3511; Sikiliza Wanachokuambia.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu vigumu sana kwa watu kufanya kwenye maisha yao ni kutunza siri au kuficha vitu.

Kila kitu kuhusu mtu huwa kinajidhihirisha chenyewe.

Kama hataongea, basi ataonyesha kwa matendo.

Kama matendo yake hayaonyeshi basi historia yake ya nyuma itaonyesha kila alama na viashiria.

Hii ina maana kwamba kama tunaona watu wamebadilika, kwa kuwa tofauti na tulivyowadhania, siyo kwamba wamebadilika, bali ndivyo walivyo.

Na kama tutaona kwamba watu hao walituficha ukweli kuhusu wao, siyo kweli, kuna namna walikuwa wanatuambia ila hatukutaka kusikiliza.

Alama na viashiria vyote vilikuwa wazi kabisa, ila sisi wenyewe tulichagua kutokusikiliza wala kuzingatia.

Unaweza kudhihirisha hili wewe mwenyewe kwa kuangalia watu wote ambao umewahi kuona wamebadilika.
Utagundua kuna namna kile kilichokuja kujidhihirisha kilikuwepo kwa muda mrefu.
Lakini kwa sababu hukutaka kusikiliza, hukuweza kujua.

Hili ni baya zaidi pale hisia zinapoingia. Mtu anapompenda au kumkubali mtu, huwa hasikii wala haoni, hata kama vitu viko dhahiri kabisa.
Ni mpaka baadaye sana, akiwa ameshadhurika, ndiyo anakuja kuona kwamba mtu alikuwa hivyo tangu awali.

Wajibu wako kwenye maisha ni kusikiliza kwa makini, kwa masikio na macho ili uweze kuona uhalisia wa mambo badala ya kujidanganya kwa yale unayotaka kusikia au kuona wewe.

Rafiki, ni kwa namna gani kutokuwasikiliza watu kile wanachokuambia au kukuonyesha kumekugharimu?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili mara zote uwe makini kwenye kusikiliza kile watu wanakuambia.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe