mpaka uweze kukipata.
Kila hapana unayoambiwa na wengine, inapaswa kukuchochea zaidi kutaka kupata hicho unachotaka.

Watu wanapokuambia hapana usione ni kama haiwezekani. Bali ona hujaweza kuwapa sababu sahihi za kukubaliana na wewe.

Badala ya kunywea pale unapoambiwa hapana, unapaswa kuwa na msukumo zaidi.

Kila unapoambiwa hapana, ongeza kasi zaidi kwenye hicho unachotaka.
Usikubali hapana ikuzuie kupata kile unachotaka.

Rafiki, umejipangaje kusema hapana bila ya majuto? Unahakikishaje kila hapana unayoambiwa inakuchochea zaidi kuliko kukukwamisha?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili uweze kutumia neno hapana kujijengea mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe