3509; Kitu pekee unachodhibiti.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kila mtu anapenda kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Lakini wengi hawajui ni kwa namna gani wanaweza kijihakikishia kupata mafanikio wanayoyataka.

Wengi wanajiendea tu na mambo vile yanavyoenda, wakiona hakuna wanachoweza kudhibiti.
Hawa hupokea kila aina ya matokeo wanayopata na hawapigi hatua kubwa.

Wengine wanakazana kudhibiti mambo yanavyoenda, wakiona kila kitu kiko chini ya udhibiti wao.
Hawa hukazana kubadili matokeo wanayopata kwa kutaka kudhibiti kila kitu.
Kwa sababu vitu vingi vipo nje ya udhibiti wao, huwa wanaishia kuchoka na hawapati matokeo makubwa.

Njia ya uhakika ya kufanikiwa ni kujua kile unachodhibiti na kukitumia vizuri kubadili matokeo ambayo mtu unayapata.

Kwenye safari ya mafanikio, kitu pekee ambacho mtu una udhibiti nacho kwa uhakika ni kazi unayoweka.

Juhudi unazoweka kwenye kutekeleza majukumu yako ya kazi zipo ndani ya udhibiti wako kabisa.
Juhudi hizo ndiyo zenye uwezo wa kubadili matokeo ambayo mtu anayapata.

Unaweza kusema mbona kuna watu wanafanya kazi sana lakini bado yawafanikiwi.
Ukweli ni kwamba siyo kila ufanyaji kazi utakupa mafanikio, ndiyo maana ni muhimu sana kuwa na udhibiti kwenye juhudi unazoweka.

Kwanza unapaswa kuwa na udhibiti kwenye vipaumbele vyako vya wapi unapeleka juhudi zako za kazi. Unapaswa kupeleka juhudi zako kwenye mambo machache muhimu zaidi na siyo kwenye kila kitu.

Pili unapaswa kuwa na udhibiti kwenye urefu wa muda wa kufanya kazi. Watu wengi wanatenga masaa kadhaa ya kufanya kazi kwenye siku na hawaendi zaidi ya hapo. Kupata matokeo makubwa ni lazima ufanye kazi kwa muda mrefu zaidi.

Tatu ni kasi na umakini wa kazi inayofanyika. Mtu anaweza kuchagua vipaumbele sahihi na akatemga masaa mengi ya kufanya kazi kwenye kila siku yake, lakini bado asipate matokeo makubwa. Hiyo inasababishwa na kuwa na kasi ndogo na kukosa umakini kwenye kazi. Kupata matokeo makubwa lazima uwe na kasi kubwa kwenye kazi na umakini wako uwe wa hali ya juu.
Kasi na umakini ndiyo vinafanya kazi ifanyike kwa tija. Masaa mengi unayokuwa umeyatumia kwenye kazi yanazalisha matokeo makubwa.

Ushahidi uko wazi kabisa kwamba wale wanaofanikiwa sana huwa wanafanya kazi kubwa na kwa muda mrefu kuliko ambao hawajafanikiwa.

Rafiki, ni udhibiti gani unaokwenda kuweka kwenye ufanyaji wako wa kazi ili uweze kupata matokeo makubwa?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uweze kubadili ufanyaji kazi wako na kufanikiwa zaidi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe